Safari ya mauti wafanyabiashara wa Mahenge (2)

Mkuu wa zamani wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaa, Abdalla Zombe akiwa katika mahakama kuu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni aliyekuwa Mkuu wa upelelezi Kinondoni, Christopher Bageni.

Muktasari:

  • Katika toleo la jana tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani.


Katika toleo la jana tuliona jinsi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani

Morogoro walivyoanza safari yao kwenda kuuza madini jijini Arusha kisha kurudi Dar es Salaam wakiwa na Sh19.5 milioni. Tuliona pilikapilika zilizowawezesha kuuza madini ya Sh15 milioni jijini Dar es Salaam na kuumaliza mchana wa Januari 14 mwaka 2006 bila matatizo yoyote kisha wakaelekea kwa shemeji yao kumpa fedha za matumizi. Endelea kusoma simulizi hii kujua yaliyojiri...

Jioni ya Januari 14 mwaka 2006, askari polisi wanane walitoka Kituo cha Polisi Chuo Kikuu kwenda kufanya doria.

Wakiongozwa na Stafu Sajenti James Masota, walikuwa ndani ya gari la wazi aina ya Toyota Stout lenye namba za usajili SU 9363. Baadhi walikuwa wamevaa sare na wengine kiraia.

Kwenye doria hiyo walikuwapo koplo wa upelelezi Festus Gwabisabi, koplo Nyangelera Moris, koplo Emmanuel Mabula, koplo Felix Cedrick, konstebo Noel Leonard na konstebo Michael Shonza.

Kutoka kituoni hapo walielekea Changanyikeni kisha Makongo walikowashusha koplo Mabula na konstebo Shonza waliopangiwa kufanya doria eneo hilo, halafu gari likaendeshwa kuelekea Survey.


Taarifa za uhalifu

Katika kitengo cha kuratibu taarifa za uhalifu (999) kilichopo Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, sajenti Revocatus, ambaye alikuwa msimamizi wa kitengo akisaidiana na koplo John aliyekuwa akiratibu simu za upepo zinazoingia na kutoka walikuwa zamu.

Pamoja nao alikuwapo koplo Maseku ambaye alikuwa anapokea ujumbe wa simu za kawaida na simu zinazopigwa, lakini saa 12:15 jioni, koplo Maseku alipokea taarifa za uporaji pesa.

Taarifa hizi zilitolewa na mtu aliyejitambulisha kama Mashaka Mashili, dereva wa gari kubwa la kampuni ya Bidco lililotumika kukusanya fedha za mauzo ya bidhaa za kampuni hiyo.

Mashili alimweleza koplo Maseku kuwa wamevamiwa na watu wakiwa Barabara ya Sam Nujoma eneo la Konoike na watu waliokuwa katika gari ndogo aina ya Mark II. Watu hao alisema walikuwa na bastola na wameporwa zaidi ya Sh5 milioni.

Baada ya kupokea taarifa hizo, koplo Maseku aliwajulisha viongozi wenye dhamana ya upelelezi katika maeneo husika yaani mkuu wa upelelezi Kituo cha Polisi Oysterbay, Urafiki na mkoa (RCO).

Kwa mfumo wa mawasiliano ndani ya jeshi hili ambao hutumia simu ya upepo, taarifa hizi ziliwafikia askari walioko doria pia.

Stafu sajenti James akiwa njiani na kikosi chake, kabla ya kufika Survey, naye alizipokea taarifa za uhalifu huo, hivyo akawaeleza wenzake kuelekea eneo la tukio.


Kituo cha Polisi Oysterbay

Akiwa ofisini, mkuu wa upelelezi Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), mrakibu wa polisi (SP) Christopher Bageni, naye alipokea taarifa za ujambazi huo. Aliondoka na askari wanne kuelekea Konoike, katika Barabara ya Sam Nujoma.

Aliongozana na makoplo wa upelelezi Rajabu Bakari, Saad Alawi na Frank Mbutu pamoja na konstebo Rashid Lema.

Bageni alimwamuru koplo Frank, dereva wa Pajero Mitsubishi walilolitumia aendeshe kuelekea Sam Nujoma kwenye tukio.


Kituo cha Polisi Urafiki

Wakati Bageni akiondoka na askari wake, mkuu wa upelelezi Kituo cha Polisi Urafiki, mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle alikuwa akiendesha gari kuingia Barabara ya Morogoro.

Punde akawaona askari wenzake, koplom Ebeneth Saro na konstebo Jane Andrew wakivuka barabara kuelekea Kituo cha Polisi Urafiki wakitokea Kituo cha Polisi Magomeni.

