Simulizi ya mwanamke mwenye miaka 62 anayeishi na Ukimwi kwa miaka 21

Dora Mwaluko (kulia) akimwonyesha mwandishi wa habari dawa zake za ARV alizozihifadhi ofisini ili hata akisahau zingine nyumbani asiache kunywa dawa hizo kila siku.

Muktasari:

  • Safari ya Dora Mwaluko (62) ya miaka 21 ya kuishi na VVU iliyojaa milima, mabonde na matumaini.

Dodoma. Dora mwaluko (62) ni mwanamke ambaye anaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa miaka 21 sasa tangu alipopimwa na kugundulika kuwa maambukizi hayo mwaka 2002.

Dora anaeleza safari yake iliyojaa misukosuko, milima na mabonde mpaka kufika hapa kwenye mahojiano maalumu na Mwanachi Digital jijini Dodoma.

Dora anasema alianza kuumwa homa zisizoisha mwaka 2002 na ndipo alifanya uamuzi wa kwenda kupima na kujua kama ana maabukizi ya VVU.

Anasema kwa miaka hiyo suala la Ukimwi lilikuwa juu sana na kila mtu alikuwa naogopa kukutwa ameathirika kutokana na hali ya unyanyapaa iliyokuwepo kwenye jamii.

Anasema baada ya kuona ameumwa sana na kila dawa nayotumia haponi aliamua kwenda kupima kipimo cha Ukimwi kwenye Hospitali ya Makey iliyopo jijini Dodoma.

Anasema baada ya kupimwa wakati wa kupewa majibu alishangaa anapewa ushauri nasah kwa muda mrefu na wakati kabla ya kupimwa alipewa hivyo alichokuwa nasubiria ni majibu.

Anasema kutokana na hali aliyokuwa nayo aliona kama wanampigia  kelele na ndipo alipowaambia wampe majibu ya vipimo vyake ambayo vilionyesha kuwa ameathirika na Ukimwi.

“Baada ya kupewa majibu kuwa nimeathirika niliona mwili wote umenyong’onyea, niilishiwa na nguvu na kumbuka wakati ule Ukimwi ulikuwa Ukimwi kweli kila mtu alikuwa anauogopa sasa mimi ndiyo nimekutwa nao,” anasema Dora.

Anasema aliyapokea majibu hayo na kuamua kurudi nyumbani ambako alikutana na unyanyapaa mkubwa kutoka kwa ndugu zake.

Anasema mama yake na baba yake walishatengana hivyo baba yake alioa mwanamke mwingine waliyekuwa wanaishi naye ambao baada ya kujua kuwa Dora ameathirika yeye na watoto wake waliamua kumtenga na kutoshirikiana naye kwa jambo lolote pale nyumbani.

Dora anasema hali hiyo ilimtesa mpaka alitamani afe, alitamani ugonjwa wa Ukimwi ungekuwa ni uchafu ambao angeweza kuoga na ukaisha lakini jambo hilo halikuwezekana kwani tayari virusi vilikuwa mwilini mwake.

Anasema mama yake wa kambo na watoto wake walimnyanyapaa na kumwona ni mtu wa kufa muda wowote lakini baba yake mzazi aliamua kusimama na yeye na kumtia moyo ili asikate tamaa ya maisha.

Dora ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema ndoa yake ilivunjika hata kabla ya kugundulika kuwa na VVU na ndipoa alipoamua kurudi nyumbani kwao.

Anasema baba yake aliamua kusimama naye na kuhakikisha kuwa anakuwa sawa kwa kumtafutia washauri nasaha wa kuzungumza naye mpaka mwisho wa siku aliamua kujikubali na kusonga mbele japo haikuwa rahisi.

“Niliamua kujikubali na kupokea matokeo kuwa ni kweli nimeathirika na sikutaka kujua nimejikwaa wapi na ni nani aliyeniambukiza Ukimwi, nikachagua kuishi,” anasema Dora.

Dora anasema wakati huo anagundulika kuwa na maambukizi ya VVU dawa za kufubaza Virus vya Ukimwi (ARV) hazikuwepo na waliokuwa wanapewa dawa hizo ni wale waliokuwa na CD4 chini ya 250 na wakati huo yeye alikuwa na CD4 469.

Anasema ilipofika mwaka 2005 afya yake ilitetereka na alipofanyiwa vipimo alianzishiwa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na wakati huo CD4 zake zilikuwa ni 345 lakini kutokana na changamoto za kiafya alizokuwa nazo waliamua kumwanzishia dawa.

