Siku 267 za Malima na Chalamila Kanda ya Ziwa

Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila (kushoto); kulia ni Adam Malima wa Morogoro.

Muktasari:

Uteuzi wa wote wawili pamoja na wenzao kadhaa ulifanyika Julai 28, 2022 kwa Malima kuhamishiwa Mwanza akitokea Mkoa wa Tanga kwa wadhifa huo huo wakati Chalamila akienda Mkoa wa Kagera akitokea benchi alikopumzishwa tangu Juni 11, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alipotengua uteuzi wake wa ukuu wa Mkoa wa Mwanza.

Mwanza/Bukoba. Adam Malima na Albert Chalamila wamehitimisha siku 267 za kuhudumu katika nafasi za ukuu wa mikoa ya Mwanza na Kagera ambazo pamoja na mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu zinaunda Kanda ya Ziwa.

Malima anayehamia Mkoa wa Morogoro na Chalamila anayeenda Mkoa wa Dar es Salaam wameongoza mikoa hiyo miwili ya Kanda ya Ziwa kuanzia Agosti 3, 2022 (kwa upande wa Malima) na Agosti 6, 2022 kwa upande wa Chalamila.

Uteuzi wa wote wawili pamoja na wenzao kadhaa ulifanyika Julai 28, 2022 kwa Malima kuhamishiwa Mwanza akitokea Mkoa wa Tanga kwa wadhifa huo huo wakati Chalamila akienda Mkoa wa Kagera akitokea benchi alikopumzishwa tangu Juni 11, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alipotengua uteuzi wake wa ukuu wa Mkoa wa Mwanza.

Kumbukumbu chanya za Malima Mwanza

Siku 267 za Malima mkoani Mwanza zinaacha kumbukumbu zenye hisia na maoni chanya na hasi kulingana na mitazamo ya watu wa kada tofauti wakiwemo wananchi wa kawaida, viongozi na watumishi wa umma.

Msimamo thabiti wa kulinda fedha za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU 1984) zinazohifadhiwa kwenye akaunti maalum (Escrow) inayosimamiwa na Serikali ni miongoni mwa kumbukumbu inayosalia kwa wana ushirika huo.

Licha ya shinikizo la kuhitaji zaidi ya Sh2 bilioni zilizohifadhiwa kwenye akaonti hiyo, Malima alisimama kidete kusimamia maamuzi ya Serikali kwa kudhibiti fedha hizo huku akimwagiza Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Mwanza, Lucas Kiondere kusimamia uandaaji wa taarifa za fedha za NCU kabla ya kuruhusu fedha hizo zianze kutumika.

Mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa NCU, Mkuu huyo wa Mkoa hakupepesa macho kwa kusisitiza kuwa fedha hizo hazitatoka hadi taarifa za fedha za ushirika zitakaporidhisha huku akiwahakikishia wana ushirika kuwa fedha hizo ni mali yao na hazitachukuliwa na yeyote.

Tukio la baadhi ya viongozi na watendaji wa Jiji la Mwanza kudaiwa kuuza viwanja viwili vilivyoko katikati ya jiji la Mwanza kwa Sh1 bilioni kinyume cha maelekezo yake na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ni kumbukumbu nyingine itakayosalia Mwanza wakati wa uongozi wa Malima.

Ingawa sababu za kutenguliwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Yahaya Selemani hazikutajwa, lakini wengi wanaamini sakata la viwanja hivyo ambavyo vilisababisha watumishi wanne wa jiji kusimamishwa kazi ilihusika.

Kumbukumbu hasi

Kwa viongozi wa wilaya na halmashauri za Mwanza, kuondoka kwa Malima ni faraja kwao katika eneo la kutunza na kuheshimu muda kutokana na kiongozi huyo kuwa na kawaida ya kuchelewa kwenye matukio kuanzia vikao vya ndani na mikutano ya nje.

Mmoja wa mtumishi mkoani Mwanza (jina limehifadhiwa) anasema kuna wakati watumishi wa umma walilazimika kukaa kwenye vikao hadi Saa 8 usiku jambo ambalo halikuwafurahisha watumishi.

‘’Tulishazoea kufanya vikao hadi usiku wa manane kwa sababu Mkuu alikuwa anafika Saa 10:00 jioni kwa shughuli ambayo ratiba yake ilipaswa kuanza Saa 3:00 asubuhi. Kuna siku tulikaa ukumbini hadi Saa 8:00 usiku baada ya RC kufika Saa 12:00 jioni wakati kikao kilitakiwa kianze Saa 4:00 asubuhi,’’ anasema mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Buchosa kwa sharti la kuhifadhiwa jina.

Mrundikano wa uchafu mitaani na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao baadhi huombaomba kwenye mzunguko wa barabara ya Nyerere na Kenyatta, hatua zisizozidi 100 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na hatua chini ya 50 kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ni eneo ambalo baadhi ya wananchi wanaamini RC Malima hakufanya vema akiwa Mwanza.

