Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria za uchaguzi zaanza kufumuliwa

Dar/Moshi. Wakati Serikali ikianza mchakato wa mabadiliko ya sheria zinazohusu uchaguzi, wadau wameibuka wakihoji nini kilipaswa kutangulia kati ya suala hilo na Katiba mpya.

Hoja hiyo ya wadau inatokana na hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuvitumia barua baadhi ya vyama vya siasa, ikivitaka kutoa maoni na mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria nne.

Sheria hizo ni ile ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, Sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi sura ya 278.

Hayo yanafanyika ikiwa ni takriban mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na miaka miwili kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Barua hiyo ya Juni 10 mwaka huu, inawataka makatibu wa vyama kuwasilisha maoni katika sheria hizo zinazosimamiwa na ofisi ya msajili kabla ya Julai 20, mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyotiwa saini na Sisty Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, mapendekezo yajielekeze katika kubainisha jina la Tume ya Uchaguzi, majukumu yake na utaratibu wa uteuzi na utenguzi wa wajumbe wa Tume hiyo.

Mambo mengine ni kubainisha chanzo cha fedha za uendeshaji wa Tume na shughuli za uchaguzi, kuainisha muundo wa utumishi wa tume hiyo na kuipa mamlaka ya kutunga kanuni, miongozo na maelekezo.

Katika marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, barua hiyo ambayo Mwananchi imeiona inasema mambo ya kuzingatia ni pamoja na kuweka sharti kwamba mtu ambaye amepatikana na hatia ya kosa la udhalilishaji wa jinsia asiwe kiongozi wa chama cha siasa hapa Tanzania.

Pia maoni hayo yazingatie kuruhusu fedha za ruzuku kugawanywa kwa vyama vya siasa kwa kuzingatia idadi ya kura za ubunge, idadi ya wabunge na madiwani ambao kinao kwa wakati husika na badala ya kura za ubunge au madiwani.

Mchakato huo umekuja wakati wadau wa uchaguzi, vikiwamo vyama vya siasa, ikiwamo Chadema, wakishikilia msimamo kuwa mwaka 2020 hapakuwa na uchaguzi huru na haki.

Hata ule wa Serikali za mitaa wa 2019, nao unakosolewa kwa kutawaliwa na matukio ya wagombea wa upinzani kuenguliwa na mawakala wao kuzuiwa vituoni.

Kutokana na matukio hayo, kutungwa kwa sheria mpya za uchaguzi ni ishara ya kupatikana kwa Tume Huru, hali inayoweza kuwa mwanzo kuelekea kwenye uchaguzi huru.

Machi 29 mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha vifungu vya sheria vinavyoruhusu wagombea kupita bila kupingwa, ikisema vinakiuka ibara ya 21 (1) na (2) vya Katiba.

Kutokana na wito huo wa msajili, Katibu mkuu wa Chama cha Chadema, John Mnyika alipoulizwa na gazeti hili, alisema suluhisho lingekuwa ama kuanza na Katiba mpya au marekebisho ya Katiba ya sasa ili kutibu matatizo ya kiuchaguzi.

Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani, kilishaweka msimamo wake kwamba hakitakubali kuingia katika uchaguzi mkuu ujao kupitia Katiba ya sasa yenye maudhui ya chama kimoja.

Mnyika alisema matatizo ya kiuchaguzi ni ya kikatiba, hivyo marekebisho ya sheria ya uchaguzi hayawezi kuyatatua kabla ya kuanza ama Katiba mpya au marekebisho ya Katiba ya 1977 kabla ya kupokea maoni.

“Kutaka maoni kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ni kurudia kazi ambayo ilishafanywa na kikosi kazi, hivyo ni mbinu ya kuchelewesha kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya,” alisema Mnyika kupitia ujumbe wake wa maandishi.

“Pia hii ni kukwepesha haja ya kufanyika kwa marekebisho ya mpito ya kikatiba kuwezesha uchaguzi huru na haki. Katika wakati muafaka chama kitatoa tamko la kina juu ya hatua hii ya msajili wa vyama vya siasa yenye nia mbaya,” alisema.

Akisisitiza msimamo huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema hawana mpango wa kushughulika na barua ya msajili.

Alisema ujumbe wa chama hicho upo kwenye mazungumzo na Serikali kuhusu masuala hayo na kwamba Mwenyekiti, Freeman Mbowe atazungumza na Watanzania kueleza hatua iliyofikiwa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini alisema wadau wa demokrasia ni wengi hivyo wangependa ukusanyaji wa maoni uhusishe Watanzania wengi kwa sababu sheria hizo na uamuzi wake utawagusa.

“Watanzania kwa mujibu wa Katiba wanapiga kura kuchagua viongozi na wanaweza kupigiwa kura. Sasa vyama vya siasa haviwezi kuwa na umiliki wa haki hiyo peke yake. Ni muhimu Watanzania waulizwe kwa sababu hili litawahusu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu maoni ya wadau hao, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alijibu kwa kifupi, “tutashughulikia.”

Selasini alisema haiwezekani kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo Rais anaendelea kuteua mwenyekiti au makamishina kwa kuwa ni lazima wataendelea kuchagua makada wenzao.

Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohammed Ngulangwa alisema hakuna mawazo mapya yanayokwenda kutolewa.

Kinachopendekezwa, alisema ni kilekile ambacho mara zote vyama vya siasa vimekuwa vikipendekeza hata kupitia michakato mbalimbali ya kutoa maoni, kikiwemo kikosi kazi.

Kwa upande wa ACT Wazalendo, Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji alisema wao kupitia majukwaa mbalimbali walishatoa maoni kuhusu namna wanavyotaka tume huru ya uchaguzi iwe.

“Tunaona kama kuna hatua zinachukuliwa, lakini nakumbuka tulishawahi kupeleka maoni yetu hata kwenye kikosi kazi, yalikuwa maoni mengi mno,” alisema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema alisema barua zinakwenda ofisi ya katibu mkuu huku akiomba atafutwe Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo ambaye hata hivyo, hakupatikana kupitia simu yake ya kiganjani na ujumbe mfupi wa maandishi aliotumiwa haukujibiwa.


Ni jambo jema

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kinachofanyika ni jambo jema na inaonyesha nia ya dhati ya marekebisho ya sheria hizo.

“Kwa sababu Rais (Samia Suluhu Hassan) alishaelekeza kuwepo na uhuru wa mikutano ya kisiasa, sheria kubadilishwa na mchakato wa Katiba kuanza na vyote hivi vinafanyika, ni dalili nzuri,” alisema.

Hata hivyo, Dk Lazzaro Swai, mhadhiri wa rasilimali watu alisema jambo muhimu ni kusimamiwa kwa mchakato huo kuhakikisha kinachotarajiwa ndicho kinachopatikana.