Shule iliyobadilishwa kutoka kilabu cha pombe yahitaji vyoo

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo, Evance Mwambebule akieleza kero ya Shule ya Sekondari Rejiko jijini Mbeya kwa Mkuu wa Wilaya, Beno Malisa hayupo pichani. Picha na Hawa Mathias

Mbeya. Zaidi ya wanafunzi 2,359 na walimu 25 wa Shule ya Sekondari Rejiko jijini Mbeya wanalazimika kutumia matundu 11 ya vyoo kutokana na uhaba wa matundu nane huku ilielezwa shule hiyo awali ilikuwa kilabu cha pombe za kienyeji na wananchi kulazimika kubadili matumizi.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo , Bujo Kasambala amesema leo Ijumaa Machi 31, 2023 wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa kwa niaba ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kukabidhi mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio.

Kasambala amesema kuwa awali wananchi waliridhia kubadili matumizi miundombinu  ya  kilabu cha pombe za kienyeji na kuwa Sekondari ili kuondoa adha ya wanafunzi wanamaliza elimu ya msingi katika shule za pembezoni kutotembea umbali mrefu kufuata elimu.

Amesema ujenzi wa  shule hiyo ni juhudi za wazazi kujichanga na kujenga vyumba 16  vya madarasa na kuanza kupokea wanafunzi mwaka 2007 ambapo kwa mwaka jana walipokea Sh40 milioni za  mapambano dhidi ya Uviko 19  ambazo zilitumika kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu.

“Tunamshukuru Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kwa kuliona hili kuja kuchangia mifuko ya saruji ambayo itasaidia kusukuma mradi wa ujenzi wa wigo ambao ukikamilika upunguza utoro na mwingiliano wa jamii,”amesema.

Kasambala amesema  mahitaji  ya matundu ya vyoo 19  vilivyopo ni 11 ambapo 12 vya wanafunzi wa kiume 1,191  huku  1,168 kwa ajili ya wanafunzi wa kike na mawili yanatumiwa na walimu 25 hali ambayo inawalazimu kujisaidia kwenye nyumba za jirani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, Evance Mwambebula ameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuitupia jicho shule hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi baada ya kubadili matumizi kutoka kilabu cha pombe za kienyeji kutokana na Kata ya Majengo kukosa shule ya sekondari.

“Mkuu wa Wilaya haya ninayoyasema kayapeleke kama jinsi yalivyo kwa uongozi wa Jiji hapa ilipojengwa shule hii kulikuwa kilabu cha pombe cha Wazee wetu tangu mwaka 1954, lakini baada ya kubaini kata ya majengo hatuna Shule mwaka 2007  tulibadili matumizi kwa kila kaya kuchanga 2,000 na kutumia nguvu kazi kujenga vyumba 16 vya madarasa,”amesema.

Ameongeza kuwa ni jambo la kusikitisha halmashauri ya jiji kushindwa kuunga mkono juhudi za wananchi kwani mpaka leo jiko na vyumba vilivyokuwa vikitumika kuuzia pombe na kupikia vinatumika kama madarasa na ofisi ya walimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema kutokana na changamoto zilizopo  watachangia matofali 500 na kuomba wazazi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya wigo, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

“Leo hii nimekuja kwa niaba ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kukabidhi mifuko 50 ya saruji ni wazi amekuwa mchango mkubw kuchangia katika sekta mbalimbali na kama Serikali wanaunga mkono jitihada zake,”amesema.

Kwa upande wake Ofisa elimu Taaluma Jiji na Kaimu Ofisa elimu, Titus Oscar amesema kuwa bado wanaendelea na maboresho ya shule mbalimbali za sekondari na kwamba tayari halmashauri ilitoa Sh20 milioni kwa ajili ya ujenzi wa matundu 11 ya vyoo.