Simba wala mifugo, wajeruhi mtu

Serengeti. Mtu mmoja amejeruhiwa na mifugo zaidi ya 16 tofauti imeliwa na simba ndani ya mwezi huu katika vijiji vya Nyichoka na Robanda wilayani Serengeti.

Mwaka 2019 na 2020 simba walijeruhiwa watu wawili na kuua mifugo zaidi ya 100 na kuilazimu Wizara ya Maliasili na Utalii kuwahamisha simba 36 kwenda Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alimtaja majeruhi kuwa ni Mgusui Chacha (32), mkazi wa Nyichoka aliyeshambuliwa na simba Januari 13 jioni katika mapambano ya kuwadhibiti wasikamate mifugo yake.

“Alifanikiwa kumdhibiti huyo simba kwa kutumia panga na kukimbia, wakati anaanza kuswaga mifugo, ghafla akavamiwa na simba mwingine aliyekuwa amebana pembeni, alipiga kelele na kuokolewa akiwa amejeruhiwa,” alisema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere, Tanu Warioba alisema majeruhi huyo anaendelea vema.

Kwa mujibu wa viongiozi wa maeneo hayo, mifugo 16 imeshaliwa na simba katika vijiji vya Bokore na Nyichoka.