Simulizi Kesi ya Zombe: ‘Afande Bageni ndiye aliyeamuru wafanyabiashara wa Mahenge wauawe’-(5)

‘Afande Bageni ndiye aliyeamuru wafanyabiashara wa Mahenge wauawe’-(5)

Muktasari:

  • Jana katika sehemu ya nne ya simulizi ya Kesi ya Zombe na askari wenzake 12 tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi walivyopelekwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kuuawa kwa kupigwa risasi kisogoni.
  • Pia, tuliona jinsi ndugu za wafanyabiashara hao walivyozunguka katika vituo vikubwa vya polisi kuwatafuta wapendwa wao bila mafanikio. Endelea…



Dar es Salaam. Jana katika sehemu ya nne ya simulizi ya Kesi ya Zombe na askari wenzake 12 tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi walivyopelekwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kuuawa kwa kupigwa risasi kisogoni.

Pia, tuliona jinsi ndugu za wafanyabiashara hao walivyozunguka katika vituo vikubwa vya polisi kuwatafuta wapendwa wao bila mafanikio. Endelea…

Zombe afika Urafiki Polisi na kutoa amri

Ilikuwa muda wa saa mbili usiku, siku waliyouawa wafanyabiashara wa Mahenge na dereva teksi. SSP Ndaki alikuwa amesimama nje ya Kituo cha Polisi Urafiki akiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni (OCD) SSP Mantage wakiangalia vielelezo vya magari aliyokabidhiwa kituoni hapo.

Haukupita muda liliingia gari alilokuwa akilitumia ASP Makelle na kuegeshwa kituoni hapo. Alipomaliza kuegesha gari hilo anakwenda ofisini kwake.

Takribani dakika 30 baada ya ASP Makelle kufika kituoni hapo, SP Bageni na timu yake nao walifika kituoni hapo. Alishuka kwenye gari na kuwaacha kina Koplo Bakari kwenye gari.

SP Bageni alimwendea SSP Mantange na kumwomba ashuhudie kilelezo kilichopatikana kutoka eneo la tukio la uhalifu. SP Bageni alimwagiza ASP Makelle aulete mkoba aliokuwa nao.

Simulizi Kesi ya Zombe:Wafanyabiashara wa Mahenge, dereva teksi wauawa kinyama Msitu wa Pande

Koplo Rajabu hana amani

Wakati SP Bageni akishughulika na vielelezo, Koplo Rajabu alipata fursa ya kumdadisi Koplo Saad kuhusu mauaji yale.

Koplo Rajabu: “Wale uliowaua kule msituni ni kina nani?

Koplo Saad: “Ni wale watu walioletwa na askari wa Chuo Kikuu.”

Koplo Rajabu: “Kwa nini umewauwa?

Koplo Saad: “Afande Bageni ndiye ameamuru wauawe.”

Baada ya ASP Makelle kuleta mkoba ule wenye vielelezo, wote waliingia ofisini kwa SSP Ndaki, wakafungua mkoba huo na kuhesabu pesa zilizokuwamo. Zilifika Sh2.7 milioni.

SP Bageni alimhoji ASP Makelle ‘kwa nini kiasi cha pesa kimepungua wakati taarifa zinaonesha walikamatwa wakiwa na Sh5 milioni?

Zombe atinga Kituo cha Polisi Urafiki

Wakiwa bado wanajiuliza, ghafla Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (ACP) Abdallah Zombe, ambaye wakati huo alikuwa pia ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam aliingia ofisini kwa SSP Ndaki.

Alipoambiwa kuwa kiasi cha pesa kimepungua, ACP Zombe aling’aka na kumwamuru SSP Mantange kuwa kiasi kilichopungua kipatikane. Aliondoka kwa hasira na kurudi ofisini kwake.

SP Bageni alichukua mkoba huo pamoja na pesa hizo zilizosalia na kuelekea kwenye gari lake. Kisha alimwamuru dereva waondoke hadi ofisini kwake.

Baada ya kufika Kituo cha Polisi Oysterbay, SP Bageni aliwaamuru askari wake waendelee na majukumu mengine.

Taarifa za kuuawa akina Jongo zaanza kuenea

Ni siku moja baada ya mauaji ya akina Jongo, Januari 15, 2006. Ndugu, jamaa na marafiki zao bado wako katika wasiwasi mkubwa kwa kutojua walipo wapendwa wao. Walianzisha juhudi mpya za kuwatafuta kila mahali, lakini hawakufanikiwa.

