Silaa ataka Serikali kutoyumbishwa uboreshaji wa bandari
Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Sakata la makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai limeendelea kujadiliwa bungeni ambapo Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa ameshauri Serikali ikubali ushauri na isikilize wananchi lakini wakati mwingine isikubali kuyumbishwa.
Dodoma. Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa ameishauri Serikali kutokubali kuyumbishwa na watu wanaotaka nchi isiendelee kiuchumi kwa kupinga utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uboreshaji wa bandari nchini.
Bunge liliridhia azimio makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania la 2023.
Silaa ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 22,2023 akichangia hali ya uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24.
Amesema makubaliano hayo yalipigiwa kelele na watu wengi na kwamba baada ya elimu juu ya suala hilo kutolewa wenye kuelewa wameelewa kuwa yalikuwa makubaliano tu.
Silaa amesema elimu iliyotolewa na Serikali imewawezesha Watanzania kuelewa juu ya makubaliano hayo yaliyoingiwa na kuridhiwa kwa azimio na Bunge.
Amesema wananchi wameelewa kuwa mikataba ya uwekezaji utakaofanyika bado haijaingiwa na pia wakati wa uingiaji wa mikataba hiyo Serikali imesema itazingatia maoni na ushauri uliotolewa na watu mbalimbali.
Amesema kwa uwekezaji huo katika bandari uchumi utakuwa na sekta nyingine pia zitaboreshwa kutokana na uboreshaji wa bandari hiyo.
“Tukubali kuwa kama Rais Benjamin Mkapa alivyokubali kupigiwa kelele mwaka 2004 (wakati wa ubinifsishaji) leo tunapokea hundi pale Mlimani City (gawio la Benki ya NMB) jina lake halikutajwa hata mara tatu,”amesema.
Ameiomba Serikali ikubali ushauri na isikilize wananchi lakini wakati mwingine isikubali kuyumbishwa na watu wenye nia zao za kutaka nchi isiendelee kiuchumi.
“Tuwe na uwekezaji na kushirikisha sekta binafsi katika maeneo wenzetu waliyobobea, tupate uwekezaji mzuri wa bandari. Tutakuja hapa miaka ijayo kushukuru. Sifa zitakwenda kwa watu wakati huo,” amesema.