Shirika la Posta lashauriwa kukumbatia Tehama

Muktasari:

  • Ili Shirika la posta liweze kudumu sokoni na kusonga mbele, ni lazima wajikite kwenye utoaji wa huduma kidigitali ikiwemo matumizi makubwa ya TEHAMA hasa kipindi hichi chenye ushindani mkubwa wa huduma na nchi zingine duniani.

Arusha. Shirika la Posta Tanzania limetakiwa kuyapa kipaumbele matumizi ya Tehama ili kuendana na kasi ya ushindani ya utoaji huduma na nchi zilizoendelea.

Hayo yamebainishwa leo Julai 26, 2023 jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Hadija Rajabu wakati akifungua kikao kazi tendaji cha baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania.

Amesema ili Shirika la Posta liweze kudumu sokoni na kusonga mbele, ni lazima lijikite kwenye utoaji wa huduma kidigitali ikiwemo matumizi makubwa ya Tehama hasa kipindi hichi chenye ushindani mkubwa wa huduma na nchi nyingine duniani.

“Kwa mabadiliko yaliyoko sasa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kimazingira, usalama wenu wa kubaki sokoni ni kuyapa matumizi ya Tehama kipaumbele ili tusiachwe nyuma na nchi zingine zinazotoa huduma hizi,” amesema.

Amesema baada ya kikao hicho Serikali inatarajia Shirika la Posta kujiboresha kwenye maswala ya biashara mtandao ambayo ndio hitaji kubwa la wananchi kwa sasa.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa shirika hilo, Macrise Mbodo amesema kuwa Viongozi wote wa Shirika la posta Tanzania bara na visiwani wamekutana  kutafakari na kutathimini utendaji kazi wao kwa mwaka na kusaini mikataba ya utendaji mpya mwakani.

“Tumedhamiria kuwa miaka minne ijayo kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka 2026, kupitia mpango wetu wa kibiashara, tutaifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa kwa posta zote za bara la Afrika,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania, Ramadhani Omary amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa maazimio yao ni kukosekana kwa anwani ya makazi hasa Zanzibar.

“Tunashukuru Serikali kwa sapoti kubwa wanayotupatia katika kutekeleza majukumu yetu, lakini tunaomba itusaidie kukamilisha anwani ya makazi Zanzibar ili tukamilishe malengo yetu ya kutoa huduma popote mwananchi alipo,” amesema Omary.