‘’Baadhi ya watoto hawa wanakuwa na wazazi au walezi wao ambao muda wote huketi kivulini huku wakiwaelekeza watoto kuomba msaada kwa wapiti njia,’’ anasema Halima Mohamed, mkazi wa Mtaa wa Fire jijini Mwanza

Akifafanua, Halima anasema; ‘’Baadhi ya wazazi na walezi hawa ni watu wenye nguvu wasio na tatizo lolote kiafya wala kimaumbile. Nadhani hili ni eneo ambalo Serikali inastahili kuingilia kati kwa kudhibiti tabia hii inayoathiri ustawi wa watoto ambao ndio Taifa la kesho. Kwa maoni yangu, Mkuu wa Mkoa anayeondoka hakufanikiwa katika eneo hili,’’

Juhudi za kumfikia Malima kupata maoni yake hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewa huku ujumbe mfupi aliotumiwa kupitia mtandao wa WhatsAPP pia haukujibiwa licha ya kupokelewa.

Yanayomsubiri Makalla

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga kuanza kurejea katika maeneo ya katikati ya jiji walikoondolewa ni moja ya changamoto atakayokumbana nayo Amos Makalla anayehamia Mwanza akitokea Mkoa wa Dar es Salaam.

Sababu kuu inayotajwa kuwaondoa wafanyabiashara hao kutoka maeneo walikohamishiwa na kurejea katikati ya jiji ni miundombinu duni katika maeneo waliyotengewa.

“Ukifika eneo la Mchafukuoga (moja ya soko ya wamachinga jijini Mwanza), meza nyingi ziko tupu baada ya wafanyaiashara kuondoka na kurejea maeneo walikoondolewa. Changamoto kubwa ni miundombinu duni; hakuna mifereji ya kupitishia maji. Mvua ikinyesha maji hutwama kwenye vibanda vyetu na kutusababishia hasara,” anasema Wilson Mtakulu, mmoja wa wamachinga eneo la Mchafukuoga

Marietha John, mkazi wa Mtaa wa Igogo jijini Mwanza anataja uchafu kurundikana mitaani licha ya wananchi kutozwa fedha za taka Sh2, 000 kila kaya kwa mwezi kuwa mzigo mzito unaomsubiri Makalla.

“Mifereji ya maji barabarani imejaa takataka kwa sababu magari ya taka hayapiti mitaani kukusanya taka. Hii ni kero tunayomtarajia Mkuu mpya wa mkoa ashughulikie,’’ anasema Marietha

Kagera wanavyomkumbuka Chalamila

Albert Chalamila, anayehamia Mkoa wa Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Amos Makalla anayekwenda Mwanza atasalia kwenye kumbukumbu ya wakazi wa Mkoa wa Kagera anakotoka, hasa kwenye maeneo makuu matatu ikiwemo jitihada za kudhibiti biashara ya kuvusha kimagendo kahawa kwenda nchi jirani.

Uimarishaji wa vyama vya ushirika na bei nzuri kwa wakulima wa kahawa ni eneo linguine ambalo wakazi wa Mkoa wa Kagera wanataka kuwa mafanikio ya Chalamila ambayo wanapenda kuona Fatuma Mwassa anayechukua nafasi yake akiendeleza.

Akizungumzia uhamisho wa Chalamila, mkazi wa Manispaa ya Bukoba, Gervase Gaiga anataja kumbukumbu nzuri wanayobaki nayo wana Kagera kuwa ni jinsi kiongozi huyo alivyoondoa vizuizi vingi vya barabarani vilivyokuwa kero kwa wananchi, hasa katika Wilaya za Karagwe, Kyerwa na Ngara.

“Tunajua kuhamishwa kwa kiongozi na mtumishi wa umma ni jambo la kawaida; lakini kuhamishwa kwa Mkuu wetu wa mkoa, Albert Chalamila ni pigo kwetu wana Kagera. Alikuwa kiongozi asiyemung’unya maneno linapofika suala la maslahi ya wananchi. Aliwakemea watendaji na kuchukua hatua papo hapo kama alivyofanya kwenye vizuizi,’’ anasema Gaiga

Kuhimiza wana Kagara kufanya kazi kwa bidii kuendeleza maeneo yao ni sifa nyingine anayopewa Chalamila katika uongozi wake wa siku 267 mkoani Kagara.

Abdul Mashankala, mkazi wa Manispaa ya Bukoba anamsihi Mwassa kufuata na kuendeleza mema yote ya mtangulizi wake, hasa utatuzi wa papo hapo wa kero za wananchi.

“Mkuu wetu wa mkoa alikuwa karibu sana na wananchi; hakuwa na urasimu na alimsikiliza kila mtu. Simu yake ilipokelewa wakati wote na hakika tulijivunia uwepo wake. Hatuna namna zaidi ya kumwombea huko aendako,’’ anasema Godelina Mathias, mkazi wa Mtaa wa Hamugembe, Manispaa ya Bukoba akimzungumzia Chalamila

Akizungumza na Mwananchi kuhusu maoni ya wananchi kuhusu utendaji wake, Chalamila anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kutimiza wajibu wake huku piaakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo.

‘’Nina deni la kufanya kazi uimarisha imani ya Rais Samia kwangu. Asanteni sana (wananchi) kwa sala na maombi yenu,’’ amesema Chalamila