Simulizi Kesi ya Zombe:Wafanyabiashara wa Mahenge, dereva teksi wauawa kinyama Msitu wa Pande

Simulizi Kesi ya Zombe:Wafanyabiashara wa Mahenge, dereva teksi wauawa kinyama Msitu wa Pande

Muktasari:

  • Jana katika mfululizo wa simulizi za kesi ya Zombe tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa Mahenge mkoani Mororogo walivyokamatwa na kutiwa pingu.
  • Tuliona pia safari ya kuwapeleka katika Msitu wa Pande ilivyoanza huku washukiwa hao wakiwa katika hofu kuu ya kutojua hatma yao. Endelea…


  


Jana katika mfululizo wa simulizi za kesi ya Zombe tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa Mahenge mkoani Mororogo walivyokamatwa na kutiwa pingu.

Tuliona pia safari ya kuwapeleka katika Msitu wa Pande ilivyoanza huku washukiwa hao wakiwa katika hofu kuu ya kutojua hatma yao. Endelea…

Kituo cha Polisi Urafiki

Mambo mengi yaliendelea jioni na usiku wa Januari 14, 2006 baada ya wafanyabiashara wa Mahenge na dereva teksi kukamatwa na msafara wa gari lililowabeba na lingine la polisi kuanza kuelekea katika Msitu wa Pande.

Jioni ya siku hiyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) Urafiki, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Juma Ndaki alikuwa ameripoti ofisini kama kawaida. Simu yake ya upepo ilikuwa hewani.

Yeye ni miongoni mwa maofisa wa usalama waliopokea taarifa za tukio la uporaji wa fedha za mauzo katika gari la Bidco majira ya saa 12 jioni.

Wakati vijana wake (akina ASP Makelle)wanaondoka kwenda kufuatilia tukio hilo, yeye alibaki ofisini akiendelea na shughuli nyingine huku akisubiri taarifa zaidi kuhusu tukio hilo kutoka kwa vijana wake.

Baada ya muda alipokea tena taarifa kutoka kwa ASP Makelle kuhusu tukio hilo kupitia simu yake ya upepo; kuwa askari wa Chuo Kikuu wamewakamata watu wanne wakiwa na bastola na pesa ambazo walihisi ndizo zilizoporwa kwenye gari la Bidco. Hakusikia kwa uhakika kiasi cha pesa alichokitaja ASP Makelle kama ni Sh3 milioni au Sh5 milioni.

Ndugu wawatafuta akina Jongo vituo vya polisi

Baadaye, SSP Ndaki akiwa bado ofisini, watu wawili (mume na mke) walifika ofisini kwake. Hawa ni Mchami na mkewe Jane Joseph. Mchami na akina Jongo walikuwa wanafanya shughuli za uchimbaji madini pamoja. Huo ulikuwa usiku ule ule waliokamatwa akina Jongo.

Walifika kituoni hapo baada ya kupokea taarifa kutoka Mahenge kwa Ngonyani (rafiki yao akina Jongo) kuwa kina Jongo wamekamatwa na askari polisi nyumbani kwake walipokuwa wamempelekea mkewe pesa za matumizi.

Ngonyani naye ilikuwa awe katika safari moja na kina Jongo wakati wanaondoka Dar es Salaam kuelekea Arusha, lakini kwa bahati nzuri hakusafiri nao. Alipata dharura, hivyo akawapa akina Jongo baadhi ya madini yake wakamuuzie.

Kituoni hapo Mchami na mkewe walikutana na SSP Ndaki na kumuuliza kama ndugu zao waliokamatwa na polisi wamefikishwa kituoni hapo.

SSP Ndaki anawajibu kuwa hajaona mtu yeyote aliyefikishwa hapo kama mtuhumiwa. Badala yake aliwaelekeza waende katika Kituo cha Polisi Mabatini, Kijitonyama kutafuta taarifa zaidi.

yMchami na mkewe waliondoka hadi kituo cha Mabatini, lakini hawakuwapata ndugu zao. Waliamua kwenda hadi Kituo cha Polisi Oysterbay ambapo waliwakosa pia. Hawakukata tamaa. Walifunga safari hadi Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police Station) ambapo walimkuta askari mmoja wa kike aitwaye Mwanne, walimweleza shida yao.

Mwanne alipekua majina ya akina Jongo kwenye kitabu cha taarifa zilizofikishwa polisi lakini hakuyaona. Aliwaeleza kuwa si rahisi kwa watu waliokamatwa Sinza kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Majibu hayo hayakuwazuia kuendelea kuwatafuta wapendwa wao. Waliongoza njia hadi Kituo cha Polisi Msimbazi. Hawakuwapata. Walikwenda pia Kituo cha Polisi Magomeni bila mafanikio.

