Shuhuda asimulia dakika 20 za hekaheka kukamatwa 'Boni Yai'
Muktasari:
- Shuhuda amesimulia mwanzo mwisho namna Boni Yai alivyokamatwa na jeshi la polisi waliomfuata katika mgahawa wa Golden Fork Sinza wilayani Kinondoni
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, limetumia takribani dakika 20 kumkamata meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu kama 'Boni Yai' katika mgahawa wa Golden Fork uliopo maeneo ya Sinza Makaburini mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi hilo, David Misime, Jacob anashikiliwa kwa makosa ya jinai anayotuhumiwa.
Mashuhuda wa tukio la kukamatwa kwake wanadai haikuwa kazi rahisi huku purukushani za hapa na pale zikizuka kati ya kada huyo wa Chadema na Polisi jambo lililozua taharuki kwa wapita njia na wateja waliokuwapo katika mgahawa hao.
Inadaiwa kuwa mjumbe huyo wa zamani wa kamati kuu ya Chadema aliingia uvunguni mwa gari kwa lengo la kujiokoa kama ambavyo mmoja wa mashuhuda (jina limehifadhiwa) aliyezungumza na Mwananchi kuelezea mwanzo mwisho wa tukio hilo.
Shuhuda huyo ameliambia Mwananchi jana Jumatano Septemba 18, 2024 kwamba ‘Boni Yai’ amekamatwa jioni akiwa na marafiki zake watatu walioketi kwenye mgahawa mmoja uliopo Sinza jijini Dar es Salaam wakibadilishana mawazo.
“Wakati wakiendelea kupiga stori ghafla wakatokea askari zaidi ya watano waliovalia kiraia kati yao watatu walikuwa na silaha na wengine takribani 10 waliokuwa wamevalia sare za Jeshi la Polisi waliokuwa nje ya kidogo ya mgahawa.
“Walikwenda moja kwa moja kwenye meza ya ‘Boni Yai’ wakaanza kuzichukua simu za mkononi,” anasimulia shuhuda huyo.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo alikuwa karibu ya eneo hilo, anasema baada ya simu hizo kuchukuliwa askari hao walisikika wakimwambia ‘Boni Yai’ kwamba unahitajika Kituo cha Polisi Oysterbay na yupo chini ya ulinzi.
Hata hivyo, shuhuda huyo anasema Boni Yai aliwauliza wao kina nani akajibiwa ni maofisa wa polisi, akauwaliza tena wanatoka kituo gani? Akajibiwa tena kwamba wanatoka Oysterbay na walitoa vitambulisho.
Shuhuda huyo anadai mlengwa wao alikuwa Boni Yai waliomwambia kwamba anahitajika kituo cha polisi, ambapo meya huyo wa zamani wa Kinondoni aliwaambia atangulie atawafuata nyuma kwa kuwa anuani yake inatambulika na yeye anajulikana.
Shuhuda huyo akimnukuu Boni Yai amedai: “Boni alikataa na kuwaambia kuwa kama nyie maofisa wa polisi tangulieni, nipo nyuma yenu nawafuata”.
Shuhuda amedai kuwa Polisi walikataa huku wakisema huyu jamaa amekuwa mbishi tutumie nguvu.
Anasema askari hao watano wakaanza kumvamia Boni Yai, wakaanza kuvutana na diwani huyo wa zamani wa Ubungo, kadiri purukushani ilivyokuwa ikiendelea polisi waliongezeka huku wananchi wakijazana katika eneo hilo.
Katika purukushani hizo, shuhuda huyo anasema nguo za Boni Yai zilichanika ikiwemo shati na suruali, ndipo katika jitihada za kujiokoa meya huyo wa zamani aliingia chini ya uvungu wa gari aina ya V8 lililokuwa limeegeshwa katika mgahawa huo.
Baada ya taarifa za Boni Yai kusambaa katika mitandano ya kijamii, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kada huyo amekamatwa na katika kurupushani hiyo amechaniwa nguo na sasa OC- CID wa Osyterbay amewataka mawakili wake kumpelekea nguo kituoni hapo.
Hata hivyo, shuhuda huyo anasema polisi hawakukata tamaa, wakaanza kuangaika naye, ndipo mmoja wa askari akatoa mkanda na kuuingiza katika shingo ya Boni Yai ili kumtoa kwa urahisi chini ya gari hilo.
Shuhuda huyo amesema baada ya kufanikiwa kumtoa Boni Yai chini ya uvungu, ndipo mmoja wa marafiki zake waliokuwa wameketi wote akawaambia askari wamuachie kwa kuwa ameshakubali kwenda kituoni, lakini wakiendelee hivyo watamuumiza.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya purukushani hizo kudumu zaidi ya dakika 20 Boni Yai alipandishwa katika difenda mojawapo kati ya mbili zilizokuja na askari hao
Wakili wake
Wakiliwa ‘Boni Yai’ Hekima Mwasipu amedai ukamataji wa Boni Yai hakuwa wa kawaida ulizua taharuki kubwa uliosababisha mteja wake huyo kupelekwa kituo cha polisi kifua wazi kwa mujibu wa maelezo ya wahudumu wa Golden Fork.
“Purukushani ilitokana na polisi kutumia nguvu kubwa kumkamata jambo ambalo Boniface hakukubaliana nalo akasema yupo radhi kwenda kituo chochote polisi mwenyewe, kutokana na matukio ya utejaji.
“Boniface alikuwa na wasiwasi kwamba wale sio polisi, lakini mwisho siku mteja wangu aliangukia mikono mwa mkuu wa upelelezi Kinondoni,” amesema Mwasipu.
Polisi wafanya upekuzi nyumba yake
Baada ya kushikilia kwa saa kadhaa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, msafara wa magari mawili mojawapo lililombeba Boni Yai ulielekea nyumbani kwa mwanasiasa huyo Mbezi Msakuzi kufanya upekuzi uliodumu kwa saa tatu kuanzia.
Akizungumza na wanahabari Mwasipu amesema polisi wamesaini nyaraka zote muhimu zinazohitaji katika upekuzi na jeshi hilo lilikuta ‘document’ ambazo ‘Boni Yai’ alikuwa anaandika mihtasari yake ya kawaida waliondoka nazo.
“Boni anashikiliwa kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo mtandaoni na kuzua taharuki kinyume na kifungu namba 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015, alivyoanza kuchukuliwa maelezo ya onyo mteja wetu tukamshauri kwamba asitoe maelezo yoyote, kama inahitaji atayatoa mahakamani.
“Baada ya hapo tukaomba dhamana bahati mbaya Mkuu wa Upelelezi Kinondoni akasema yeye mikono yake imefungwa kwa sababu mlalamikaji ni Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma,” amesema Mwasipu.
Mwasipu anasema kwa mujibu wa sheria polisi wanatakiwa kumshikilia mtuhumiwa muda usiozidi saa 24, kwa kuwa ‘Boni Yai’ alikamatwa saa 10 alasiri, hivyo wanatarajiwa hadi leo Alhamisi jioni mteja wao atapewa haki ya dhamana.
“Asipopata dhamana tutachukua hatua za kisheria za kuhakikisha polisi wanalazimishwa kwa mujibu wa sheria kumpa dhamana Boniface,” amesema Mwasipu.