Watanzania 74,642 kuchagua madiwani kesho

Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Watanzania 74,642 kesho watatumia haki yao kikatiba kuchagua madiwani katika uchaguzi mdogo kwenye kata 13 za Tanzania Bara.
Dar es Salaam. Watanzania 74,642 kesho watatumia vituo 205 kuchagua madiwani katika uchaguzi mdogo kwenye kata 13 za Tanzania Bara ikiwa ni njia itambuliwayo kisheria, katika kujaza nafasi za madiwani zilizokuwa wazi.
Wapiga kura hao ni wenye sifa za kupiga kura ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 12, 2023, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Jacobs Mwambegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Jaji Mwambegelea ameshauri kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi huo.
“Jukumu la kulinda amani ya nchi yetu ni la kila mmoja wetu wakiwemo wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema uchaguzi huo utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
“Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifika kabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo wa NEC amevikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo mdogo, kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura.
Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292, imeruhusu wapiga kura waliopoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.
Uchaguzi huo mdogo utafanyika kwenye kata na halmashauri kwenye mabano; Ngoywa (Sikonge), Kalola (Uyui), Sindeni (Handeni).
Pia kuna Kata ya Potwe (Muheza), Kwashemshi (Korogwe), Bosha (Mkinga), Mahege (Kibiti), Bunamhala (Bariadi), Njoro na Kalemawe (Same), Kinyika (Makete), Magubike (Kilosa), na Mbede (Mpimbwe).