CCM yaanza kampeni

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi (kulia) akimnadi mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Njoro wilayani Same, Omari Abdallah. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Kata ya Njoro ni miongoni mwa kata 14 za Tanzania Bara, zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya uchaguzi mdogo wa madiwani, ambao unatarajiwa kufanyika Julai 13, mwaka huu.
Same. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kampeni za udiwani katika Kata ya Njoro, Wilaya ya Same na kumnadi mgombea wake, Omari Abdallah huku Chadema kikiendelea kusimamia msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi kwa madai hadi itakapopatikana Katiba Mpya.
Mbali na CCM vyama vingine vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huo ni Chama cha NCCR Mageuzi, ADC na TLP na kata hiyo inarudia uchaguzi, baada ya diwani aliyekuwepo, kufariki dunia.
Wakati vyama hivyo vikijitokeza katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Same, Rockson Kashamba amesema hawawezi kushiriki uchaguzi huo, kwa kuwa chama kilishatoa tamko la kutoshiriki chaguzi mpaka itakapopatikana katiba mpya.
"Ni kweli kutafanyika uchaguzi mdogo Kata ya Njoro na Kalemawe Wilaya ya Same, lakini Chadema kupitia mwenyekiti wetu Taifa, alishatoa tamko, kuwa hatutashiriki uchaguzi hadi ipatikane katiba mpya. Hivyo hatushiriki uchaguzi mdogo kwa kuwa hakuna kilichobadilika kutoka uchaguzi mkuu uliopita, hivyo maridhiano ya kikatiba ndiyo yatakayotufanya tushiriki uchaguzi wowote katika nchi hii,"amesema Kashimba.
Akizungumza leo Julai 3, 2023 katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni, Abdallah amesema anazifahamu vyema changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, hivyo akishinda atashirikiana kikamilifu na watendaji wa halmashauri pamoja na mbunge wa jimbo hilo, Dk Mathayo David ili kuzitafutia ufumbuzi.
"Nafahamu zipo changamoto hapa Njoro ikiwemo ya upatikanaji wa maji na hii itatatuliwa siku si nyingi kwani mradi mkubwa wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe unaendelea vizuri, pia baadhi ya maeneo wananchi hamjafikiwa na umeme, nipeni nafasi nikawatumikie na kuhakikisha changamoto hizi zinakwisha," amesena Abdallah.
Ameongeza kuwa, "Pia, nafahamu kuna tatizo la uvamizi wa tembo katika Mashamba ya watu na kwa sasa wananchi wako mashambani wakilinda mazao yao pamoja na changamoto ya barabara inayounganisha Kijiji cha Emuguri na Njoro, nitafanyia kazi haya kwa kushirikiana na Mbunge na watendaji, msifanye makosa Julai 13."
Akimnadi mgombea huyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema Abdallah ni mwanasheria na kuwaomba wananchi kumchagua ili akashirikiane na serikali kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika kata hiyo.
Aidha Boisafi ametumia pia mkutano huo kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa usahihi, ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.
"Tulipofikia Watanzania, hatupaswi kufanya kazi kwa kusukumwa, mnaona miradi ya elimu, afya, barabara na mingine ikitekelezwa kwa kasi, kila mmoja atekeleze wajibu wake kikamilifu na wale wanaotakiwa kulipa kodi wailipe kwa usahihi ili kuwezesha utekekezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa," amesema.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amewaomba wananchi kuendelea kukiamini chama hicho na kumchagua Abdallah ili akashirikiane na serikali kuwaletea maendeleo.
"Tunaomba wananchi mwendelee kutuamini na mpeni nafasi mgombea udiwani wa CCM, ili kuiendeleza kata hii kimaendeleo, kwani huwezi kuweka kiraka cheupe kwenye nguo nyeusi halafu ukategemea ikae sawa, tupeni diwani akashirikiane na Mbunge na Rais kuleta maendeleo ya kweli," amesema.
Kata ya Njoro ni miongoni mwa Kata 14 za Tanzania Bara, zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya uchaguzi mdogo wa madiwani, ambao unatarajiwa kufanyika Julai 13, mwaka huu.
Kata hiyo ina jumla ya wapigakura 2,495, ambao wanatarajiwa kupiga kura Julai 13, mwaka huu, kumchagua diwani wa kata hiyo.