Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria aliyoikosoa Ndugai kufumuliwa, Waziri Mkuu asema...

Muktasari:

  • Sheria hiyo ni ile ambayo aliyekuwa Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai, aliwahi kuhoji kuwa wakati inapitishwa huenda alikuwa amesinzia au kulala.



Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza kutekelezwa mara moja kwa uamuzi wa mahakama kwa wafugaji walioshinda kesi za mifugo iliyotaifishwa, akisema endapo mifugo hiyo haipo, wahusika walipwe fidia stahiki.

Aidha, amesema Serikali itawasilisha bungeni katika mkutano ujao unaotarajiwa kuanza Agosti 25, 2026, muswada wa marekebisho ya sheria inayosimamia utaifishaji wa mifugo na mali zinazokutwa katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Sheria hiyo ni ile ambayo aliyekuwa Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai (marehemu), aliwahi kuhoji kuwa wakati inapitishwa huenda alikuwa amesinzia au kulala, huku akisema sheria hiyo ni ya kinyonyaji na dhuluma.

Akizungumza leo Ijumaa, Juni 26, 2026, wakati akiwasilisha hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge, Dk Mwigulu amesema kuna baadhi ya wafugaji walioshinda kesi ya kutaifishwa kwa mifugo yao, lakini bado hawajapata haki zao kwa kuelezwa kuwa mifugo yao ilikufa baada ya kutaifishwa.

"Naiagiza Wizara ya Fedha ikae pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mifugo kushughulikia kadhia hii. Kama watu wameshinda kesi, kwa nini wasilipwe haki zao?" amehoji Dk Mwigulu.

Amesema sheria hiyo imekuwa ikitumika vibaya na baadhi ya watu wasiowaaminifu kuwanyang'anya wananchi mifugo yao, hivyo Serikali imeamua kuifanyia marekebisho ili kuondoa upungufu uliopo.

"Serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria zinazosimamia utaifishaji wa mifugo na mali katika maeneo yaliyohifadhiwa, ikiwemo kuondoa utaratibu wa kutaifisha mifugo ya Watanzania inapokutwa katika maeneo hayo," alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo amepiga marufuku tabia ya kuwafukuza wafanyabiashara wadogo bila kuwapatia maeneo mbadala yanayofaa kwa shughuli zao.

Amesema mamlaka husika zinapaswa kutenga maeneo rafiki yatakayowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea kujipatia kipato.


Awagusa wanaosubiri teuzi

Dk Mwigulu pia amekosoa baadhi ya viongozi wanaodaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu ya kusubiri uteuzi wa nafasi nyingine.

Amesema viongozi wote wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na ufanisi, akisisitiza kuwa watakaobainika kutotekeleza wajibu wao hawastahili kuendelea kushika nafasi hizo.

Kuhusu migogoro ya ardhi, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa ngazi za chini kuitatua mapema badala ya kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa.

Pia, ameagiza watendaji kuacha kushikilia vitendea kazi vya wajasiriamali wakati wa uchunguzi wa makosa yanayoweza kupewa dhamana, akisema hatua hiyo huwanyima wananchi fursa ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Wakati huohuo, amesema Serikali itawasilisha pia marekebisho ya sheria yatakayowezesha Makamu Wenyeviti wa Halmashauri na Manaibu Meya kuchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano badala ya mfumo wa sasa wa uchaguzi wa kila mwaka.

Amesema lengo ni kupunguza kampeni za mara kwa mara na migogoro inayojitokeza katika halmashauri.


Serikali yasisitiza kulinda amani

Akizungumzia hali ya usalama nchini, Dk Mwigulu amesema Serikali haitamvumilia mtu au kundi lolote litakalojaribu kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

"Serikali iko imara katika kulinda amani, usalama na umoja wa Tanzania. Haitaruhusu mtu yeyote au kikundi chochote kutumia Watanzania, hususan vijana na watoto, kwa maslahi binafsi yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi," alisema.

Ameongeza kuwa vyombo vya dola vitaendelea kufuatilia watu na makundi yanayodaiwa kupanga au kufadhili vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, pamoja na mawasiliano yanayofanyika kupitia mitandao ya kijamii.


Zungu akiahirisha mkutano

Naye Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kufuatilia taarifa za baadhi ya watendaji wanaodaiwa kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kushindwa kufuatilia na kukamilisha taratibu za upatikanaji wa mikopo hiyo.

Akiahirisha mkutano huo wa Bunge, Zungu amesema haikubaliki kwa baadhi ya watendaji kufanya kazi kwa kusuasua wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Amesema zipo taarifa za watendaji wanaodaiwa kuchelewesha utekelezaji wa miradi kwa kushindwa kufuatilia taratibu mbalimbali, ikiwemo kukamilisha hatua zinazohitajika ili mikopo ya maendeleo ipatikane kwa wakati.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka Kamati ya Bajeti kufuatilia kwa karibu suala hilo na kubaini sababu zinazokwamisha utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kufadhiliwa kwa mikopo.

Wakati huohuo, Zungu amewataka watendaji wa Serikali kuiga mfano wa Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ambaye amesema alifanya juhudi kuhakikisha Serikali inapata mkopo kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

Amesema mkopo huo utalipwa ndani ya kipindi cha miaka 40 na umelenga kuimarisha sekta ya afya nchini.

Aidha, Spika ameonya kuwa haikubaliki baadhi ya mikopo ya maendeleo iliyoombwa kushindwa kutumika kwa sababu ya watendaji kuchelewesha au kutokamilisha hatua za mwisho za kiutawala, ikiwemo kusaini nyaraka zinazohitajika