Sio Boeing Max pekee, kuna ndege nyingine mbili

Ndege mbili aina ya CESSNA 172S Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) zikiwa kwenye kwa ajili ya mafunzo ya urubani zikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. 

Muktasari:

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) leo Jumanne Oktoba 3, 2023 saa tisa alasiri, litapokea ndege mpya ya Boeing 737-9 Max kutoka Seattle, Marekani. Hii ni ndege ya 13, ikiwa ni pamoja na ya mizigo. Pia, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kitapokea ndege mbili za mafunzo, CESSNA 172S.

Dar es Salaam. Hafla ya mapokezi ya Boeing 737-9 Max ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inayotarajiwa kuwasili Tanzania leo Jumanne Oktoba 3, 2023 saa tisa alasiri, itaambatana na mapokezi ya ndege nyingine mbili ndogo za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Ndege hiyo ya ATCL inayotarajiwa kuwasili ikitokea katika Jiji la Seattle, Marekani ni ya 13 ya shirika hilo ikiwamo ya mizigo moja.

Mwananchi Digital imezishuhudia ndege hizo mbili aina ya CESSNA 172S zikiwa zimeegeshwa leo Oktoba 3, 2023 katika eneo la karibu na jukwaa la mgeni rasmi.

Mapokezi ya ndege hizo mbili za NIT yataifanya taasisi hiyo kuwa na uwezo wa kudadhili wanafunzi 10 wa taaluma ya urubani kwa mkupuo.

Ndege hizo zitaiwezesha NIT kutoa mafunzo ya urubani daraja la awali (PPL) kwa miezi sita kwa ada ya Sh21 milioni, daraja la biashara (CPL) kwa miezi 12 kwa Sh53.8 milioni, badala ya Sh300 milioni za mafunzo hayo nje ya nchi.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa amesema ndege hizo ambazo ni za kwanza kwa taasisi hiyo zililetwa Januari mwaka jana kutoka Marekani na zilifikia Dodoma kwa ajili ya kuunganishwa.

"Zilikuja ndani ya containers (makontena), zimeunganishwa Dodoma. Hapa Dar es Salaam zilikuja juzi," amesema Profesa Mganilwa.

Amesema ndege hizo mbili kila moja ina injini moja na kwamba  chuo hicho kipo mbioni kupata ndege nyingine yenye injini mbili ambayo amesema malipo ya awali yameshafanyika.