Anasema tangu wakati huo mpaka sasa amekuwa ni mfuasi mwaminifu wa dawa na hajawahi hata siku moja kuacha kutumia dawa zake hata akisafiri kitu cha kwanza kuweka kwenye begi ni dawa zake.

“Dawa walizonianzishia mara ya kwanza zilinipa shida kidogo na baada ya kuwaeleza walinibadilishia dawa nyingine ambazo mpaka sasa naendelea kutumia na afya yangu ni njema kama unavyoniona,” anasema.

Kugundulika hana VVU

Akizungumzia kuhusu kugundulika hana tena VVU, Dora anasema mwaka 2011 alipopimwa kipimo cha Target Not Directed (TND) ambacho kinaonyesha wingi wa Virus mwilini alionekana hana Virus hivyo tena lakini hakuacha kumeza dawa.

Anasema alielezwa madhara ya kuacha kumeza ARV ghafla bila ushauri wa wataalam wa afya kuwa utarudisha maendeleo ya afya yake nyuma na anaweza kufa.

"Waliniambia siyo kwamba sina virusi mwilini bali vimefubazwa kutokana na kuwa mwaminifu kwenye kunywa dawa lakini nikiacha ghafla nitasababisha virusi hivyo kuzaliana kwa wingi na hali yangu itakuwa mbaya zaidi kwa sababu kila ugonjwa utanipiga na mwisho nitakufa," anasema Dora.

Dora anasema hana mpango wa kuacha kutumia dawa za kufubaza VVU mpaka wataalam wa afya wamwambie asitumie tena kwani ameona madhara waliyoyapata wenzake ambao walioacha ghafla matumizi ya ARV.

Anawashauri watu wanaoishi na VVU kunywa dawa kwa uaminifu na kuacha tabia ya kukatisha dozi kwani inasababisha afya zao kuzorota na mwisho wa siku wanapoteza maisha.

Anasema kuacha matumizi ya dawa kunasababisha virusi kuzaliana kwa wingi na kuushambulia mwili kunakopelekea hali kuwa mbaya lakini matumizi endelevu ya dawa yanamweka mtu kwenye nafasi nzuri ya kujikinga na magonjwa nyemelezi.

"Tunajua kila nafsi itaonja mauti, kila mtu atakufa lakini kufa kwa ugonjwa wa Ukimwi ni uzembe," anasema Dora.

Anasema kila anapokwenda ni lazima abebe dawa zake na hata ofisini kwake zipo dawa ambazo akisahau nyingine nyumbani anakutana nazo ofisini na haoni aibu kumeza mbele za watu kwa sababu ni sehemu ya maisha yake.

Dora anaiomba serikali kupima kipimo cha wingi wa virusi mwilini (HVT) ifanyike mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja kwani kufanya mara moja kunaleta utata hasa mtu akikutwa virusi vimeongezeka badala ya kupungua.

Anasema kupima mara moja kwa mwaka na mtu akikutwa virusi vimeongezeka anakuwa hajui ni wapi alikosea mpaka hali hiyo ikatokea lakini ikifanyika mara mbili kwa mwaka inakuwa ni rahisi kugundua makosa yaliyosababisha virusi kuongezeka.

Dora ambaye pia ni mwenyekiti wa watu wanaoishi na VVU Wilaya ya Dodoma Mjini anasema kwenye Konga yao ya Dodoma Mjini wana jumla ya wanachama 641 kwenye Kata zote 41 zilizopo ambao wamejiunga na chama chao ambapo kazi kubwa wanayoifanya ni kuhamasishana kuhusu matumizi endelevu ya dawa ili wawe na afya bora na waendelee kuishi.

Anasema kazi nyingine ni kuwakutanisha waviu hao na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye jamii kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Dora anatoka wito kwa wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Ukimwi kwani bado upo, hauna dawa na unaua.

Septemba 8, 2023 wakati akifungua mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoshi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha) jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka watu wanaoishi na VVU waliopimwa na kugundulika hawana tena Virusi wasiache matumizi ya dawa mpaka watakapoambiwa na wataalamu wa afya.

Waziri Mkuu alisema wapo baadhi ya watu ambao walipimwa na kuonekana hawana tena virus vya Ukimwi wakaacha dawa ghafla bila ushauri wa wataalamu wa afya na wakapata madhara makubwa.