Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi kata ya Ng’ambi ilivyofanikiwa mapambano mabadiliko ya tabianchi

Baadhi ya wanufaika wa mradi wa ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi wakishiriki mavuno ya mtama.

Mpwapwa. Kata ya Ng’hambi wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma kama ilivyo kwenye maeneo mengine, athari za mabadiliko ya tabianchi zilidhihirika na kuathiri shughuli za wananchi.

Kata hiyo iliyokuwa na watu 11,926 katika kaya 3,014 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, ilikumbwa na changamoto ya hali ya hewa, zikiwemo ukame wa mara kwa mara na ukosefu wa maji ya kutosha.

Changamoto hizo ziliathiri sekta za kilimo na ufugaji, huku wakulima wakishindwa kupata mavuno ya kutosha na ufugaji ukikosa tija kutokana na uhaba wa malisho na maji. Mazingira hayo yalizorotesha hali ya kiuchumi na kijamii ya wakazi wa eneo hilo.

“Nilikuwa mkulima wa mahindi, mazao yaliharibika kila mara kutokana na jua kali,” anasema William Samwel, mkulima kutoka kijiji hicho. William anasema athari za ukame zilisababisha kukosekana maji ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani na mifugo. “Hili liliathiri ustawi wa jamii nzima. Watoto walikosa lishe bora, hali iliyozorotesha afya yao na kuathiri maendeleo yao kwa jumla.” Katika mahojiano na Mwananchi Desemba, 2024 alisema ukosefu wa maarifa na nyenzo za kilimo mbadala ulikuwa kikwazo kwa wakazi wa Ngh’ambi kujikwamua kiuchumi na kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya zao.

Mazingira hayo magumu yalihitaji hatua za haraka ili kuleta mabadiliko na kuboresha maisha ya wakazi wilayani humo.

Novemba, 2024 viongozi kadhaa duniani walikutana kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP 29) uliofanyika Baku, Azerbaijan, miongoni mwa ajenda ikiwa kuongeza hamasa na kuwezesha kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko na kuhakikisha mchakato unaojumuisha wote katika kufanya uamuzi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo barani Afrika kuandaa Mpango wa Nchi wa Kuendeleza Programu ya Kuongeza Kasi ya Urekebishaji Afrika (AAAP) – njia ya uwekezaji inayoonyesha vipaumbele vya uwekezaji wa urekebishaji, mahitaji ya kifedha na mikakati ya kuhamasisha fedha kwa ajili ya kutekeleza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Mabadiliko ya kilimo

Wakazi wa Kata ya Ng’hambi, chini ya Asasi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA Tanzania) kupitia mradi wa kijamii wa ustahamilivu wa mabadiliko ya tabianchi wamebadilisha mtazamo wa kilimo.

Sasa wanajishughulisha na kilimo himilivu wakitumia njia bora za uhifadhi.

Katika kutekeleza mradi huo, jamii ya Ng’hambi ilipokea elimu ya mabadiliko ya tabianchi kuelewa athari na jinsi wanavyoweza kujihusisha na kilimo endelevu.

Mratibu wa mradi huo, Ally Mwamzola anasema: “Tulianza kwa kutoa elimu ili jamii ielewe vizuri athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kujikinga dhidi yake.”

Mafunzo yaliyotolewa anasema yalisaidia wakulima kuelewa umuhimu wa kilimo cha mtama, zao lenye uwezo wa kuvumilia ukame badala ya mahindi.

“Kabla ya mradi huu mkulima alikuwa na uhakika wa kuvuna gunia tatu hadi nne kwa ekari moja, lakini baada ya mradi sasa wakulima wana uhakika wa kuvuna magunia tisa hadi 10 kwa ekari moja,” anasema Mwamzola, akionyesha jinsi wakulima walivyobadili kilimo kuendana na hali ya hewa.

Mwamzola anasema ili kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazao, jamii ilijifunza namna ya kuongeza thamani.

“…pia walipokea nyenzo sahihi za kilimo, kama mbegu, mbolea na magunia ya kuhifadhia chakula, hii imeongeza hali ya usalama wa chakula,” anasema.


Lishe kwa watoto

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef), tangu mwaka 2010, Tanzania imepiga hatua katika kupunguza viwango vya udumavu, ambavyo vimepungua kutoka asilimia 42 hadi asilimia 30.

Katika kupambana na utapiamlo kwa watoto uliosababishwa na lishe duni, familia sasa zimeanzisha bustani za mboga nyumbani, jambo lililoboresha lishe na afya za watoto.

Diwani wa kata hiyo, Richard Matonya anasema: “Hivi sasa karibu kila kaya ina bustani ya mboga, tunatumia maji kidogo kuzitunza. Uanzishaji wa bustani za mboga umesaidia kuboresha afya za familia na kupunguza utegemezi wa mazao ya kilimo kikubwa pekee kama chanzo kikuu cha chakula.”

Kupitia mradi wa ustahamilivu, asilimia 71.4 ya wakulima sasa wana uelewa wa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Kwa kuzingatia uendelevu wa mradi, elimu ilitolewa pia shuleni.

Shamba darasa lilianzishwa Shule ya Sekondari Ng’hambi, ambalo licha ya kuwawezesha kupata elimu ya kilimo cha kisasa, pia wanapata chakula wawapo shuleni.

“Tunatumia shamba la shule kutoa lishe kwa wanafunzi na kuwafundisha mbinu za kisasa za kilimo ambazo na wao wamekuwa wakiwapatia wazazi wao,” anasema Juma Yahaya, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ng’hambi.

Anasema: “Kupitia mkakati huo wa shamba darasa, wanafunzi sasa wana uhakika wa chakula wakiwa shuleni na hata kutumia ujuzi wanaoupata juu ya mbinu bora na za kisasa katika kilimo, pia kuurithisha kwa wazazi na jamii inayowazunguuka.”

Kupitia mradi huo unaoendeshwa na UNA Tanzania na washirika wao LM International na SMC, Mpwapwa sasa imeanza kupata matumaini ya kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuhuisha hali ya uendelevu wa sekta za maendeleo ya jamii.


Mavuno ya maji, mabwawa

Mwaka 2023 ulirekodi joto la juu zaidi katika historia ya Tanzania, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wastani ukiwa nyuzi joto 24.5 sentigredi, nyuzi joto 0.6 sentigredi juu ya zile za kawaida.

Mpwapwa, yenye hali ya nusu jangwa, inakumbwa na ukame, huku juhudi za mradi zikihusisha kuvuna maji ya mvua kwa kilimo na matumizi ya nyumbani.

Felista Isaya, mnufaika wa mafunzo ya uvunaji maji ya mvua anasema: “Nilijifunza kuchimba shimo la kuvunia maji ya mvua na sasa natumia kwa kilimo na hata kuuza maji.”

Kupitia mradi huo kumejengwa mabwawa mawili katika vijiji vya Kazania na Kiegea, kila moja likihifadhi lita milioni tisa.

Ujenzi umefanyika kwa kushirikiana na UNA Tanzania, LM International, na wakazi wa Ng’hambi.