Wakati huo askari polisi waliohusika katika tukio hilo walikuwa katika pilikapilika na mikakati ya ‘kuweka mambo sawa.’

Asubuhi hiyo mjomba wao akina Jongo, Emmanuel Ekonga alilirudisha gari la Jongo gereji ili ‘likapigwe’ tena rangi. Huko alikutana na Vasco ambaye alimfahamisha kuwa akina Jongo hawakurudi hotelini walipopanga. Wote wawili waliamua kuelekea huko hotelini (Bondeni Hotel) kujua kinachoendelea.

Yapata saa tatu asubuhi. Mchami yuko nyumbani kwake. Anatafakari ni wapi waliko akina Jongo baada ya kuwakosa katika vituo vyote vya polisi walikokwenda jana yake usiku.

Mara alipokea simu kutoka kwa mchimbaji madini mwenzao aitwaye Ndongo akimtaka afike Bondeni Hotel.

Mchami alifika na kumkuta Ndongo akiwa na mmiliki wa Bondeni Hotel, Hashim Masongolo. Mchami aliwaeleza jinsi alivyozunguka katika vituo vya polisi kuwatafuta akina Jongo bila mafanikio.

Mara Masongolo akawaaga kuwa anatoka kidogo kwenda mahali ambapo anaweza kupata taarifa zao.

Takribani saa moja baada ya Masongolo kuondoka, Mchami alipokea simu kutoka Mahenge kwa Ngonyani. Ngonyani alimwambia asogee pembeni kidogo anataka kumwambia jambo zito.

Baada ya Mchami kusogea kando, Ngonyani alimwambia kuwa akina Jongo wameuawa.

“Umepata wapi taarifa hizo?” Mchami alimwuliza Ngonyani.

“Nimepewa na Hashim (Masongolo- mmiliki wa Bondeni Hotel). Sitaweza kupatikana tena sasa hivi, hivyo nendeni Muhimbili.” Ngonyani alimjibu Mchami.

Mchami alirudi kwa wenzake na kuwaeleza taarifa hiyo. Wakati huo tayari Ekonga na Vasco walikuwa wamekwishafika hapo Bondeni Hotel.

Waliondoka wote-Mchami, Ekonga, Vasco na Kibanga, ambaye pia aliwahi kuwa dereva wa Jongo, pamoja na Ndongo na kuelekea Muhimbili mochwari.

Kituo cha Polisi Oysterbay

Asubuhi ya siku hiyo, baada ya kumaliza doria, Koplo Rajabu, Koplo Rashid (Lema) na Koplo Saad walirudisha na kukabidhi kituoni silaha walizokuwa wamepewa jana yake kwa ajili ya doria.

Silaha hizo zilipokewa na mtunza ghala la silaha, CPL Exavery Kajela. Kama ulivyo utaratibu, CPL Kajela alizikagua kuona kama zimetumika au la, kisha aliweka kumbukumbu.

Koplo Kajela alibaini kuwa silaha aliyokuwa amempatia Koplo Rajabu, bastola aina ya Chinese, haikuwa imetumika kwani ilirejeshwa na risasi zake zote 8; silaha ya Koplo Rashid, aina ya Sub Machine Gun (SMG) nayo hakuwa imetumika kwani ilirudishwa ikiwa na risasi zake zote 30.

Baada ya kumaliza kukabidhi silaha hizo, Koplo Rajabu na Koplo Rashid waliondoka. Koplo Saad alibaki kituoni hapo akifungua jalada la kufyatua silaha.

Zombe awapongeza askari walihusika

Katika kituo Kikuu cha Polisi, ACP Zombe, kupitia simu yake ya upepo, alitoa maelekezo kwa wakuu wa vituo vya askari hao, pamoja na Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs), akiwataka wawapeleke askari hao Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central Police) ili kuwashika mkono na kuwapongeza kwa kile alichokiita kazi nzuri.

Nini kiliendelea baada ya ACP Zombe kutoa amri ya askari walihusika na mauaji hayo wafike ofisini kwa kwa ajili ya kupongezwa?. Fuatilia simulizi hii kesho ndani ya gazeti la Mwananchi.