Prime
Simulizi ya mizimu ya mganga na mauaji ya muuguzi mstaafu -5
Katika gazeti hili jana tulikuletea namna Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi alivyoanza kuchambua ushahidi wa pande mbili na tulimalizia katika kanuni ya mtu wa mwisho kuwa na marehemu ndiye atahesabika kuwa muuaji.
Leo tunakuletea mwendelezo wa hukumu hiyo na sababu za kwa nini mahakama ilimtia hatiani mganga wa jadi, Omary Mahmoud Rang’ambo kwa mauaji ya muuguzi huyo mstaafu, Patricia Ibreck mwaka 2021.
Jaji aliendelea kueleza kuwa mshitakiwa katika kesi hiyo alikuwa na wajibu wa kisheria kueleza namna alivyoachana na marehemu baada ya kumpa dawa za mitishamba, kwa kuwa ushahidi ukiwemo wa shahidi wa sita unamlenga yeye.
Kulingana na Jaji katika kutekeleza wajibu wake, upande wa mashitaka uliweza kuunganisha ushahidi wa shahidi wa sita, Wende Mrema ambaye ni mtoto wa marehemu na maelezo ya onyo ya mshitakiwa ya kukiri kufanya mauaji hayo.
Akinukuu maelezo hayo, Omary aliulizwa alikamatwa lini na alikamatiwa wapi ambapo alijibu “Mimi nilikamatwa tarehe 2 huko Kigamboni Tungi na kushushwa kituo cha Polisi Chang’ombe na kisha nilifuatwa na askari wa Moshi”
“Nililetwa hapa Moshi ambapo baada ya kufika nilihojiwa na kwenda kuonyesha nilipofukia mwili wa marehemu (Patricia Ibreck),” mwisho wa kunukuu.
Jaji alisema kwa maelezo hayo, mshitakiwa anaeleza mwenyewe kuwa baada ya kufikishwa Moshi akitokea Dar es Salaam alipokamatiwa, alihojiwa kisha kwenda kuwaonyesha makachero wa polisi mahali alipokuwa amezika mwili wa Patricia.
“Ieleweke kuwa kwa ujumla wa ushahidi wa Jamhuri, ni baada ya mshitakiwa kukiri, ndiyo ulipatikana mwanga kuwa Patricia aliuawa na kuzikwa nyuma ya nyumba yake huko Rau,”alisema Jaji Simfukwe na kuongeza:
“Ikizingatiwa kuwa mshitakiwa ndiye mtu wa mwisho kuonekana na marehemu na pia kukiri kwake, kwa mdomo na kwa maandishi, sinashaka kuwa mshitakiwa aliyepo kizimbani ndiye aliyesababisha kifo cha Patricia Paul Ibreck”
“Nikiongozwa na kesi mbalimbali nilizozinukuu, ninaridhika kuwa kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa hai, inatosha kumtia hatiani mshitakiwa katika kesi hii,”aliongeza kusema Jaji Simfukwe katika hukumu yake.
“Zaidi ni kwamba ushahidi wa mazingira uliopo katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi hii unajenga msingi pasipo kuacha mashaka kuwa ni mshitakiwa ndiye aliyemuua Patricia,”anasisitiza Jaji katika uchambuzi wake.
Je aliua akiwa na nia ovu?
Katika kujibu hoja hiyo, Jaji Simfukwe anasema kumbukumbu za mahakama zinaonyesha baada ya kumuua marehemu, mshitakiwa alimzika na zaidi akamdanganya mtoto wa marehemu kuwa mama yake amechukuliwa na mizimu.
“Mbali na hilo, mshitakiwa alimtenga marehemu katika chumba cha peke yake kwa saa nyingi na kumpiga marufuku mtoto wa marehemu kuingia chumba hicho. Hii inaonyesha alikuwa na misheni ya kukamilisha. Hii inaonyesha alikuwa na nia ovu”
Jaji alinukuu kesi ya Chacha Bhoke Nyaitati dhidi ya Jamhuri ambapo mahakama iliweka msimamo kuwa kwa kawaida mshambuliaji hawezi kutangaza nia yake ya kusababisha kifo au madhara mwilini na hilo hupimwa kwa vigezo vifuatavyo:-
Moja ni aina ya silaha iliyotumika, mbili ni nguvu iliyotumika, tatu ni maeneo ya mwili au mapigo yaliyoelekezwa kwa marehemu, nne ni aina ya majeraha, tano ni maneno anayoyatamka kabla na baada ya kufanya mauaji na sita ni matendo.
