Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria hifadhi ya jamii kurekebishwa

Muktasari:

Serikali yapendekeza kurejesha utaratibu waliojiajiri kujiunga.

Dodoma. Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii unaopendekeza watu waliojiajiri katika sekta binafsi kujiunga na kufaidika na mafao katika mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria.

 Utaratibu unaofanana na huu uliwahi kuwepo kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018 na kuunda mifuko miwili; Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Uchangiaji ulikuwa ukifahamika kama uchangiaji wa hiari uliowezesha Watanzania wote waliokosa fursa hiyo na wanaohitaji kupata huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni jana kwa mara ya kwanza, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameupeleka kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuuchambua.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako anapendekeza marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii.

Amesema lengo la marekebisho ni kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa watu waliojiajiri.

Pia kifungu cha 12(1) cha muswada huo kinapendekezwa kurekebishwa, ili kuainisha asilimia za kiwango cha uchangiaji kinachopaswa kuwasilishwa na mwajiri kwenye mfuko.

Amesema kifungu cha 12(3) kinapendekezwa kufutwa, ili kuruhusu mwajiri kuchangia kwa kiasi kikubwa au kiasi chote.

Profesa Ndalichako amesema kifungu cha 12(5) kinapendekezwa kurekebishwa kuainisha namna ya uchangiaji kwa wanachama waliojiajiri.

Kifungu cha 12A kinapendekezwa kuongezwa ili kuruhusu mfanyakazi aliyeajiriwa na mwajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na waajiri wote kwa ridhaa yake. Lengo la marekebisho haya ni kumpa mwanachama uhuru wa kuchangiwa na zaidi ya mwajiri mmoja.

Pia, kifungu cha 23 kinapendekezwa kufutwa na kuandikwa upya, ili kuruhusu michango iliyowekwa na mwanachama baada ya umri wa kustaafu hadi kufikia miaka 70 kuzingatiwa katika ukokotoaji wa malipo ya mafao ya pensheni.

Amesema lengo la marekebisho haya ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa mafao ya pensheni kwa mwanachama ambaye amefikisha umri wa kustaafu, lakini hajakidhi vigezo vya kupata pensheni na amekuwa akichangia kuanzia umri wa miaka 61 mpaka 70.

Vifungu vingine vinavyopendekezwa kurekebishwa ni vya 52 na 76, lengo likiwa ni kumruhusu mwanachama ambaye hajafikia umri wa kustaafu kutumia sehemu ya mafao yake kama dhamana kwa mkopo wa nyumba.

“Lengo la marekebisho haya ni kutoa ufafanuzi kwa kuwa vifungu hivyo vinazuia matumizi ya mafao kama dhamana ya mkopo isipokuwa kwa mkopo wa nyumba kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 20,” amesema Profesa Ndalichako.


Pia amesema kifungu cha 90 kinapendekezwa kurekebishwa, ili kuyajumuisha mafao yanayolipwa chini ya sheria hiyo kwenye orodha ya masuala yasiyopaswa kutozwa kodi kama ilivyoorodheshwa katika kifungu hicho.

Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuzuia utozaji wa kodi mara mbili kwenye mafao yanayolipwa chini ya sheria.

Marekebisho sheria tatu

Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2024 uliwasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni jana, Februari 15, 2024 unapendekeza marekebisho katika sheria tatu.

Muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usimamizi na Maendeleo ya Uvuvi wa Bahari Kuu; Sheria ya Madini, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania.

Katika marekebisho ya Sheria ya Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amependekeza marekebisho katika kifungu cha 73, ili kutofautisha leseni za wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite na wafanyabiashara wa madini ya vito vingine vya rangi.

“Lengo la marekebisho haya ni kuweka udhibiti wa madini ya Tanzanite kwa namna maalumu na kuyatangaza kwa kuzingatia uwepo wa madini hayo wa kipekee nchini Tanzania,”amesema.

Amesema kifungu cha 86A kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho, muingizaji wa madini nchini hatatakiwa kulipa mirabaha kwa madini yanayoingizwa nchini endapo atathibitisha kuwa amelipa mirabaha katika nchi yalikotoka.

Amesema lengo la marekebisho ni kuepusha ulipaji wa mirabaha zaidi ya mara moja.

Pia amependekeza kifungu cha 87 kufanyiwa marekebisho kwa kuongeza viwango vya mirabaha inayopaswa kulipwa serikalini na wafanyabiashara wa madini ya vito yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi ambayo yamenunuliwa katika minada ya madini na maonyesho ya kimataifa ya madini ya vito.


Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka katika shughuli za madini.

Dk Feleshi amesema kifungu cha 90A kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuondoa masharti kuhusu ukaguzi kwa madini yanayouzwa wakati wa mnada wa madini unaosimamiwa na Serikali au unaotokana na maonyesho ya kimataifa ya vito.

Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuepusha gharama za minada kwa wafanyabiashara na kuongeza ushiriki wao katika mnada unaosimamiwa na Serikali.

Kifungu cha 100C kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho, ili kupunguza vikwazo kwa usafirishaji wa nje ya nchi vito vya thamani vilivyouzwa na Serikali au katika maonyesho ya kimataifa ya madini.

Kifungu cha 100D kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuruhusu biashara ya makinikia ndani ya nchi.

Amesema lengo la marekebisho haya ni kuvutia uwekezaji katika viwanda vya madini ghafi nchini.

Amesema kifungu cha 106 kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho, ili kuwataka wafanyabiashara wa madini walio na leseni na mawakala au madalali walio na leseni kuapa kiapo cha uadilifu.

Amesema lengo la marekebisho haya ni kudumisha viwango vya maadili, uaminifu, na uadilifu katika shughuli za madini, pamoja na kuzingatia sheria.