Prime
Simulizi za jiwe ‘linaloongea’ Iringa
Muktasari:
- Hili ndilo jiwe Gangilonga linalobeba jina la kata maarufu ya Gangilonga na kufanikiwa kuua jina la zamani la Uzunguni.
Iringa. Wenyeji wa Mkoa wa Iringa huliita Gangilonga yaani Liganga Lelilonga wakimaanisha ‘Jiwe linaloongea’.
Inaaminika mtawala wa zamani wa kabila la Wahehe Chifu Mnyigumba, baba yake Chifu Mkwawa alikua analitumia jiwe hilo kuzungumza na mizimu kuhusu masuala mbalimbali ya utawala wake.
Hili ndilo jiwe Gangilonga linalobeba jina la kata maarufu ya Gangilonga na kufanikiwa kuua jina la zamani la Uzunguni.
Wakati wa utawala wa kikoloni, uzunguni walikuwa wakiishi matajiri, watawala na ndiko ilikokuwa Ikulu.
Hata baada ya jina la Gangilonga kuanza kutumika, Ikulu ya Mkoa wa Iringa imebaki eneo hilo.
Mpaka sasa watu mashuhuri wa Mkoa wa Iringa, wakiwemo viongozi mbalimbali kama mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wanaishi Gangilonga.
Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), kupitia mradi wake wa Fahari Yetu kimefanya utafiti na kubaini sio tu kwamba jiwe hilo lilitumika kama eneo la ‘matambiko’ ya Wahehe na hapo ndipo dhana ya kuzungumza ilipoanza.
“Gangilonga maana yake ni jiwe linalozungumza, tumefanya utafiti na kugundua mengi kuhusu jiwe hili. Ibaki kusema ni jiwe linalozungumza kwa sababu wazee akiwemo baba yake Chifu Mkwawa, alitumia jiwe hili kuzungumza na mizimu,” anasema Jimson Sanga, mhadhiri wa UoI.
Sanga anasema inasadikiwa kwamba jiwe hilo lilimsaidia Chifu Mnyigumba kumtabiria mambo mengi yaliyosaidia kuimarisha utawala wake.
Inasadikiwa kuwa hata baada ya mzee Munyigumba kufariki, mwanawe aliyerithi utawala wake, Chifu Mkwawa aliendelea kutumia jiwe hilo kwa tafsiri ya mambo ya mbele kitu kilichomsaidia kushinda vita mbalimbali vikiwemo vile vya Wajerumani na makabila mengine.
Uzuri wa jiwe la Gangilonga
Unapokua juu kabisa ya jiwe hilo unapata fursa kuona vizuri mandhari ya mji wa Iringa, jambo ambalo limekuwa likiwavutia wengi hasa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Ukweli ni kwamba, kati ya maeneo unayoweza kufurahia na kuvutiwa nayo ukiwa mjini Iringa ni kutembelea Jiwe la Gangilonga.
Juu ya jiwe hilo kuna eneo tambarare ambalo watu 50 wanaweza kuketi kwenye viti na kufanya mkutano wao bila wasiwasi wowote.
Watalii wengi wanaoingia kutembelea katika mji wa Iringa wamekuwa wakifurahia utalii wa Kuzama Jua ‘Sun-set’ wanapokuwa juu ya jiwe hilo.
Sanga anasema baada ya kugundua jiwe hilo linaongeza chachu ya utalii wa asili, waliamua kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa katika kuendeleza utalii kupitia jiwe hilo.
Mmoja wa wazee wa Iringa, Vangile Wikesi anasema uzuri wa jiwe hilo ndio ambao uliifanya kata hiyo ibadilishe jina, badala ya kuitwa uzunguni itumie jina la Gangilonga.
Simulizi ya Gangilonga
Zipo simulizi nyingi za kusisimua kuhusu Jiwe la Gangilonga kubwa ikiwa ni matambiko.
Sanga anasema walipata nafasi ya kukutana na wazee ambao walidai kusimuliwa mambo mengi na wazee wao ambao wengi hawapo duniani.
Wazee hao wanasisitiza kuwa kulichosababisha jiwe hilo kuitwa Gangilonga ni kwa sababu kuna sauti walikuwa wanazisikia na ndio maana likatumika kama sehemu ya matambiko.
“Wao wametafsiri kutokana na matumizi yao ya kila siku. Walitumia jiwe hili kuomba mvua, kushukuru kwa kwa kupata mavuno, matambiko ya kujiandaa au kujikinga na vita, matambiko ya kupata uzao kwenye familia na mengine,” anasema na kuongeza;.
“Sasa suala la jiwe kuzungumza ni la kiimani, kama kwenye vitabu vya Mungu kuna maandiko yanasema nyoka alizungumza, nyoka anaongeaje? Haya ni masuala ya kiimani zaidi,” anasema Sanga.
Latumika kama kamati ya ufundi
Sanga anasema katika tafiti zao waligundua kwamba jiwe hilo lilitumika kama kamati ya ufundi wakati wa vita kati ya Mkwawa na Wajerumani.
“Inasadikika kwamba ni jiwe ambalo wakati wa maandalizi ya vita lilitumika kuomba nguvu, kutambika au kuomba uwezo. Ilikuwa ni kamati nyeti na watumia mahali hapo kutambika,” anasema.
‘Moja ya maeneo muhimu ya Wahehe kutambikia inasadikika ni pale Gangilonga,” anasema.
Juu ya jiwe hilo kuna eneo kubwa na chini yake kuna pango ambalo lilitumika kama nyumba ya ibada kwa ajili ya kutambika.
Tafsiri ya mwangwi
Wapo watu ambao wanaamini suala la jiwe hilo kuzungumza ilikuwa ni mwangwi wake.
“Wapo wanaoamni kwamba kwenye jiwe hilo ilikuwa mtu akipiga kelele kuna sauti nyingine inatokea lakini kwenye simulizi zetu wazee, hatukuambiwa kwamba walikuwa wanapiga kelele, lakini taarifa muhimu tulizonazo ni miongoni mwa maeneo matakatifu ya kimila,” anasema Sanga.
Kwa nini Gangilonga?
Simulizi za Gangilonga yenyewe ni thamani kubwa kwa utalii wa Mkoa wa Iringa, ukiwamo utalii wa kuzama jua.
“Sisi Fahari Yetu tumeweka pale bango kwa ajili ya kutoa elimu kwa wageni na wanaopita ili waelewe kuhusu jiwe hilo,” anasema na kuongeza;
“Ukiwa juu ya jiwe unaona sehemu kubwa ya mji wa Iringa juu yake na unaweza ukatembea juu ya jiwe na kupiga picha za kufurahisha,” anasema.
Anasema kutokana na jiwe hilo kuzungukwa na miti, waliona umuhimu wa kuweka huduma za kibinadamu kama kibanda cha mlinzi na vyoo.
“Majengo hayo yapo na huduma za vyoo sijui kama zipo kwa sababu ya shida ya maji,” anasema Sanga.
Suala la jiwe kuongea
“Ukweli ni kwamba, hakuna kitu kinachoweza kuongea haya masuala ni ya imani. Ni kuamini tu kwamba linaongea,” anasema.
Anasema vitu vya asili vinavyotumika kwenye matambiko vinapaswa kuwa vitakatifu lakini kwa sababu ya matumizi yasiyo sahihi.
‘Ili Gangilonga liendelee kung’aa lazima tuheshimu simulizi tulizorithishwa na wazee wetu zamani,” anasema.