Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raia wa Burundi alivyomchinja mtu na kupeleka kichwa uhamiaji

Muktasari:

  • Katika hukumu iliyotolewa Julai 6, 2026 na Jaji Augustine Rwizile na kuchapishwa Julai 9, 2026 katika tovuti ya Tanzania Legal Information Institute (TanzLII), Mahakama ilieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha kuwa mshtakiwa alisababisha kifo cha mwanaume ambaye hakufahamika kwa jina.



Kigoma. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imemtia hatiani raia wa Burundi, Ndaize Alfred kwa kosa la mauaji ya kudhamiria baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

Katika hukumu iliyotolewa Julai 6, 2026 na Jaji Augustine Rwizile na kuchapishwa Julai 9, 2026 katika tovuti ya Tanzania Legal Information Institute (TanzLII), Mahakama ilieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha kuwa mshtakiwa alisababisha kifo cha mwanaume ambaye hakufahamika kwa jina.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, tukio hilo lilitokea Septemba 19, 2025, wakati Ndaize alipofika katika Ofisi za Uhamiaji Kasulu akiwa amebeba begi lililokuwa na sehemu ya mwili wa marehemu.

Baada ya kuwafahamisha maofisa wa uhamiaji kuhusu tukio hilo, polisi waliitwa na kumkamata kwa ajili ya mahojiano.

Mahakama ilieleza kuwa baadaye siku hiyo, mshtakiwa aliwaongoza askari polisi, akifuatana na daktari pamoja na viongozi wa eneo husika, hadi Kijiji cha Mulubanga, wilayani Kasulu, ambako mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umefichwa.

Uchunguzi wa maiti uliofanywa na daktari ulionyesha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali.

Katika hatua za uchunguzi, mshtakiwa alitoa maelezo ya ungamo yaliyorekodiwa kwa mujibu wa sheria, akieleza kuwa alimuua marehemu akidai alikuwa akimuibia.

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, alifikishwa Mahakama Kuu kujibu shtaka la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa Serikali Fortunatus Malicha na Stephano Nyogoto, huku Anthony Kigonga akisimamia utetezi wa mshtakiwa.


Alivyojibu shtaka

Katika mwenendo wa kesi, mshtakiwa hakupinga kuwa alisababisha kifo cha marehemu, lakini alidai wakati wa tukio alikuwa na tatizo la afya ya akili.

Kutokana na hoja hiyo, mahakama iliamuru apelekwe katika Taasisi ya Isanga kwa uchunguzi wa afya ya akili.

Hata hivyo, Aprili 24, 2026, ripoti ya kitabibu iliwasilishwa mahakamani ikionyesha kuwa hakuwa na tatizo la afya ya akili wakati wa kutenda kosa, hivyo kesi ikaendelea kusikilizwa kama ilivyo.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alidai kuwa kabla ya tukio hilo alikuwa amekuwa akikumbwa na vitendo vya wizi na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa watu wasiojulikana.

Alidai watu hao waliwahi kuiba mazao na mifugo yake, kuchoma nyumba yake na kumshambulia mara kadhaa, huku akisema baadhi ya matukio hayo aliyawasilisha kwa mamlaka bila mafanikio ya kuwabaini wahusika.

Alidai kuwa usiku wa tukio alisikia watu nje ya nyumba yake na kushambuliwa, ndipo akajihami kwa kutumia panga. Baadaye aligundua kuwa mmoja wa watu hao ameanguka na akaendelea kumshambulia akiamini kuwa alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakimsumbua kwa muda mrefu.


Mahakama ilivyoamua

Akitoa hukumu, Jaji Rwizile alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, vielelezo vilivyowasilishwa na maelezo ya mshtakiwa mwenyewe vinaonyesha pasipo shaka kuwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu.

Alisema pia ushahidi ulionyesha kuwa baada ya tukio, mshtakiwa aliwaongoza polisi hadi eneo ambako mwili wa marehemu ulikuwa umefichwa.

Kuhusu hoja ya kutokuwa na afya njema ya akili, Jaji alisema utetezi haukuwasilisha ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo, huku ripoti ya daktari ikionyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na utimamu wa akili wakati wa kutenda kosa.

Mahakama pia ilikataa hoja ya kwamba kitendo hicho kilitokana na hasira pekee.

Jaji alisema mazingira ya tukio, aina ya silaha iliyotumika, sehemu ya mwili iliyoathiriwa, pamoja na mwenendo wa mshtakiwa baada ya tukio, vinaonyesha kuwepo kwa dhamira ya kuua.

"Baada ya kuzingatia ushahidi wote uliopo, Mahakama imeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hili pasipo kuacha shaka yoyote," alisema Jaji Rwizile.

Kutokana na sababu hizo, mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji ya kudhamiria.

Hukumu hiyo haikuonyesha adhabu aliyopangiwa mshtakiwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, adhabu ya kosa la mauaji ni kifo.