Sheikh wa Mkoa wa Dodoma ataka watu wasife kizembe

Muktasari:

Sheikh Mustafa amesema kuna watu wanakufa kwa sababu ya kukaidi maagizo ya wataalamu wa afya na viongozi wa Serikali.

Dodoma. Watanzania wametakiwa kuchukua tafadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 ili wasife kizembe.

Wito huo umetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab katika swala ya Eid Al Adha alipoongoza mamia ya waumini katika msikiti wa Gaddafi Jijini Dodoma.

Sheikh Mustafa amesme suala la kuchukua tafadhari kwa Watanzania na waumini wa dini ya kiislamu halipaswi kupuuzwa.

Amesema kuna vifo ambavyo husababishwa na uzembe hasa pale mtu anaposhindwa kuchukua tahadhari hata anapoambiwa na wataalamu badala yake watu wanaishia kulalamika.

Kiongozi huyo ameagiza misikiti yote kuwakumbusha waislamu kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono kila inapobidi.

"Lakini msitumie siku ya leo kubadili maudhui yake, leo ni siku ya kuchinja isiwe ya kufanya matendo maovu ya kumchukiza Mwenyezi Mungu, nendeni mkasaidie wasiojiweza na kuwahurumia masikini," amesema Sheikh Mustafa.

Katika uwanja wa Jamhuri, Sheikh Abdul Mussa Kondo amewataka Watanzania kuwa makini kwa kuwa dunia inapita katika kipindi kigumu zaidi.

Sheikh Kondo amesema ni wakati kwa wataalam na madaktari kutumia mbinu zote katika uchunguzi ili watoke hadharani kueleza kuhusu chanjo.

Amesema gonjwa la Covid-19 halichagui dini wala rangi ya mtu hivyo mapambano yake yanapaswa kuanzia kwa jamii kwa mashirikiano na kumuomba Mungu kwani hakuna maradhi yasiyokuwa na tiba.