Shaka ampa tano Rais Samia
Rais Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kioo cha uongozi anayefuata nyao za waasisi wa Umoja wa Afrika (AU), katika kuleta umoja na mshikamano kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kioo cha uongozi anayefuata nyao za waasisi wa Umoja wa Afrika (AU), katika kuleta umoja na mshikamano kwa Watanzania.
Shaka ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC), amesema hayo leo Alhamisi Julai 5, 2023 katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zilizofanyika viwanja vya Magubike wilayani humo.
Amewataja waanzilishi hao, wakiwemo hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume (Tanzania) Dk. Kwame Nkurumah (Ghana), Jomo Kenyatta (Kenya), Gamal Abdi Naaser (Misri), na Ahmed Sekeu Toure (Guine) ambao ni vioo vya uongozi unaopaswa kuigwa.
"Wazee hawa walifanya kazi kubwa katika kuimarisha umoja na upendo kwenye nchi zao na Afrika kwa ujumla. Waliyafanya hayo kwa uadilifu, uaminifu na kujitolea wakati wote na Rais Samia amekuwa akipita kwenye njia hiyo hiyo kwa vitendo” amesema Shaka.
Amesema Serikali inapambana kuimarisha maisha ya Watanzania, kuhimiza usawa na haki, kutanua wigo wa demokrasia na ushirikishwaji wananchi kwa kuwataka kujituma zaidi hususan katika uzalishaji mali ili kujikwamua kiuchumi.
"Wahenga wetu wana kioo cha mtu ni mtu, kila mmoja ajipime, ajitathmini na kujitambua kutokana na usahihi wa mwenzake. Aina ya uongozi wa Rais Samia ndiyo unaohitajika katika kuwatumikia awanyonge,”amesema Shaka.
Shaka amewataka wananchi, viongozi wa kisiasa, mashirika yasiyokuwa ya Kkiserikali, madhehebu ya dini na makundi mengine ya kijamii kusimama imara kuunga mkono juhudi za Serikali ya katika mapambano ya kuimarisha uchumi ili kuharakisha maendeleo ya Watanzania.