Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi maisha ya vijana Daraja la Kijazi Ubungo

Simulizi maisha ya vijana Daraja la Kijazi Ubungo

Muktasari:

  • Wakati Daraja la Kijazi lililopo Ubungo likielezwa kuwa tangu kukamilika kwake limesaidia kupunguza foleni barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma, baadhi ya vijana wamegeuza daraja hilo makazi.

Dar es Salaam. Wakati Daraja la Kijazi lililopo Ubungo likielezwa kuwa tangu kukamilika kwake limesaidia kupunguza foleni barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma, baadhi ya vijana wamegeuza daraja hilo makazi.

Kuanzia saa nne usiku si ajabu kuwaona vijana zaidi ya 50 wakiwa wamelala chini ya daraja hilo na asubuhi huamka mapema kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Mwananchi ilitembelea eneo hilo kwa siku tatu mfululizo na kushuhudia vijana wenye umri kati ya miaka 11 hadi 26 wakiwa wamejilaza na baadhi kueleza mwanzo, mwisho wa maisha yao darajani hapo.

Musa Onyango (24), mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza anasema anaishi eneo hilo mwaka wa tano sasa.

Anasema kabla ya kuhamia chini ya daraja hilo alikuwa akilala ndani ya stendi ya mabasi yaendayo mikoani (Ubungo) kabla haijahamishiwa Mbezi.

Onyango anasema aliyemshawishi kutoroka na kuja jijini Dar es Salaam ni marafiki zake wakiamini kuna maisha mazuri.

Hata hivyo, Onyango anasema baada ya kufika Dar es Salaam alikuta maisha ni tofauti na aliyokuwa anategemea, kwa kuwa ameishia kuombaomba kwenye magari na kulala chini ya daraja hilo.

“Nimekuja tangu mwaka 2016, lakini maisha niliyokutana nayo ni tofauti na nilivyokuwa nafikiria na wenzangu walivyokuwa wakieleza,” anasema Onyango.

Shughuli kubwa wanayofanya vijana hao ni kuosha vioo vya magari, kutafuta vyuma chakavu kwa ajili ya kuuza na kuomba omba angalau wapate fedha ya kula.

Onyango anasema katika maisha yao hutumia Mto Ng’ombe ulioko jirani kwa ajili ya kufua na kuoga.

“Huwa tunatumia mto ulioko jirani kwa ajili ya kufua na kuoga,” alisema Onyango.

Pia, anasema endapo atapata nauli yuko tayari kuachana na shughuli ya kuombaomba na kurudi nyumbani kwao kwani maisha wanayoishi hapo ni ya shida.

Mbali na Onyango, kijana mwingine anayeishi kwenye daraja hilo ni Pius Benedikto, mzaliwa wa Mwanza.

Anasema alishawishiwa na wenzake kuja Dar es Salaam kisha wakamtelekeza.

Benedikto anasema baada ya yakufika Dar es Salaam walijumuika na wenzao waliokuwa wakiishi eneo hilo la Ubungo mataa lakini baadaye mwenzake alimuacha na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

“Natamani nirudi nyumbani hapa nateseka tu, kama unavyoona nguo zangu ni hizi nilizoshika natembea nazo, kulala nalala hapa chini ya daraja lakini wakati mwingine polisi hutufukuza,” anasema Benedikto.

Anasimulia kuwa wanapohitaji kufua na kuoga hutumia mto ulioko jirani, ingawa maji yake sio safi na salama kwa kuwa wakati mwingine hutiririsha maji yaliyochanganyika na kinyesi.

“Nilishawishiwa na mwenzangu, baada ya kuiba hela kwao alinipitia tukaondoka kuja Dar es Salaam, tulipofika akaniacha na wenzangu yeye akaenda kutafuta kazi,” anasema.

Benedikto anasema kwa sasa hana mawasiliano ya nyumbani kwao wala rafiki zake, endapo itatokea bahati ya kurudishwa kwao yuko tayari kurudi kutokana na shida anazopata.

“Nimekuja huku Dar es Salaam kwa sababu wazazi waliachana na baada ya mama kunilazimisha kunipeleka nikaishi kwa baba na mama wa kambo, ndipo nilipokimbilia huku kutafuta maisha,” anasema kijana mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Pius Ramadhani.

