Shule yaiangukia Serikali miundombinu ya wenye ulemavu

Muktasari:

  • Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mbula ‘B’ iliyopo Wilayani Lushoto mkoani Tanga, Reuben Menga ameiomba Serikali kuiwezesha kupata miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu ili wapate fursa ya kujifunza.

Lushoto. Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mbula ‘B’ iliyopo Wilayani Lushoto mkoani Tanga, Reuben Menga ameiomba Serikali kuiwezesha kupata miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu ili wapate fursa ya kujifunza.

Shule hiyo yenye wanafunzi 648 ni mchanganyiko pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu, ikiwa na wanafunzi wenye ulemavu wa usonji na mtindio wa ubongo wakiwa 26.

Mwalimu Menga ameyasema hayo leo Juni 4 wakati akisoma taarifa ya shule hiyo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022, Sahil Geraruma wakati wa ukaguzi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa Kwa fedha za michango ya mwenge.

Amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu rafiki kwa walemavu jambo linalopelekea walimu kuwabeba wanafunzi wanapotaka kuingia darani na kutoka.

"Hapa tuna watoto wenye uhitaji maalumu wapatao 26  ambapo wasichana 16 na wavulana 10,  changamoto kubwa wanayokutana nayo walimu ni pamoja na zana za kufundishia na kujifunza.

“Lakini pia tuna uhaba wa walimu wa elimu maalumu shuleni hapa ambapo kwa sasa shule ina walimu wawili wa elimu maalumu jambo linalopunguza ufanisi kwa walimu hao ambapo mwongozo unaelekeza mwalimu mmoja afundishe watoto watano,” amesema.

Aidha, amesema changamoto nyingine ni Jamii husika kuwa na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wenye ulemavu na kwamba bado wapo baadhi ya wazazi wanawaacha majumbani watoto hao wakati Serikali inasisitiza watoto hao kupata elimu sawa na wengine.

Shule ya msingi Mbula ina vyumba vinane vya madarasa na kwamba inahitaji kuongezewa vyumba vitatu vingine ili kuondoa adha ya mlundikano wa watoto darasani.

Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 Sahil Geraruma amesema wameridhishwa na ubora wa darasa lililojengwa kwa fedha za michango ya mwenge na kwamba kinaweza kutumika kwa wanafunzi shuleni hapo.

"Tumeridhishwa na darasa lina ubora na viwango vinavyohitajika. Naahidi kuzifikisha changamoto zenu kwa Rais Samia (Suluhu Hassan) na tuna imani zitapatiwa ufumbuzi,”

Akiuzungumzia mwenge huo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Lushoto  utakimbizwa umbali wa kilometa 369  kwamba utazindua miradi 11 yenye thamani ya Sh 3.46 bilioni.