Simu janja inavyotumika mbadala wa funguo ya gari

Simu janja inavyotumika mbadala wa funguo ya gari

Muktasari:

  • Umewahi kuwaza kuwasha gari yako kwa kutumia simu ya mkononi hata kama umesahau funguo? Kama hujawahi basi hilo linawezekana.

Dar es Salaam. Umewahi kuwaza kuwasha gari yako kwa kutumia simu ya mkononi hata kama umesahau funguo? Kama hujawahi basi hilo linawezekana.

Hiyo ni baada ya Kampuni ya Pips Technologies kuja na programu ya Smartkey inayowawezesha watu kuwasha magari yao kwa kutumia simu za mkononi, kufunga na kufungua milango, kuifuatilia (track) gari ilipo.

Ikiwa na watumiaji zaidi ya 200 mpaka sasa, wazo hilo lilipatikana siku ambayo gari ilijifunga (lock) milango huku funguo ikiwa ndani ya gari, pia ndani ya hilo gari kuna funguo ya nyumba.

“Funguo ya nyumba ingekuwapo tungeweza kupata spare key iliyo ndani, katika kuwaza namna ya kutatua hilo ndipo nikasema kama ningekuwa na programu kwenye simu inayowezesha kufungua mlango wa gari nisingehangaika,” anasema Mkurugenzi mkuu a Pips Technologies, Victor Rweyemamu (25).

Akizungumza na Mwananchi, Rweyemamu anasema wazo hilo lilianza mwaka 2020 mwishoni nchini, lakini hadi inaanza kufanya kazi ilikuwa mwanzoni mwa mwaka huu.

Akiwa ni mhitimu wa shahada ya Science and Geoinformatics anasema kukosa msaada kutoka kwa watu wa karibu na kushindwa kubeba wazo alilokuwa nalo kama vile yeye anavyoliona ilikuwa ni moja ya changamoto, lakini halikumfanya kurudi nyuma bali kusimamia kile anachoamini.

Changamoto ya mtaji katika kufanikisha utekelezaji wake ni kitu kingine ambacho kikimpa tabu na hata ilipofika wakati wa kubadili wazo kuwa kitu kukosekana kwa watengezaji wa bidhaa hizo nchini ilikuwa kikwazo kingine.

“Tanzania haina manufactures wa hizi hardware, hivyo ili kufanikisha hili ilinibidi kusafiri karibu mara tatu kwenda nje kutafuta watengenezaji,” anasema.

Baadaye walipata kampuni iliyopo nje ya nchi inayofanya kazi ikiwa na muelekeo sawa na wazo walilonalo, kupitia mazungumzo walifanikiwa kuingia ubia wa kutengenezewa vifaa hivyo.

Teknolojia hiyo inaweza kutumika katika gari yoyote ile isipokuwa zinazotoka Ulaya na kutumia umeme mwingi ikiwemo BMW, Range Rover, Benz.


Inavyofanya kazi

Smart key, haimpi mtu tu uhuru katika kutumia gari yake, bali mambo mengi yamezingatiwa ikiwemo kuboresha usalama wa gari la mtumiaji.

Pia programu hiyo uwekaji wake haiathiri mfumo wa funguo, hivyo kumfanya mtu kuwa na chaguo katika njia anayotaka kutumia.

Mtu akiwa na programu hiyo, inampa uwezo wa kuwasha na kuzima gari, kufunga na kufungua milango na kufuatilia mwenendo wa gari kujua mara ya mwisho ilikuwa wapi, pia ikiwa inatembea mtu anajua kwa sasa iko wapi.

“Pia programu ina uwezo wa kufanya gari kuwa na uwezo wa kujifunga mlango na kujifungua, inafanya gari kuwa na uwezo wa kujiwasha na kujizima ikiwa mtu atakuwa katika umbali fulani.

“Kutokana na namna tulivyofanya mtu akiisogelea gari inaweza kujifungua milango na kuwaka, ukitoka ukiacha inawaka ukiwa katika umbali fulani inajizima na kufunga milango,” anasema Rweyemamu.

Pia mtu akiwa umbali wa mita 100 anaweza kuwasha gari yake huku akielezea kuwa ni kama ni sehemu yenye jua kali inampa mtu fursa ya kufanya gari yake ipoe.

Katika upande wa ulinzi wa gari, Rweyemamu anaeleza kuwa mtu anapokuwa na programu hiyo huwa na uhakika wa ulinzi, kwani hata mtu akiiba funguo au kuchongesha anaweza kushindwa kuiwasha.

“Hapa kuna vitu viwili, engine activation na automatic security, katika upande wa injini mtu anaweza kuzima na kuwasha kupitia simu, ukiwasha ni kama umeiambia gari usiwake kwa kutumia funguo, hata kama mtu ataiba simu pia gari haitowaka hadi mtu awe anajua kutumia programu hiyo,” anasema.

Njia ya pili ni ya kujifunga milango ikiwa utasahau kufunga, pia mtu ana uwezo wa kuweka muda maalumu ikiwa gari itaibiwa na muda huo unapokwisha gari ikizima hakuna namna ambayo anaweza kuiwasha tena.

Katika kuazimana magari alisema kuna namna ambayo inamuwezesha mtu kutumia gari ya mwingine bila kupewa funguo, bali kupewa access ya programu.