Kijana huyo anasema haikuwa rahisi kukimbia, lakini kwa kuwa alikuwa anapigwa mara kwa mara ilimlazimu kufanya hivyo na hakuna aliyemwambia au kumshawishi ni yeye mwenyewe baada ya kuwasikia rafiki zake wakisema upatikanaji wa fedha ni rahisi.

“Kahama mkoani Shinyanga ni nyumbani kwetu, nina miezi sita tangu nimekuja Dar es Salaam,” alisimulia Ramadhan.

“Niliingia stendi ya Kahama nikakaa kidogo, baadaye nikapata gari ya kuzamia na kuja hadi Dar es Salaam na kufikia stendi ya mabasi Ubungo, shughuli zangu kubwa zilikuwa kusafisha vioo vya magari na kuokota makopo na kwenda kuuza.”

Anasema baada ya stendi hiyo kuhamishiwa Mbezi, maisha yalianza kuwa magumu kwa kuwa kazi ya kuosha vioo vya magari haipatikani.

Ramadhan anasema anafikiria kurudi nyumbani kwao endapo atapata mtu wa kumsaidia nauli.

“Nafikiria kurudi nyumbani kama atajitokeza mtu wa kunisaidia nauli nitafanya hivyo, sioni kama naweza kuendelea kuishi hapa kwa kuwa upatikanaji wa fedha umekuwa mgumu, tofauti na ilivyokuwa wakati nakuja,” anasema Ramadhan.

“Hadi sasa nina Sh 15,000 na nahitaji Sh30,000 nauli ikamilike ya kwenda nyumbani, bado nikifika Kahama hadi kijijini ninapotokea nauli ya daladala ni Sh2,000 nifike kwa mama yangu mzazi.”

Dickson France (21), mzaliwa wa Uyole mkoani Mbeya anasimulia kuwa amekulia mkoani Mwanza na baadaye alihamia Tabora.

Anasema kutokana na changamoto nyingi aliamua kuja Dar es Salaam. France anasema baada ya kufika, alipitia changamoto nyingi katika utafutaji wa riziki.

“Tulitakiwa kuwa darasani ili siku zijazo tujisaidie, lakini haya maisha tunayopitia ni funzo kubwa kwetu, sijajua kwa wenzangu wanachukuliaje. Wengine wameshazoea kupata fedha kidogo wanaridhika lakini mimi kwangu napata shida,’’ anasema France.

“Siwezi kuridhika na hali kama hii kwa sababu sijazaliwa kuja kuishi maisha haya, nina wazazi wangu wote wawili, lakini hatuna mawasiliano kabisa na hawajui mimi naishi wapi,” anasema France.

France anaeleza kuwa maisha ni magumu, hakuna mtu wa kuwasaidia hata wakiugua, mfano yeye mwenyewe ana miaka 14 atamsaidia nani ilhali ametoka nyumbani na kuwakimbia wazazi.


Changamoto

Hata hivyo pamoja na kuishi maisha hayo, wamekuwa wakipitia changamoto nyingi, ikiwemo kukosa milo mitatu kwa siku, kuibiwa na kupigwa na watu pale wanapohisiwa na majirani wameiba.

Pia wanaeleza kuwa wakati mwingine wamekuwa wakivamiwa na polisi nyakati za usiku na kupigwa, kukosa matibabu pindi wanapougua pamoja na watu wasio wajua hupita usiku na magari yao kuwapakiza na kuwachukua kwa ajili ya kwenda kuwalawiti kwa ahadi ya kuwasaidia.

Simulizi maisha ya vijana Daraja la Kijazi Ubungo

Kauli ya jeshi la polisi

Kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema suala la vijana hao kuishi chini ya daraja hilo ni tatizo la kijamii na kukosekana kwa malezi.

Alisema watoto wadogo wamekuwa wakitoroka kwenye familia zao na kujiunga na makundi ya uhalifu, hivyo jeshi hilo kwa kushirikiana na ustawi wa jamii wamekuwa wakiwaondoa.

“Hawa vijana wamekuwa wakikimbia majumbani kwao na baadhi yao hujihusisha na vitendo vya kihalifu, jeshi la polisi kwa kushirikiana na ustawi wa jamii tumekuwa tukiwaondoa, lakini baada ya muda hurejea tena,” alisema Mambosasa.