Simulizi Kesi ya Zombe: Wafanyabiashara watatu wa Mahenge watiwa pingu, wapelekwa Msitu wa Pande

Wafanyabiashara watatu wa Mahenge watiwa pingu, wapelekwa Msitu wa Pande

Muktasari:

  • Jana tulisome jinsi wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro walivyokamatwa na polisi eneo la Sinza, Dar es Salaam, Januari 14 mwaka 2006, muda mfupi baada ya kumkabidhi shemeji yao fedha za matumizi. Tuliona pia msafara wa magari ya polisi na washukiwa hao ulivyoondoka kuelekea eneo la Super Star ambapo, majambazi waliofanya uporaji katika gari la kampuni ya Bidco walidaiwa kukumbilia. Endelea…

Barabara ya Sam Nujoma, eneo la Konoike.

Wakati upekuzi wa wafanyabiashara wa Mahenge ukiendelea huko Sinza, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na timu yake wanafika eneo hili la Konoike, barabara ya Sam Nujoma na kukuta gari la kampuni ya Bidco na wafanyakazi wake wakiwa eneo la tukio.

SP Bageni aliwahoji nao walijitambulisha kuwa ni wafanyakazi wa kampuni ya Bidco. Walidai watu waliokuwa wakitumia gari dogo waliwapora Sh5 milioni baada ya kuwatisha kwa bastola.

Baada ya maelezo hayo SP Bageni alisogea pembeni, akaongea kwa kutumia simu yake ya mkononi na mtu ambaye wenzake hawakumfahamu.

Mara tu baada ya SP Bageni kumaliza kuongea na simu, lile gari la Polisi Chuo Kikuu lilifika likiwa na askari pamoja na wafanyabiashara watatu na dereva teksi wao. Walikuwa wamekalishwa nyuma ya gari lile aina ya Toyota Stout huku wakiwa wamefungwa pingu. Gari hilo la polisi Chuo Kikuu linafuatiwa na gari la akina Jongo likiendeshwa na Koplo Nyangelera. Kisha linafuata gari la ASP Makelle na askari wenzake wawili kutoka Kituo cha Polisi Urafiki.

ASP Makelle na Stafu Sajenti James wanatoa maelezo kwa SP Bageni kuwa watu wamewakamata watu wanne eneo la Sinza wakiwa na bastola na pesa taslimu Sh5 milioni. Dereva wa gari la Bidco anadai kuwa anahisi kuwa mmoja kati ya watu hao (akina Jongo) ni miongoni mwa waliowapora. Anaonesha kutokuwa na uhakika na maelezo yake. Wakati huo wafanyakazi wenzake walikaa kimya.

Akina Jongo walikuwa kwenye mshangao na waliingiwa na wasiwasi mkubwa kuwa walikuwa hawaelewi kinachoendelea. Hawajui chochote kuhusu tukio hilo la uporaji wa Bidco na hawana maelezo ya kuwashawishi askari wale wawaamini.

Baada ya maelezo hayo SP Bageni anasogea pembeni kidogo kisha anaongea na simu na mtu wa upande mwingine, ambaye hakuwepo hapo.

Muda mfupi baadaye lilifika gari moja aina ya Landrover Defender TZR 9559. Hili pia ni mali ya Polisi Oysterbay. Ndani kuna askari wanne. Hawa ni pamoja na Koplo Benedict, ambaye ndiye dereva wa gari hilo; D/C John Maganya, D/C Abubakar na CPL Jackson.

SP Bageni aliamuru akina Jongo washushwe kutoka kwenye gari la Polisi Chuo Kikuu na wapandishwe kwenye Defender kutoka Oysterbay. Pia, anaamuru wale askari wa Chuo Kikuu waingie kwenye hilo.

Mkuu huyo wa Upelelezi Kinondoni pia alimwamuru dereva wa gari la Chuo Kikuu na Koplo Nyangelera aliyeendesha gari la akina Jongo kuyapeleka magari hayo katika kituo cha Polisi Urafiki.

Gari la akina Makelle liliondoka eneo hilo na kwenda uelekeo wa Ubungo likifuatiwa na Defender lililoelekea pia Ubungo.

Baada ya magari hayo kuondoka, SP Bageni alisogea kando tena, akaongea na simu na baada ya maongezi alirudi walipoegesha gari lao na kuwaamuru askari. Askari walilisukuma hadi likawaka. Aliwaamuru wapande gari na kumwelekeza dereva ageuze na wakaondoka kuelekea Ubungo.

Walifika Ubungo mataa, wakaaingia barabara ya Morogoro na kuelekea Kimara. Mbele kabisa ya safari yao, SP Bageni na timu yake waliingia kituo cha mafuta. Waliongeza mafuta katika gari lao na kuendelea na safari.

Kituo chao cha kwanza palikuwa Kituo cha Polisi Mbezi Luis. Pale SP Bageni alishuka na kuingia kituoni hapo. Aliongea na askari mmoja mwenye sare na kumwamuru aingie kwenye gari lao, kisha waligeuza kama wanarudi Ubungo hadi kituo cha zamani cha daladala, Mbezi.

Hapo SP Bageni aliamwamuru dereva asimamishe gari. Alishuka na kwenda mbele ya gari na kufanya tena mawasiliano kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Wakati SP Bageni akiendelea kuongea na simu, Koplo Rajabu alipata mwanya wa kumdadisi yule askari waliyemchukua Mbezi Luis kuhusu safari hiyo.

“Afande, tunakwenda wapi?” anauliza Koplo Rajabu.

“Tunakwenda hapo mbele ya Makabe,” anajibu askari wa Mbezi.

“Kuna mtu wa kumkamata? anauliza tena Koplo Rajabu.

“Hata mimi sijui,” anajibu askari wa Mbezi.

Baada ya kumaliza mazungumzo na simu, SP Bageni anaendelea kusimama mbele ya gari hilo kwa takriban dakika 10. Mara upande wa pili wa barabara ya Morogoro usawa wa gari lao linasimama gari lingine aina ya defender.

Kisha SP Bageni anarudi kwenye gari na anapoingia anamuuliza huyu askari wa Mbezi mwelekeo na yule askari anaonesha uelekeo kisha SP Bageni aliamuru waendelee na safari.

Waliacha barabara ya lami wakaingia barabara ya vumbi upande wa kushoto. Wakati huo lile Landrover Defender lilikuwa likiwafuata kwa nyuma.

Akina Jongo hawapatikani

Dereva wa akina Jongo, Ekonga, Vasco na fundi aliyetengeneza gari lao pale gereji ya Yamungumengi hawakujua lolote kuhusu kilichowapate wateja wao.

Walikwenda hadi Kisarawe kulijaribu gari hilo baada ya kulitengeneza. Bila kujua yaliyowapata, baadaye Vasco alijaribu bila mafanikio kumpigia simu Jongo kumjulisha kuwa gari lilikuwa limekamilika ili waje kulichukua. Jongo hakupatikana kwenye simu.

Waliendelea kulijaribu gari mpaka Chanika. Wakiwa huko Ngonyani alimpigia simu Vasco kumjulisha kuwa akina Jongo wamekamatwa na Polisi.

Walirudi mpaka pale gereji muda wa saa moja usiku. Walitawanyika kila mtu na kwake. Ekonga aliamua kwenda na gari lile nyumbani kwake ili kesho yake asubuhi alirudishe kwa ajili ya ‘kulipiga’ tena rangi.

Je nini kiliendelea huko? Baada ya kupewa taarifa za akina Jongo kukamatwa na polisi Ngonyani alifanya nini?

Fuatilia kesho kufahamu zaidi.