Simba, Chui, fisi ‘waingia’ Zanzibar

Mhifadhi wa Wanyamapori Mkuu, Ashraph Shemoke akimuonyesha Simba akiwa katika eneo maalumu katika maonyesho ya Tamasha la Kizimkazi. Picha na Jesse Mikofu

Unguja. Wakati wanyamapori hususani simba na chui wakivushwa kwa mara ya kwanza kwenda kisiwani Zanzibar katika maonyesho ya tamasha la Kizimkazi, Ofisa Utalii kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Lusajo Nsweve, akisemani mpango katika kutanga utalii.

Wanyama hao ambao kwa mujibu wa Nsweve ni mara ya kwanza kupelekwa kisiwani humu tangu uhuru, wananchi wamevutiwa kuwaona huku wakiomba kuwapo eneo maalumu la kudumu la wanyama hao na kivyo kutoa fursa kwa wengi kuwaona.

Nsweve ameyasema hayo leo Agosti 25, 2023 eneo la Paje Mkoa wa Kusini Unguja ambapo linafanyika tamasha la Kizimkazi, linalotarajiwa kufunguliwa kesho na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kulifunga Agosti 31, 2023.

Tamasha hilo lilianzishwa rasmi mwaka 2016 likitambulika kwa jina la Samia day kabla ya kubadilishwa jina mwaka 2018 na kuitwa ‘Kizimkazi Day’ lengo likiwa ni kutangaza utamaduni, vivutio na rasilimali za Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja ambapo hufanyika kila mwaka mwezi Agosti.

Ofisa huyo wa Tawa amesema kuwa katika kuunga jitihada za Serikali kutangaza utalii Tawa imeamua kupeleka wanayama hao ikiwa ni kivutio kimojawapo kwa wanananchi hao sambamba na kuwapa burudani.

“Tunaendelea kutangaza utalii kwa nguvu zote lengo kubwa kuongeza idadi ya watalii na mapato kama ambavyo inajulikana kwamba sekta inayochangia pato la taifa zaidi ya silimia 17 ni utalii na inaongeza ajira rasmi na zisizo rasmi zaidi ya ajira milioni 1.5,” alisema.

Amesema hiyo ni fursa kwa wananchi kwa sababu inaweza kutoa pato binafsi na pato la taifa na kwamba ndiyo maa Tawa wamekuja kutoa elimu ya jinsi ya kuwafuga wanyamapori hao kupitia mashamba ya wanyama hao (zoo).

Wanyama waliovushwa kuja Zanzibar ni pamoja na simba, chui, fisi, pundamilia, pofu, nungunungu na ndege aina ya korongo.

“Ukiachilia mbali kuwaona kwenye picha, sijawahi kuwaona wanyama hawa kwakweli, nimevutika kuona kwa macho yangu, nimefurahi kweli,” amesema Khamis Rashidi mkazi wa Paje Zanzibar.

Kwa upande wake Khadija Fahma, pamoja na kueleza furaha yake ya kuwaona wanyama hao kwa mara ya kwanza, ameishauri Serikali kungalia uwezekano kuweka hifadhi kisiwani humo ili iwe rahisi na kutoa fursa kwa wananchi wengi kuwaona wanyama hao fahari ya Tanzania.