Baadaye Mchami na mkewe walirudi tena kwa SSP Ndaki na kumjulisha kuwa hawakuweza kuwaona ndugu zao katika vituo vyote vya polisi walivyofika.

SSP Ndaki hakuwa na jipya. Aliwaeleza hata yeye hajamwona yeyote kati ya hao akifikishwa kituoni hapo. Hawakuwa na la kufanya. Waliamua kuondoka zao huku wakiwa na wasiwasi mkubwa juu ya hatma ya ndugu zao.

Gari la akina Jongo lapelekwa polisi Urafiki

Koplo Nyangelera alifika Kituo cha Polisi Urafiki akiendesha gari la akina Jongo kama alivyoelekezwa. SSP Ndaki alimuuliza Koplo Nyangelera na mwenzake kuwa wanatoka wapi. Walijitambulisha kuwa wao ni askari kutoka Kituo cha Polisi Chuo Kikuu.

Aliporidhika na utambulisho wao, SSP Ndaki hakuendelea kuwahoji. Koplo Nyangelera alilikabidhi gari hilo kituoni hapo, lakini baada ya makabidhiano hayo, badala ya kuondoka, waliendelea kubakia palepale kituoni.

Akina Jongo wauawa kinyama Msitu wa Pande

Msafara wa SP Bageni wakiwa na wafanyabiashara watatu wa Mahenge na dereva teksi uliendelea hadi wakavuka maeneo ya makaz,i kisha waliingia kwenye msitu mnene. Huu ni Msitu wa Pande, uko katika eneo la Mbezi mbele ya Makabe, wilayani Kinondoni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

“Eneo lenyewe ni hili. Lakini hapa kuna Chui sana,” alisema yule askari waliyemchukua Kituo cha Polisi Mbezi, akimweleza SP Bageni.

Msafara ulisogea mbele kidogo, kisha SP Bageni aliamuru dereva wa gari lao asimame na kugeuza gari. Kisha ile Landrover Defender waliyobebwa akina Jongo inageuza pia. Ni umbali wa kati ya mita 15 na 20 hivi kutoka gari la SP Bageni hadi kwenye Landrover Defender.

SP Bageni, Koplo Rashid na Koplo Saad Alawi walishuka. Koplo Rajabu na yule askari wa Mbezi walibaki ndani ya gari. Ndani ya gari Koplo Rajabu anawasha radio call (simu ya upepo). Mara anasikia taarifa za tukio la ujambazi eneo la Kijitonyama.

Wakati akiendelea kusikiliza redio, mshindo mkubwa wa risasi ulisikika. Alishuka kutoka kwenye gari hilo na kusogea karibu na lilipoegeshwa Landrover Defender.

Alipokaribia aliona mtu akishushwa kutoka kwenye gari hilo na kulazwa chini kifudifudi. Kisha alimwona Koplo Saad akiwa ameshika bunduki. Koplo Saad hakupoteza muda. Alifyatua risasi na kumpiga mtu huyo. Alipoangalia vizuri aliona watu wengine watatu wakiwa wamelala chini na anabaini kuwa tayari walishapigwa risasi.

Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo, Ephraim Sabinus Chigumbi, Protasi Lunkomba na dereva teksi Juma Ndugu wamekwishauawa. Wote walipigwa risasi kichwani upande wa kisogoni na kutokea kwa mbele. Eneo walilopigiwa risasi lilitapakaa damu.

Koplo Rajabu aliitambua ile Landrover Defender iliyowafuata nyuma wakati wakielekea msituni kuwa ni ya kituo cha Polisi Oysterbay, baada ya kuwaona askari wenzake wa kituo hicho.

Baada ya mauaji hayo, SP Bageni anaamuru miili ya akina Jongo ipakiwe kwenye Landrover Defender lililowaleta kwenye msitu wa mauti. Alimwamuru pia Stafu Sajenti James kusimamia gari hilo na maiti. Kisha msafara wa magari hayo unaanza kutoka msituni.

Mauaji hayo katika Msitu wa Pande yalimchanganya na kumnyima raha askari Kituo cha Mbezi Luis. Hakutaka tena kurudishwa kituoni kwake walikomtoa. Badala yake aliomba ashushwe. Walimshusha na kisha wao kuendelea na msafara.

INAENDELEA KESHO