Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya mwandishi wa Mwananchi ndani ya lori Dar - Tunduma-1

Sehemu ya mbele ya lori (dashboard) nililopanda kuelekea Tunduma kama inavyoonekana ikiwa ‘imepambambwa’ kwa kiroba cha pombe kali alichokuwa akitumia dereva na maji aliyokuwa akitumia mwandishi. Picha na Florence Majani.

Muktasari:

  • Katika simulizi hii hakutumia majina halisi ya wahusika kutokana na sababu za kiufundi. Fuatana naye kufahamu vituko vya kila aina alivyoshuhudia katika safari yake kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma akiwa ndani ya lori.

Kuna msemo kwamba maisha bila Ukimwi yanawezekana, lakini kwa Tunduma maisha bila ukahaba hayawezekani. Mwandishi wa Mwananchi amefanya utafiti kujua maisha ya madereva wa malori wanapokuwa njiani, uhusiano wao na wanawake njiani hadi wanavyopokewa Tunduma.

Katika simulizi hii hakutumia majina halisi ya wahusika kutokana na sababu za kiufundi. Fuatana naye kufahamu vituko vya kila aina alivyoshuhudia katika safari yake kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma akiwa ndani ya lori.

Ajali mbili tulizokutana nazo kabla ya kufika Mikese na tabia ya huyu dereva wa lori letu ya kufakamia ‘viroba’ vilinifanya niingiwe na wasiwasi kama nitaweza kufanikisha kazi yangu ya utafiti wa maisha ya madereva wa malori wanaosafirisha bidhaa kati ya Dar es Salaam na Tunduma.

Ajali ya kwanza tulikutana nayo Chalinze, ambako tulilikuta lori aina ya Mitsubishi Canterlikiwa limepinduka matairi juu na nyingine tuliikuta Mikese ambako lori pia lilikuwa limepinduka.

Naanza kuingiwa hofu kwa kuwa tangu tuanze safari yetu, huyu dereva amekuwa akinywa viroba bila ya kupumzika; kimoja baada ya kingine na kunifanya muda mwingi nitafakari kama itakuwa sahihi kumuuliza kuhusu unywaji wake na kazi hii ngumu anayoifanya, au nimuache hadi hapo atakaponieleza.

Lakini kwa kuwa nimeamua kutafuta maisha halisi ya hawa madereva wanapokuwa njiani, ulevi, uzinzi na makandokando mengine, nimeamua kuacha hadi hapo muda muafaka utakapofika.

Safari hii nimeianza saa 1.35 asubuhi ya Juni 19, mwaka huu siku niliyojihimu kwenda Mbezi kwa Musuguri, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Akili yangu na mwili vyote viko tayari kwa safari ya kuelekea Nakonde nchini Zambia.

Kama ilivyo kawaida ninaposafiri kwa kazi za uchunguzi, siku hii pia nimejiandaa vilivyo kwa ajili ya kukabiliana na mazingira ya safari. Nimevaa jeans nyeusi, fulana ya mistari na raba huku nimebeba begi dogo ili iwe rahisi kupanda na kushuka na hata kujipweteka kwenye gari.

Mazingira ya safari yananilazimisha niwe hivyo. Nimepanga kutumia usafiri wa lori la mizigo linalosafiri kati ya Dar es Salaam na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Wakati nafikiria kusafiri kwa lori nilifanya utafiti kwa wafanyabiashara wa kike wanaotumia usafiri wa malori yaendayo Zambia ili nijue mambo ya msingi na ya kuchukua tahadhari.

“Safari ni ngumu, ndefu, inachukua siku hadi tatu kufika Tunduma. Vaa kiskauti lakini kati ya yote shoga yangu usisafiri na dereva usiyefahamiana naye,” alinitahadharisha dada mmoja mzoefu wa kusafiri kwa malori yanayoanzia yadi iliyo karibu na ofisi za Mwananchi.

Ni kweli sikuwa namjua dereva, lakini msimamizi wa malori ya kampuni ya RST Investment (siyo jina halisi) alinihakikishia usalama. Msimamizi huyo nilimwambia nia yangu ya kusafiri kwa lori kwa lengo la kufanya uchunguzi wa biashara ya uchangudoa njiani, ulevi, mwendo wa madereva, rushwa kwa trafiki na ajali.