Jaji Simfukwe anasema katika kesi iliyopo mbele yake na kwa kuzingatia matendo ya mshitakiwa kabla na baada ya kifo cha marehemu, anaridhika kuwa dhamira ovu ya mshitakiwa imeweza kuthibitishwa pasipo kuacha mashaka yoyote.
Nafasi ya utetezi wa mshitakiwa
Jaji Simfukwe anasema kigezo cha mwisho cha kukitolea uamuzi ni kama ushahidi wa utetezi wa mshitakiwa uliibua mashaka yoyote dhidi ya ushahidi wa Jamhuri.
“Kuhusiana na utetezi wake kuwa mtoto wa marehemu alimtengenezea tuhuma hizo baada ya kukataa kurudiana, haileti mashaka yoyote kwenye ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka,”alieleza Jaji Simfukwe na kuongeza kuwa;-
“Ningeweza kusimama na kuamua kwa upande wa mshitakiwa kama angeeleza namna marehemu alivyofariki nje ya kile kilichoelezwa na upande wa mashitaka. Badala yake alieleza namna alivyomuua na kumzika nyuma ya nyumba yake”
“Baadaye mshitakiwa akaendelea kumdanganya mtoto wa marehemu (Wande) na kuendelea kujipatia fedha kutoka kwake akijifanya kuwa mizimu ilikuwa bado inaendelea kumtibu mama yake. Utetezi wake wa baadae ni wa kujinasua tu”
Jaji akasema mahakama imemtia hatiani kwa kosa la kumuua Patricia kwa kukusudia na kwamba kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, adhabu ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa.
USULI:
Mauaji hayo yaliyotokea tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2021 katika eneo la Rau Mrukuti nje kidogo ya mji wa Moshi. Hata hivyo, awali ilifahamika Patricia yuko India kwa matibabu, lakini baadaye ikagundulika aliuawa na kuzikwa pembeni ya nyumba yake.
Baada ya kupita zaidi ya miezi tisa, baadhi ya ndugu na uongozi wa kijiji cha Rau walipata mashaka na kuanza kumdodosa mtoto wa marehemu, Wande Mrema juu ya mahali alipo mama yake, naye aliwajibu kuwa yuko India kwa matibabu.
Majibu hayo hayakuwaridhisha hivyo wakaamua kutoa taarifa Polisi ambapo katika mahojiano, binti huyo alitoa hadithi mbili zinazotofautiana, moja kwamba yuko mama yake India na pili ni kuwa alichukuliwa na vijana wawili ambao ni waganga wa jadi.
Ni kutokana na utata wa maelezo hayo, polisi walimshikilia Wande kwa mahojiano zaidi, ambayo yalisaidia kupatikana kwa mganga aitwaye Waziri Seleman mkazi wa Korogwe na Njoro ambaye alikamatwa akiwa Korogwe Desemba 31, 2021.
Na baadaye, alikamtaja mganga mwingine, Omary Mahmoud Rang’ambo kuwa ndiye anaweza kujua mahali alipo Patricia, ambapo polisi walifanikiwa kumkamata Januari 2, 2022 jijini Dar es Salaam.
Baada ya kukamatwa, Januari 8, 2022 Rang’ambo alirejeshwa Moshi ambapo katika mahojiano alikiri kumuua Patricia na kukubali kwenda kuwaonyesha polisi mahali alipomzika.
Mwili wake ulifukuliwa Januari 9, 2022 ikiwa ni baada ya mwaka mmoja kupita na ndani ya shimo alipozikwa, kulikutwa pia jambia lililotumika katika mauaji, shuka lililotumika kufunika mwili wake.
Kabla ya kesi, Januari 11,202, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alitoa taarifa ya tukio hilo na kudai kuwa katika matibabu ya jadi ya Patricia, waganga walijipatia zaidi ya Sh60 milioni kwa vipindi tofauti.
Januari 26, 2022, Wande na waganga hao wawili, Omary Mahmoud Rang’ambo na Waziri Ally, walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Rehema Olambo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kusomewa shitaka la kumuua kwa makusudi Patricia.
Agosti 19,2022, Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) aliwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shitaka hilo dhidi ya mshitakiwa wa Pili, Wande na mshitakiwa wa tatu, Waziri na hivyo mahakama ikawaachia huru.
Kesi ilisikilizwa dhidi ya mshitakiwa namba moja, Omary ambapo upande wa mashitaka uliita mashahidi 13 na kuwasilisha vielelezo vinane ambapo mahakama ilimuona mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu hivyo kumtaka ajitetee.
Omary alijitetea mwenyewe akijaribu kujinasua na tuhuma hizo lakini katika hukumu yake aliyoitoia Novemba 5, 2025, Jaji Simfukwe alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo ambayo ndio pekee kwa kosa la kuua kwa kukusudia.