Makelle aliwamuru wawili hao kuingia ndani ya gari lake na kuondoka nao. Wakiwa njiani Makelle aliwaeleza kuhusu tukio la unyang’anyi lililofanyika Barabara ya Sam Nujoma. Kwa pamoja, walielekea eneo la tukio.


Barabara ya Sam Nujoma

Gari la polisi waliotoka Chuo Kikuu lilifika Konoike na kukuta lori aina ya Benz limesimama katikati ya barabara. Nje ya gari hilo la kampuni ya Bidco kulikuwa na watu wanne wamesimama.

Stafu sajenti James na koplo Festus walishuka na kuwasogelea na James akaanza kuwahoji.

Mmoja wao alijitambulisha kuwa wao ni wafanyakazi wa Bidco na kwamba walikuwa wameporwa Sh5 milioni na majambazi waliotumia gari aina ya Toyota Mark II jeupe. Mmoja wao, alisema alikuwa na bastola, na walielekea njia ya Super Star.

Baada ya maelezo hayo James aliongoza msafara kuelekea Super Star.


Sinza Palestina

Wakati sakata ya ujambazi wa Sam Nujoma likiendelea, Jongo na wenzake walifika nyumban kwa mke wa rafiki yao Ngonyani aitwaye Benadetha Lyimo. Walimkuta amekaa baraza la nyumba ya jirani akisukwa na jirani yake.

Benadetha aliwakaribisha ndani lakini walikataa wakidai wana haraka. Jongo alimvuta Benadetha pembeni na baada ya kuteta kidogo alimpa Sh30,000.

Waliagana na Jongo akaingia kwenye gari lao ili waondoke. Wakati dereva anageuza gari, mara gari la polisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilifika na kuwazuia.

Askari walishuka kwenye gari lao na kuwaamuru akina Jongo washuke wakiwa wamenyoosha mikono juu. Jongo na wenzake walitii bila kutoa neno. Askari waliwapekua maungoni.

Lunkombe alijaribu kuhoji kwa nini waliwakamata lakini akaishia kupigwa kwa kitako cha bunduki na mmoja wa askari. Hakuwa na namna, akanyamaza.

Koplo Festus alimpekua Jongo na kumkuta na bastola mfukoni mwa suruali yake.

Aliwatahadharisha wenzake wawe makini na kuwataka wananchi wasisogee kwani waliowakamata walikuwa majambazi.

Licha ya kujitetea kuwa aliimiliki bastola ile kihalali, askari hawa hawakusikia neno. Watuhumiwa wengine walikutwa na simu ambazo askari walizichukua pia.

Wakati upekuzi ukiendelea, koplo Festus alifungua buti ya gari la akina jongo na kukuta mkoba mdogo (briefcase). Aliwauliza ndani kulikuwa na nini. Jongo alikuwa mwepesi kujibu. Alimweleza kulikuwa na pesa zao. Kopla Festus alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha na kujibiwa zilikuwa Sh5 milioni.

Koplo Festus alilifungua lile begi na kukuta mfuko mwingine ndani yake ukiwa na pesa zikiwa zimefungwa mabunda mabunda. Alishauri waelekee kituoni kwa mahojiano zaidi na ili pesa zikaguliwe kwani zaweza kuwa ndizo zilizoporwa katika gari la Bidco.

James alichukua begi hilo, Jongo alimsihi awarudishie lakini hakusikilizwa.

Haukupita muda, lilifika gari jingine, Toyota Corolla lenye namba T 262 AAP. Askari mmoja wa Chuo Kikuu alilisimamisha, waliokuwamo ndani walishuka. Walikuwa ASP Makelle, koplo Saro na Jane wa kituo cha Urafiki.

Makelle alijitambulisha na askari mmoja akampa maelezo kuwa wanawashuku waliowakamata kwa kuwa walikuwa na bastola.

ASP Makelle alishauri wapelekwe kituoni kwa mahojiano. Askari wale walitoa pingu na kuwafunga wawiliwawili, kisha waliwapakia kwenye gari lao na kuondoka nao.

Baada ya kutoa maelekezo, Makelle alirudi kwenye gari lake na kutoa taarifa ya watuhumiwa waliowakamata wakiwa na bastola na pesa taslimu Sh5 milioni.

Stafu sajenti James alimwamuru koplo Nyangelera kuliendesha gari la watuhumiwa na msafara ukaelekea Super Star.

Itaendelea kesho…