Msimamizi huyo aliahidi kunichukua au kunitafutia dereva mwaminifu. Alinitaka nijiandae kwa safari siku yoyote kuanzia Juni 19, ambayo atakuwa amepakia mzigo. Usiku wa Juni 18 alinipigia simu kunijulisha kuwa safari imeiva na kwamba nitasafiri na dereva aitwaye Temba hivyo nifike kituoni mapema kwa kuwa safari itaanza saa 2.00 asubuhi.

Usiku huo sikupata usingizi wa haja kutokana na kufikiria mazingira ya safari, usalama na afya yangu, hasa kusafiri na dereva nisiyemjua hata kama nimetambulishwa kwake kama dada wa msimamizi wa kampuni. Pili, nilifikiria umbali, siku nitakazotumia njiani pamoja na namna nitakavyofanikisha kazi yangu.

Ili nisiwe abiria msumbufu, siku hii nadamka mapema na baada ya kujiswafi ninachukua bodaboda kuhakikisha nafika Mbezi Kwa Msuguri mapema zaidi.

Baada ya kushuka, nayaona malori kadhaa mengine yakiwa yamewashwa ili kupasha injini huku madereva na utingo wakiyakagua kabla ya kuanza safari. Naamua kumpigia simu dereva niliyepangiwa kusafiri naye.

“Halo, habari za asubuhi kaka,” namsalimu naye anaitikia na kunisabahi na baadaye najitambulisha.

“Naitwa Doreen. Wewe ni kaka Temba, nimepewa namba hii na kaka Mambeya kwamba nitasafiri na wewe,” ninamweleza.

“OK, tazama yaliko malori,” anasema Temba huku akiwa amenyanyua mkono akiniita kwa kunipungia. Navuka barabara kuelekea alipo ambako kuna lori refu aina ya Scania lililo na tanki la mafuta.

“Ok Doreen, naitwa Mustafa Temba (si jina lake). Umesema unaitwa Doreen eh?” ananiuliza nami namkubalia na ndipo ananikaribisha kwa bashasha na kuniambia nisubiri wakamilishe taratibu za kupitia nyaraka muhimu.

Temba, dereva mwingine wa lori la kampuni hiyo na utingo wao wanazungumza huku wakihakiki nyaraka na magari yao ambayo yamewashwa kwa ajili ya kupasha injini na baada ya muda ananifuata.

Safari inaanza

“Haya panda tuondoke,” anasema Temba huku akinifungulia mlango wa upande wa kushoto.

Baada ya kuingia nagundua kuwa sehemu au chumba cha dereva ni pana; kuna kiti kwa ajili ya wasaidizi wake wasio abiria na nyuma ya kiti kuna vitanda viwili juu na chini. Wakati wa safari kitanda cha chini hutumika kama kiti kwa ajili ya ‘abiria’, lakini usiku hugeuzwa kitanda.

Safari inaanza. Katika lori hili nipo mimi na Temba tu, hakuna hata utingo lakini lori jingine la kampuni hiyo ya RST kuna dereva aitwaye January (si jina halisi) na utingo wawili. Kama kawaida yangu naomba dua ili Mwenyezi Mungu aniepushie balaa zote; aibariki safari nifike na nirudi salama.

Dua hiyo inatosha kumjulisha dereva kuwa mimi si kati ya waombao lifti kwa ajili ya kwenda Tunduma kufanya ukahaba. Dereva anapoliweka sawa gari barabarani nagundua kuwa ni la kisasa, halina mtikisiko mkubwa lakini najiuliza sababu za kuwa peke yake wakati kanuni inataka madereva wa magari ya masafa marefu kuwa wawili. Je, ni mtego?

Temba anaonekana mchangamfu na ananihoji maswali kadha wa kadha kutaka kunijua zaidi, sehemu ninakokwenda na lengo la safari.

“Umesema unaitwa Doreen?” ananiuliza kana kwamba amesahau.

“Umewahi kusafiri kwa malori au ni mara yako ya kwanza?” anauliza.

“Ni mara ya kwanza,” namjibu.

“Kama ni mara ya kwanza, usitarajie kufika leo leo Tunduma kwa sababu hatutakiwi kukimbia kama mabasi,” anasema nami nakubaliana naye.

