Simba wavamizi sasa wasakwa kwa helikopta

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Iringa. Siku 11 tangu simba walipovamia baadhi ya vijiji vya Kata za Kiponzelo, Maboga na maeneo ya Tanangozi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy ametoa tahadhari kwa wananchi kutotembea usiku na kuwa kwenye makundi nyakati za mchana.

Mbali ya kuagiza muda wa mwisho wa matembezi kuwa saa 11 jioni, pia amewataka wananchi kutowafukuza simba wanapovamia mazizi ya mifugo yao ili washibe na kutoleta madhara kwa binadamu.

Wakati Kessy akieleza njia za kufanya ili kujihadhari na simba, Hifadhi ya Taifa Ruaha jana ilianza kutumia helikopta kuwasaka wanyama hao ambao mpaka sasa wameua ng’ombe 11, nguruwe mmoja na kuku.

Tangu simba wavamie kwenye vijiji mbalimbali, hofu imetanda miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi washindwe kutembea kwa uhuru, hasa usiku.

Akizungumza na Mwananchi, Kessy alisema simba huanza kutembea usiku kutafuta chakula, hivyo ni vizuri muda huo wananchi wasitembee ikiwa ni mojawapo ya mbinu ya kujihami.

Alisema wakati wa mchana wananchi wanapokwenda shambani wawe kwenye makundi ili kuepuka madhara kwa wanyama hao.

“Safisheni maeneo kuzunguka mazizi, kama kuna mahindi yavunwe, majani yaondolewe. Chukueni magogo mkoke moto. Simba akija hataleta madhara,” alisema na kuongeza:

“Wametembea zaidi ya kilomita 11 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Serikali tunahangaika kuhakikisha simba wanarudi kwenye maeneo yao na ikiwezekana tuwaondoe kabisa na ikibidi kuwaua tutafanya hivyo.”

Kessy alisema tangu Juni 13, mwaka huu simba waliingia kwenye makazi ya wananchi kupitia Kijiji cha Magunga.

“Walipofuatiliwa waliondoka Magunga walikoua ng’ombe wanne, wakaingia Kiponzelo ambako pia waliua wanne. Wakaingia vijiji vya Makongati, Sadani, Tanangozi na Malagosi,” alisema Kessy.

Aliwataka wananchi waelewe kwamba simba pia wapo kwenye taharuki.

“Simba wanataharuki kwa sababu maeneo waliko hawajazoea, wanapohangaika hivyo wana njaa pia. Magunga waliua ng’ombe wakakurupushwa hivyo hawakushiba.

“Kama simba ameshaingia kwenye eneo amefanya uharibifu asikurupushwe, aachwe ale mpaka ashibe ndiyo aondoke. Kinachosumbua, simba kwa sababu wana njaa hawatulii sehemu moja na matokeo yake inakuwa kazi ngumu kwa watu wa hifadhi,” alisema.

Alisema kwa sababu mahindi bado hayajavunwa na kuna mapori, imekuwa kazi ngumu kuwapata.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuacha kula mizoga kwa madai kuwa kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha afya zao kwa sababu simba ni mnyama wa porini.

“Acheni hiyo mizoga, simba ana tabia ya kurudi kula mizoga. Wataalamu wana uwezo wa kuwaita kwa kutumia milio ya fisi au simba wenzao kuwafanya warudi,” alisema Kessy.

Diwani wa Kata ya Maboga, Venserus Muyinga alisema wananchi wameshapewa elimu ya namna ya kufanya ili kupambana na simba.

"Wananchi wapo tayari kufuata masharti na mbinu walizopewa kupambana na simba, tunashukuru tumeona jitihada za kuwatafuta wanyama hawa," alisema.

Mmoja wa wananchi ambaye mifugo yake ilivamiwa, Fanuel Malekela alisema tangu wakati huo amekuwa akipambana kuhakikisha zizi lake linalindwa.