Simulizi Mtanzania aliyenusurika kutekwa na Hamas

Ezekiel Kitiku.

Muktasari:

  • Kitiku na wenzake wawili Joshua Mollel na Clemence Mtenga walikwenda nchini Israel Septemba mwaka huu, kwa lengo la kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.

Dar es Salaam. Mtanzania anayejulikana kwa jina la Ezekiel Kitiku ambaye yuko nchini Israel kwa mafunzo ya kilimo, amesema kubadilika kwa zamu katika shamba alikokuwa akifanya kazi, ndiko kumemuokoa kuwa mateka, baada ya wanamgambo wa Hamas kuvamia nchi hiyo.

Akizungumza na BBC nchini Israel, Kitiku amesema ilikuwa ni Oktoba 7, 2023; ambapo wanamgambo hao walipoivamia Israel na kufanya shambulio hilo la kushtukiza, ambapo inadaiwa licha ya mauaji kutokea, idadi kubwa ya raia, wageni na wanajeshi walitekwa na wapiganaji hao.

“Kama nisingekuwa niko zamu shambani, basi huenda na mimi ningekuwa mmoja wa waliotekwa katika Ukanda wa Gaza, ambao uko chini ya udhibiti wa Hamas," Kitiku amesimulia.

Kwa mujibu wa Mtanzania huyo, yeye na wenzake wawili Joshua Mollel na Clemence Mtenga walifika nchini Israel mwezi Septemba mwaka huu, kwa lengo la kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.

Tangu kuwasili kwao, Kitiku na Mtenga walikuwa wakiishi Kibbutz Nir Oz na kufanya kazi katika shamba la maziwa muda wa mchana, huku Mollel akiishi na kufanya kazi huko Kibbutz Nahal Oz.

BBC imeripoti kuwa, jiografia ya miji hiyo miwili ya Kibbutz, iko karibu na Gaza ambako kumekuwa na mapambano baina ya wanamgambo wa Hamas na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).


Namna alivyonusurika

Katika simulizi yake amesema: “Wiki hiyo ratiba mpya ilitayarishwa ambapo jina langu lilitajwa kufanya kazi za usiku na Clemence alibaki zamu ya mchana," amesema.

Kitiku ameiambia BBC kuwa pia Mollel alikuwa zamu za mchana lakini katika shamba tofauti.

Siku ya tukio, Kitiku amesema alianza zamu yake saa 7 usiku na kwamba ilipofika asubuhi saa 12 na dakika kadhaa wakati jua linachomoza, alisikia mlipuko mkubwa.

“Niliposikia kelele hizo, nikakumbuka tuliambiwa kwamba tukisikia milio ya za risasi au mabomu twende kwenye makazi, hivyo ndivyo nilivyofanya. Niliogopa. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia kelele kama hii," amesema.

Alipokuwa akielekea kwenye makazi yaliyopo shambani hapo, aliona moshi mwingi na miali ya moto kutoka karibu na makazi yake Kibbutz, hivyo mara moja akawasiliana na marafiki zake wote wawili bila kujua kuwa wanamgambo wa Hamas walikuwa tayari wameivamia Israel.

"Niliamua kuwasiliana na wenzangu na waliniambia kuwa kulikuwa na roketi nyingi sana zinazokuja kutoka Gaza, saa chache baadaye, niligundua ujumbe wa WhatsApp niliowatumia, haukufika na nikadhani labda simu zao zimeisha chaji.

“Ujumbe wa mwisho ulikuwa mko salama?” amesema.

Kitiku amesema kuwa hakupata majibu yeyote kutoka kwa wenzake hao wawili na kwamba hajasikia chochote kutoka kwao tangu wakati huo.


IDF yamhamishia sehemu salama

Kwa kuwa makombora yaliendelea kurushwa siku nzima, Kitiku alilazimika kubaki katika makazi ya shambani hapo. Hata hivyo, siku iliyofuata kulionekana kuwa shwari kidogo ndipo akamuomba meneja wake (shamani) amrudishe kwenye makazi yake ya Kibbutz, ambapo alikutana na wanajeshi wa IDF.

"Kwenye lango la Kibbutz kulikuwa na askari wengi wa IDF. Walinizuia kuingia na kunitaka nirudi shambani kwani ndiko kulionekana kuwa salama zaidi, jambo ambalo nilifanya na nikakaa shambani kwa siku nyingine mbili zaidi."

Kwa maelezo yake, baadaye IDF ilimtaarifu kuwa asingeweza kurudi kwenye makazi yake ya Kibbutz na hivyo kumsindikiza hadi eneo jingine karibu kilomita 30 kaskazini mwa Gaza.

"Mifumo ya maji ilikuwa imepigwa kwa mabomu, na maji yalikuwa yakitiririka kila mahali. Niliona maiti mtaani....Iwapo nisingekuwa shambani asubuhi hiyo, ningekuwa mmoja wa waliotekwa."

Kwa sasa Kitiku anafanya kazi katika shamba tofauti.

"Mamlaka nchini Israel walituambia tuko salama na tunaweza kuendelea na mafunzo yetu hapa.”


Wizara yakiri kupotea kwa Watanzania wawili

Alhamisi, Oktoba 26, 2023; Serikali ya Tanzania ilitoa taarifa ya kupotea kwa Watanzania wawili nchini Israel ambao ni miongoni mwa vijana 260 waliokwenda nchini humo kwa ajili ya mafunzo ya kilimo cha kisasa.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilisema kuwa, Tanzania ikishirikiana na mamlaka mbalimbali nchini Israel, wanaendelea na juhudi za kuwapata vijana hao ili kuwapeleka katika mazingira salama.

Aidha, Serikali imesema familia za vijana hao zimejulishwa kuhusu jitihada hizo na inaendelea kuwasiliana nao.

Ikumbukwe kuwa Oktoba 18, 2023, Watanzania tisa waliokuwa wanaishi nchini Israel waliitikia wito wa mpango wa Serikali wa kuwarejesha nyumbani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo.


Imeandaliwa na Mwandishi wetu kwa msaada wa mashirika.