SIMULIZI YA MAJONZI: A to Z kuuawa kwa Theresia kwenye vurugu za Polisi, wananchi Geita
Muktasari:
- Inaelezwa kuwa Theresia alifikwa na mauti baada ya kupigwa risasi iliyoingia kupitia dirisha la chumbani kwake kutoka kwenye vurugu kati ya wananchi na Polisi.
Lulembela. "Mwanangu alikua amekaa ndani chumbani kwake mimi nilikuwa sebuleni, nje ya nyumba kulikua na kelele za watu ghafla mwanangu akapiga kelele ya kuita mamaaa…Kwa sauti kisha akaanguka chini, nilivyomuangalia alikuwa anavuja damu nyingi."
Hayo ni maneno ya Grace Wilson mama wa mwanafunzi, Theresia John (18) aliyefariki dunia jana Septemba 11, 2024 baada ya kuzuka vurugu kati ya Polisi na wananchi eneo la Lulembela Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.
Grace amesimulia hayo leo Alhamisi Septemba 12, 2024 alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital nyumbani kwake, ambapo maandalizi ya mazishi ya Theresia yanaendelea.
Mama huyo kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi anaendelea kusimulia kuwa “Nilimvua nguo ili kumkagua, nikakuta tundu kifuani ambalo lilitokeza hadi mgongoni, nikamuita jirani yangu, alikuja baba mmoja, tukatoka nje kukagua kimemkuta nini, tuligundua kioo cha dirisha la chumbani kwake kimepasuka.”
Mama huyo mwenye watoto sita amesema Theresia akiwa ndani chumbani kwake risasi ilipitia dirishani na kumpiga.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa yake jana Jumatano kuhusu tukio hilo, alisema chanzo cha vurugu hizo ni baada ya watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba watoto wawili na wananchi waliokuwa kwenye mnada wa Lulembelea kuwadhania ni wezi wa watoto kisha kuwashambulia.
“Walipokuwa wanawashambulia alitokea ofisa mtendaji wa kata akawabeba kwenye pikipiki na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi Lulembela baada ya watu hao kwenye gari, akawapeleka kituoni, hata hivyo wananchi takribani 800 walifika kituoni na kuwataka polisi wawakabidhi watuhumiwa hao ili wawaue," amedai Misime.
Ilivyokuwa kabla ya Theresia kufikwa na mauti
Grace akizungumza namna mauti yalivyomkuta mwanaye amesema, zilipoanza vurugu nje kwenye kituo cha Polisi ambapo ni jirani na anapoishi, marehemu Theresia aliwasihi wadogo zake na mama yake waingie chumbani na wasitoke nje.
"Mwanangu alitoka shuleni mchana aliniambia amekuja kuchukua nguo ya kuvaa siku ya sherehe ya dini, alienda kwa fundi akajaribu nguo ikambana akairudisha kwa ajili ya marekebisho.
“Alivyokuwa anarudi nyumbani akakuta vurugu nje, alikuja moja kwa moja na kuingia ndani kisha kufunga geti akaniambia tusitoke nje kuna kundi kubwa la watu na kuna vurugu kituoni, na kweli hatukutoka lakini risasi ilimfuata mwanangu ndani," amesema Grace huku akitokwa na machozi.
Amesema mwanaye huyo alikua tegemeo kwake. “Binti yangu alikuwa na ndoto ya kusoma hadi chuo kikuu.”
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Lulembela ambako binti huyo alikuwa akisoma, Richard Mgisha amesema mwanafunzi huyo alikua tegemeo na walitarajia atafaulu kuingia kidato cha tano kutokana na juhudi zake.
"Ni mwanafunzi mwenye tabia nzuri, alikuwa na juhudi darasani na tulitegemea afaulu kwenye mtihani wake wa mwisho, tuliposikia amefikwa na mauti tulishituka kwa kuwa ni mchana huohuo alitoka hapa shuleni," amesema mwalimu Mgisha.