Shaka: CCM haitakufa, ni imara nyakati zote

Muktasari:

  • Februari 5, Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafikisha maiaka 45 tangu vyama vya Tanu na ASP vilipoungana mwaka 1977 na kuzaliwa kwa chama kipya cha CCM. Chama hicho kimeendelea kuongiza nchi tangu uhuru.

Musoma. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema chama hicho hakiwezi kufa badala yake kitaendelea kuimarika na kuwa chama imara na bora miaka yote.

Shaka ametoa kauli hiyo mjini hapa leo Januari 14, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua maandalizi ya maadhimisho ya miaka 45 ya CCM yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma mkoani Mara.

Amesema wale wanaodhani chama hicho kitakufa wasahau kwa sababu chama kimekuwa kikiimarika siku hadi siku na kwamba hakina mpango wa kufa siku za usoni.

“Hiki chama ndicho chama pekee chenye kujielewa kwani kinajua kilipotoka, kilipo na kinapokwenda ila hakijui kitakufa lini kwani mpango huo haupo kabisa,” amesema Shaka.

Amebainisha kwamba viongozi wa chama ndiyo watakaokufa kwa mapenzi ya Mungu na kuongeza kuwa kabla hawajafa hivi sasa kazi ya kukijenga chama zinaendelea ikiwa ni pamoja na kurithisha vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Kama kawaida viongozi wa chama hiki ni binadamu, kwa hiyo suala la kifo halikwepeki lakini tumejiwekea utaratibu wa kujenga chama imara kwa kurithishana vizazi na vizazi ili kuwepo na uendelevu,” amesema.

Shaka amewataka wanachama wa CCM kuhakikiaha kuwa wanafanya uchaguzi kwa uadilifu ili kuonyesha ukomavu ndani ya chama na kwamba kamwe uongozi hautavumilia vitendo vya rushwa na udhalilishaji katika mchakato wa uchaguzi ndani ya chama.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara,  Samwel Kiboye amesema kuwa maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea vizuri huku akisema wanachama wa CCM mkoa wa Mara wanatambua na kuthamini jitihada zimazofanywa na mwenyekiti wa chama hicho taifa , Samia Suluhu Hassan za kuleta maendeleo nchini.