Shule sita zafungwa Dar, Mbeya kupisha mvua

Muktasari:

Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha baadhi ya shule kufungwa na wazazi wa shule nyingine kuwazuia watoto wao wakiwa wanasubiri mabadiliko ya hali ya hewa.

Dar/Mbeya. Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini Tanzania, baadhi ya shule katika mikoa ya  Dar es Salaam na Mbeya zimefungwa kwa muda.

Shule ya awali na msingi ya Tusiime na Fountain Gate, zote  za Dar es Salaam zimefungwa kwa siku mbili kuanzia leo Jumatano, Aprili 24 hadi 25, 2024. Zitafunguliwa Jumatatu, Aprili 29, 2024. Ijumaa ya Aprili 26 ni sikukukuu ya Muungano.

Halmashauri ya Kyela, Mkoa wa Mbeya yenyewe imetangaza kuzifunga shule zake nne ikiwemo moja ya sekondari iitwayo Tenende. Za msingi zilizofungwa ni Matebe, Tenende na Ndola.

Hatua hiyo inatokana na mvua kubwa zinazonyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara kupitika kwa shida pamoja na baadhi ya shule kuzingirwa na maji.

Jana Jumanne, Aprili 23, 2024, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza mwendelezo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Mvua hizo ndizo zilizosababisha vifo vya wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyopo Murieti jijini Arusha baada ya gari la shule kusombwa na maji Aprili 12, 2024.

 Katika tukio hilo, msamaria mwema mmoja aliyejitolea kuwaokoa wanafunzi hao, naye alifariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 24, 2024,  Mmiliki wa Tusiime, Dk Albert Katagira, amesema wamefunga shule kwa muda kutokana na mvua zinazoendelea, kwani watoto wamekuwa wakichelewa kufika shuleni na majumbani.

“Tumeona hali imekuwa mbaya watoto wanafika nyumbani saa sita usiku kutokana na gari kukaa muda mrefu kwenye foleni kutokana na barabara kutopitika tukaona ni kuwatesa watoto,” amesema Dk Katagira.

Amesema watoto wamekuwa wakiamka mapema lakini wanafika shule saa tatu hadi saa nne asubuhi, hivyo hata utaratibu wa ufundishaji umekuwa ukibadilika.

Dk Katagira amesema kuchelewa kwa watoto kufika shule, kumesababisha kuchelewa kwa vipindi vya asubuhi badala ya kuanza saa mbili wanajikuta wameanza kwa kuchelewa.

Pia, amesema kutokana na kuharibika kwa miundombinu,  wamehofia usalama wa watoto wanapokwenda shuleni au kutofika kabisa na sababu hizo zimewasukuma wafunge shule kwa siku mbili.

“Wanaokuja na usafiri wa kawaida wanawahi lakini wanaotumia gari la shule wanachelewa. Kati ya watoto 40 ni watoto 15 wanaoweza kuwahi kwa sababu kuna maeneo gari haliwezi kufika kutokana na ukatikaji wa njia na mzazi ameshalipa huwezi kumwambia amlete shule,” amesema.

Rehema Ramadhani, mzazi ambaye watoto wake wanasoma Fountain Gate ya Tabata amethibitisha ni kweli wametumiwa ujumbe wa kusitishwa kwa masomo kutokana na mvua zinazoendelea.

“Tumetumiwa ujumbe jana kuhusu watoto kutokwenda shule hadi Jumatatu Aprili 29 kutokana na mvua na  njia hazipitiki,” amesema Rehema.

Naye Athuman Bilal mkazi wa Tabata Liwiti amesema hajaruhusu mtoto wake kwenda shule kwa kuhofia usalama wa mwanawe kupita kwenye njia zinazojaa maji.

“Sijaona haja ya kulazimisha mtoto kwenda shule kwa kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha mfululizo.Nimemwambia mtoto akae nyumbani maana nakutana na watoto njiani wakiwa wanateseka kwenye mvua,” amesema Bilal.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwaya, Venista Mpogole, amesema kata hiyo ni miongoni mwa kata 11 zilizokumbwa na mafuriko na kwamba wamesitisha masomo baada ya hali ya mafuriko kuwa mbaya na miundombinu ya shule kuzingirwa na maji.

"Tunasubiri hali itakapotengamaa kwani haya maji yanakuja kwa wingi na baada ya siku tatu yanaisha, ili kulinda usalama wa wanafunzi Serikali imeona ni vyema kusitisha masomo kwa muda," amesema.

Imeandikwa na Devotha Kihwelo na Hawa Mathias