Sigara yasababisha kifo Babati

Wednesday September 15 2021
pombeepic
By Joseph Lyimo

Babati. Mkazi wa mtaa wa Negamsi Mjini Babati Mkoani Manyara, Gift Mihayo amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa anaishi kuwaka moto uliosababishwa na sigara aliyokuwa akiivuta.

Hata hivyo, mke na mtoto wake, walifanikiwa kutoka nje na kunusurika kifo wakati Mihayo alishindwa kufanya hivyo kutokana na mlango wa nyumba kujifunga.

Mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo Abdi Kasimu amesema kuwa marehemu Mihayo ni mpangaji kwenye nyumba hiyo na huwa ana tabia ya kunywa pombe kila siku.

Kasimu amesema siku ya tukio mke wa marehemu baada ya kuona moto huo alianza kufanya jitihada za mwananawe na alijaribu kufanya hivyo kwa mumewe alishindwa kwakuwa moto ulishaongezeka.

 “Mke wake akafanikiwa kumtoa mtoto nje na wakati anamfuata mume wake ndani, kwa bahati mbaya moto ukawa mkubwa na mlango ukajifunga na kushindwa kumuokoa,” amesema Kasimu.

Amesema pamoja na jitihada za majirani waliotoka nje usiku huo baada ya mwanamke huyo kuanza kupiga yowe na kuomba msaada hawakufanikiwa kumuokoa marehemu Mihayo.

Advertisement

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) Merrison Mwakyoma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Kamanda Mwakyoma amesema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa kwenye hospitali ya Mrara inayomilikiwa na halmashauri ya mji wa Babati kwa uchunguzi zaidi.

“Inasemekana Mihayo alikuwa amekunywa pombe na kulewa hivyo hata kama tunakunywa tuwe na tahadhari kwa kunywa kwa kiasi,” amesema Kamanda Mwakyoma.

Advertisement