Shule zafunguliwa, changamoto kibao

Dar/mikoani. Wakati shule zikifunguliwa jana, mrundikano wa wanafunzi umeonekana kuwa changamoto kubwa kwa shule za msingi huku baadhi ya wazazi wakishindwa kuwaandikisha watoto wao kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa.

Jijini Dar es Salaam, shule nyingi za msingi za Serikali zilionekana kufurika wanafunzi na wazazi waliowapeleka watoto wao kuwaandikisha.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mabibo iliyopo Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Hussein Dady alisema kuanzia asubuhi hadi saa 8.00 mchana jana alikuwa tayari ameshaandikisha zaidi ya watoto 20 wanaofanya idadi kufikia 110 huku wengine wakiwa wameandikishwa siku za nyuma kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza.

“Hawa 110 tutawagawanya katika madarasa mawili ya mkondo A (55) na B (55), uandikishaji unaendelea hadi Machi 31, kwa hiyo hadi jioni leo (jana) tunaweza kuwa na 120 au 130,” alisema huku akifafanua kuwa shule itawapokea wanafunzi katika mikondo hiyo miwili bila kujali idadi yao.

“Huwezi kuwakataa watoto wakiletwa, madarasa tunayo mengi ila yanahitaji ukarabati tu,” aliongeza mwalimu Dady.

Mwandishi wa Mwananchi alishuhudia msafara wa wazazi wakiwa wameongozana na watoto wao, wengine wakiwa kwenye sare za shule na wengine mavazi ya kawaida wakielekea katika shule za msingi Tabata, Mabibo na Makuburi, Dar es Salaam.

Pia baadhi ya shule za Mwanza na Tabora zilifurika kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.

Akizungumzia changamoto zilizopo, ofisa elimu ya msingi wa Jiji la Mwanza, Ephraim Majinge alisema kuna upungufu wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na madawati.

Alisema wana lengo la kuandikisha wanafunzi wa elimu ya awali 4,972 na tayari wameshaandikisha wanafunzi 869.

Pia alisema walitegemea kuandikisha wanafunzi 9,733 kwa ajili ya kuingia darasa la kwanza na tayari wameshaandikisha wanafunzi 2,074.

Alisema halmashauri hiyo ina jumla ya vyumba vya madarasa 747 kati ya 2,295 vinavyohitajika hivyo kuifanya kuwa na upungufu wa vyumba 1,548.

Kuhusu matundu ya vyoo, alidai wanahitaji 4,170 wakati yaliyopo ni 1,028 ambao ni upungufu wa matundu 3,142.

“Tunahitaji madawati 34,596, lakini yaliyopo ni 20,460, kwa hiyo upungufu ni 14,129,” alisema.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa mjini Moshi umegundua kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wazazi kukosa nafasi za watoto wao katika shule zilizopo karibu na makazi yao.

Miongoni mwa shule ambazo zimefurika wanafunzi hao wa darasa la kwanza ni Mawenzi na Uhuru zilizopo katika Manispaa ya Moshi.

Hata hivyo hadi kufikia jana asubuhi, jumla ya wanafunzi 1,686 sawa na asilimia 48.2, walishaandikishwa kujiunga na darasa la kwanza katika shule mbalimbali za Manispaa ya Moshi, huku katika shule za awali wakiandikishwa wanafunzi 1,214 sawa na asilimia 40.

Manispaa hiyo inakusudia kuandikisha wanafunzi 3,646 wa darasa la kwanza ambapo wavulana ni 1,884 na wasichana 1,746 huku kwa wanafunzi wa awali, manispaa hiyo ikikusudia kuandikisha wanafunzi 3,061.

Mmoja wa wazazi, Eunice Mbise alisema amezunguka shule zote zilizopo karibu kama vile Mji Mpya, Mawenzi na Uhuru lakini zote alikuta zimejaa na kwamba hana uhakika kama mtoto wake atapata nafasi ya kujiunga darasa la kwanza au la.

Hata hivyo, ofisa elimu ya msingi Manispaa ya Moshi, Nicholaus Ngonyani alisema bado wanaendelea na uandikishaji na kwamba hali halisi itapatikana kuanzia Januari 7, 2020, kwa kuwa wazazi wengi huenda kuandikisha wanafunzi siku ya kufungua shule.

Mkoani Morogoro imeelezwa kuwa upungufu wa miundombinu ya shule yakiwemo madarasa ndiyo limekuwa tatizo kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi jana, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kambarage iliyopo Manispaa ya Morogoro, Magreth Msacky alisema upungufu wa madarasa bado ni tatizo kwa shule hiyo na watoto waliojitokeza kujiandikisha ni wengi ukilinganisha na wale wanaotakiwa kuchukuliwa.

Alisema mpaka sasa amepokea wanafunzi zaidi ya 179 wakati shule kwa darasa la kwanza ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 na bado kuna wazazi wanawapeleka watoto wao shuleni hapo.

“Madarasa ni kidogo na darasa moja linaweza kuwa na wanafunzi zaidi ya 150, kama kuna uwezekano Serikali inabidi ifanye utaratibu ili kuwa na uwiano wa watoto kwa shule zote, sikatai kupokea watoto laiti kama kungekuwa na madarasa ya kutosha isingekuwa tatizo,” alisema.

Baadhi ya wazazi akiwemo Suzana Andrea walilalamikia kutakiwa kupeleka vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao ndio watoto wapokelewe.

“Nimekuwa nikifuatilia cheti cha kuzaliwa cha mtoto Rita (Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini) lakini wamenieleza nifuatilie mkoani Kigoma alikozaliwa,” alisema mzazi huyo.

Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Msacky alisema hilo ni agizo la Serikali linalolenga wazazi kuandika majina yaliyo sawa na yaliyomo kwenye vyeti vyao vya kuzaliwa.

Wakati shule zikifunguliwa, mkuu wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula ametoa agizo kwa wazazi kupeleka chakula kwa ajili ya watoto wao kutokana na umbali kati ya shule hizo na makazi ya watu.

Chaula alisema kutokana na umbali huo, ameshaagiza wazazi na walezi kuchangia chakula ili watoto wao waweze kula shuleni na kuongeza kiwango cha taaluma shuleni.

“Walimu hawapaswi kushika fedha au kuwa kwenye kamati za fedha za chakula, kuna mwongozo wa serikali unatamka hilo, ila wazazi na walezi pekee ndiyo wenye kutakiwa kusimamia,” alisema Chaula.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi alisema wanafunzi 4,496 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza.

Myenzi amesema shughuli ya uandikishaji inafanyika kwa muda wa miezi mitatu hivyo uandikishaji unaendelea kwenye shule mbalimbali.

Jijini Arusha, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Meru, Mussa Rwambano amesema shule hiyo ilitarajia kuandikisha watoto 160 wa darasa la kwanza na 100 wa chekechea lakini idadi imekuwa kubwa zaidi.

“Tunaendelea kuwapokea hadi muda huu tayari tumeandikisha watoto 148 wa darasa la kwanza naona bado wapo wengi hapa na wazazi wao.

“Kuhusu madawati hatuna shida watoto wote 160 ambao tulipanga kuwapokea watakaa kwenye madawati,” alisema.

Hata hivyo, tayari katibu tawala mkoa wa Arusha, Richard Kwitega ameagiza watoto wote kupokelewa wakati jitihada za kukamilisha madarasa na madawati zikiendelea.

Imeandikwa na Janeth Joseph, Flora Temba, Yuvenal Theophil, Lilian Lucas, Hamida Sharif, Kelvin Matandiko, Peter Elias, Jesse Mikofu, Mgogo Kaitira na Robert Kakwesi.