Ukweli ni mara yangu ya kwanza kusafiri kwa lori, lakini si kupita njia hiyo. Nimewahi kusafiri kwa mabasi hadi Iringa, pia nimewahi kusafiri hadi Sumbawanga lakini kwa lori ni uzoefu mpya.

“Huko ni nyumbani au unakwenda kikazi,” ananiuliza.

“Mimi ni mfanyabiashara, nitakaa kidogo Tunduma lakini nakwenda Nakonde,” namjibu kwa uangalifu sana ili asinishtukie.

Temba anafurahia majibu hayo na anaanza kuzungumzia uzoefu wake wa kusafiri Zambia, DRC, Burundi, na Rwanda. Anasema hadi Nakonde, katika Jimbo la Muchinga, Zambia ni safari ya zaidi ya kilomita 1,000.

Saa 2.30 asubuhi tunafika kituo cha ukaguzi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Visugusu, Kibaha mkoani Pwani. Tofauti na January ambaye utingo ndiyo hushuka na kupeleka nyaraka ili zikaguliwe kituoni, Temba anashuka mwenyewe ili kukamilisha kazi hiyo.

Baada ya kumaliza mchakato wa ukaguzi ambao unachukua muda kiasi anarudi kwenye gari na kuniuliza: “Utatumia kinywaji gani?”

“Nitakunywa maji,” namjibu na ninapomuangalia usoni namuona anashangaa

“Hutumii pombe kabisa?” anauliza kana kwamba asiyeamini jibu langu.

“Hapana situmii, maji yananitosha,” namjibu kwa msisitizo.

Temba haamini majibu yangu, lakini analazimika kukubali. Anarudi ndani ya gari akiwa na paketi ya viroba ambayo anafungua moja na kukata na kukimiminia mdomoni mwake hadi nusu, na nusu iliyobaki anaiweka kwenye ‘dashboard’.

Safari yetu inaanza vizuri na gari linashika kasi huku tukipata burudani ya muziki wa kizungu.

Kwa mara ya kwanza naanza kupata hofu ya safari na anayenisababishia hofu ni dereva mwenyewe kwa namna anavyokunywa viroba. Temba akimaliza kiroba kimoja anachukua kingine na kumiminia mdomoni kama maji huku akiendesha kwa kasi.

“Sijui nimuulize kama ataweza kuendesha akiwa amelewa? Akifurahi atanijibu vizuri akichukia nitakuwa nimemkorofisha,” najisemea. “Maji ukishayavulia nguo huna budi kuyaoga,” najipa moyo.

Ukweli, kila ninapomtazama akiongeza viroba napata shida. Najitahidi kuwa macho lakini mara najikuta nimesinzia. Barabara ni nzuri, magari ‘yanateleza’.

Ajali mbili

Tunapofika eneo la Mbala, Chalinze tunashuhudia ajali ya lori aina ya Mitsubishi Canter lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Dar es Salaam limepinduka kichwa chini miguu juu.

Kazi yangu ya kujua sababu za ajali inaanzia hapo. Maelezo ninayopata nayahifadhi kichwani bila kuandika popote ili Temba asinishtukie. Mashuhuda wa ajali hiyo wanaeleza kuwa dereva wa lori alikuwa katika mwendo wa kasi na alipokuwa akimkwepa mwendesha bodaboda, akapinduka.

Majibu hayo yananiongezea hofu zaidi juu ya kasi ya lori nililopanda huku dereva akipiga viroba. Natumia simu yangu kuandika ili kuhifadhi matukio.

Tunakutana na ajali nyingine eneo la Mikese iliyohusisha lori la mizigo lililokuwa linatoka Tunduma kwenda Dar es Salaam. Taarifa tulizozipata ni kuwa dereva alikuwa amesinzia.

Pia, katika eneo hilo la Mikese tunaikuta ajali nyingine ya lori ambalo liliacha njia na kuingia vichakani na kupinduka. Kwa bahati mbaya dereva alikufa. Utingo ananieleza kuwa yeye na dereva wake walipitiwa na usingizi.

Hadi hapo ninajiridhisha kwamba malori mengi hupata ajali za barabarani kuliko mabasi. Pia, najisemea moyoni kwamba sababu za ajali hizi ni usingizi na mwendokasi. Sasa kama ni usingizi kwa nini wasilale njiani Kwa nini wanajilazimisha kuendesha usiku kucha?

ITAENDELEA KESHO