Siri biriani kuliwa Ijumaa

Muktasari:

  • Maeneo mengi katika mikoa ya pwani na Zanzibar, biriani hupikwa Ijumaa na walaji wameelekeza akili zao kutafuta chakula hicho siku ya Ijumaa na si siku nyingine katikati ya wiki.

Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza ni kwanini biriani huliwa zaidi siku ya Ijumaa? Mwanazuoni wa dini ya kiislamu, wapishi na walaji wa chakula hicho wanatoboa siri hiyo.

Biriani asili yake ni nchi za India na Uarabuni. Chakula hiki hupikwa kwa kutumia mchele maalumu unaojulikana kwa jina la pishori au mchele wa biriani.

Ili unukie huwekwa viungo mbalimbali ikiwemo karafuu, zafarani, giligilani, mdalasini, hiliki na majani ya mbei.

Katika mapishi hayo, pembeni hupikwa mchuzi mzito wa nyama ama ya kuku, ng’ombe au nyama yoyote ikiwa imechanganywa vitu mbalimbali kama mtindi, vitunguu maji, vitunguu saumu, tangawizi iliyotwangwa, limao na nyanya ya kopo au ya pakti.

Hata hivyo, mara nyingi chakula hiki katika maeneo mengi hupikwa na kuliwa zaidi Ijumaa, ambapo awali ilikuwa zaidi mikoa ya Pwani, lakini sasa kutokana na mwingiliano wa watu, mikoa mingine nako wanakula chakula hiki.


Kwanini Ijumaa?

Licha ya kuwa wengine wanapika biriani siku yoyote wanayojisikia, maeneo mengi ikiwemo hotelini wanapendelea kupika chakula hiki siku ya Ijumaa.

Mwananchi limefanya mahojiano na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la WaislamTanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anayeeleza biriani inapikwa Ijumaa kwa sababu siku hiyo kwa Waislamu ni sikukuu, pia ni siku ya mapumziko ambayo watu huitumia kujumuika pamoja.

“Katika dini ya kiislamu, kuna sikukuu tatu; sikuku ya Eid El- Fitri, Eid El Hajj na sikukuu ya wiki ambayo ni Ijumaa.

“Hivyo, moja ya mambo wanayopaswa kufanya ni kula vizuri kuliko siku nyingine zinavyokuwa ambapo moja ya chakula pendwa ni biriani ukiachana na pilau,” anasema Sheikh Mataka.

Hata hivyo, amesema hii haimaanishi kwamba watu wasile vizuri siku nyingine, kwani hata dini inasema mtu anapaswa kula vizuri kila siku tena mlo kamili.

Lakini anabainisha  kwa kuwa ni utamaduni wa tangu enzi na enzi, sikukuu watu wanakula tofauti na siku nyingine na biriani ni chakula pendwa kwa kuwa huwezi kukipika kila siku.

“Hii pia imekuja kujenga mazoea katika hoteli mbalimbali kupenda kupika chakula siku ya Ijumaa kwa kufuatisha watu wanavyopenda, kwani huwa na uhakika wa kupata wateja.

“Pia, kwa sasa walaji wa chakula hicho si tu waislamu pekee, bali hata waumini wa dini nyingine,”anasema Sheikh Mataka.

Rukia Abdu, mmoja wa wafanyabiashara wa chakula maeneo ya Tabata, hakuwa mbali na Sheikh Mataka, anaeleza wateja wake wengi wa biriani ni wa Ijumaa.

“Siku za kawaida unaweza kupika biriani ikakudodea, lakini sio Ijumaa, kwani ni kama kautamaduni kamejengeka hivi, hata ukipita kwenye hoteli au migahawa mbalimbali utaona wameandika leo Ijumaa biriani ipo hapa na sio leo Jumatatu biriani ipo hapa,” anasema Rukia.

Mmoja wa wateja aliyejitambulisha kwa jina la Daud Msele, mkazi wa Dar es Salaam, anasema amejiwekea ratiba kila Ijumaa lazima ale biriani kwa kuwa anajua ndio ataipata ile yenyewe inayopikwa na watu wanaoijua kwa kuwa vijiwe hivyo vinajulikana vilipo.

Kwa upande wake, Shamsa Tamimu anasema kwake chakula hicho huwa kitamu zaidi anapojumuika na wenzake Ijumaa, kwani ndio wikiendi kwao huanza na  huenda kuagiza wakiwa watu wasiopungua watano kwa kuwekewa kwenye sinia ambalo bei yake ni Sh20,000.

“Mkiwa wengi chakula hiki ndio kinanoga kuliko kula mwenyewe, halafu raha zaidi ukishushia na sharubati (juice) ya muwa ya baridi au shurubati ya matunda mengine,” amesema.