Prime
Siri mauaji kutikisa
Muktasari:
- Miongoni mwa matukio ya mauaji yanahusisha wanandoa kuuana, wazazi kuua watoto na ugomvi wa watu walio karibu.
Dar/mikoani.Wakati matukio ya mauaji na vitisho yakiendelea kushika kasi nchini, viongozi wa dini na wanasaikolojia wameitaka Serikali kuingilia kati ikiwa ni pamoja na kuboresha afya ya akili kwa wananchi.
Baadhi ya waliozungumza na Mwananchi Digital kuhusu matukio hayo wanahoji uwezo wa akili za watu kudhibiti hisia zao.
Miongoni mwa matukio hayo yanahusisha wanandoa kuuana, wazazi kuua watoto na ugomvi wa watu walio karibu.
Kwa kipindi cha takribani miezi mitatu, Mwananchi Digital imesharipoti matukio 16 yaliyosababisha vifo vya watu takribani 20.
Tukio jipya ni lililotokea leo Aprili 2 2024, ikielezwa kuwa Ofisa Kilimo wa Kata ya Neruma, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, Julius Rubambi (38), amefariki dunia akidaiwa kuchomwa kisu na mke wake baada ya kutokea ugomvi kati yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase, amesema tukio hilo lilitokea leo eneo la Kibara wilayani Bunda, saa nne asubuhi, akimtaja mtuhumiwa kuwa ni Elizabeth Steven (30), ambaye anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi.
Alisema taarifa za awali zinadai wanandoa hao walikuwa na ugomvi, mume alimtuhumu mke wake kuwa na uhusiano mwingine, hivyo kuwapo majibizano yaliyoibua ugomvi kati yao.
Mbali ya hayo, Machi 29, 2024 gari la mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka lilishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Alipoulizwa kuhusu matukio hayo leo, Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime alisema kabla ya kutoa majibu yoyote ni lazima aangalie pia na taswira ya nchi.
Hata hivyo, hakutaka kufafanua zaidi akisema: “Kama ni Jeshi la Polisi kujipanga, ulishawahi kuona wapi mtu anauza ramani ya vita.”
Akihubiri wakati wa ibada ya Pasaka Machi 31, 2024 katika Usharika wa Azania Front jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, alisema tukio la kushambuliwa gari la Ole Sendeka ni ishara ya kutoweka kwa amani.
“Mimi nina uhakika wale wenye mamlaka watalisimamia jambo hili ili Tanzania yetu iendelee kuwa ya amani kwa sababu ndiyo sifa ya bwana (Yesu) anayefufuka,” amesema.
Katika tukio hilo, gari la Ole Sendeka lilishambuliwa kwa risasi akiwamo ndani pamoja na dereva wake eneo la Ndaleta.
Akiwasilisha ripoti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, akizungumzia ukaguzi wa ufanisi, aliitaja Wizara ya Afya kama mfano wa ufanisi mdogo kwenye eneo la afya ya akili.
“Napendekeza kuongeza fedha kwa ajili ya huduma ya afya ya akili hasa katika ngazi ya jamii, pia kwa ajili ya wataalamu zaidi wa afya ya akili, na kuboresha miundombinu na vifaatiba katika vituo vya afya, kuhakikisha huduma ya kisaikolojia zinapatikana kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya jamii.”
“Pia kuanzisha vituo vya utengamo katika mikoa yote ili kuboresha ujuzi, wataalamu na kusaidia wagonjwa kupona,” alisema Kichere.
Viongozi wa dini, wanasaikolojia wazungumza
Mwanasaikolojia, Jacob Kilimba alisema chanzo cha kukithiri kwa mauaji katika jamii, ni kutokana na watu kuiga na kufanya masuala hayo kama suluhisho wanapokumbwa na matatizo.
“Matatizo haya yanatokana na habari zilizoenea na jinsi watu wanavyojenga tabia kutokana na habari hizo. Kwa mfano, zamani tulisikia watu wa Iringa wanajiua sana, kwa sababu wameshaona wengine wanafanya hivyo kwa hiyo tabia inajengeka, kwamba ikishindikana hivi, suluhisho ni kuua.
Alishauri pia watu kupima afya kwa kwenda hospitali kuzungumza na madaktari.
“Mtu unaweza kwenda hospitali hata kama huumwi chochote, msimulie daktari maisha yako ukimweleza jinsi unavyotatua shida zako, anaweza kujua tatizo liko wapi na kukupa ushauri,” alisema.
Akizungumzia matukio hayo, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma, alisema yanapaswa kukemewa.
Alisema ni wakati sasa Serikali ifanye uchunguzi wa kina na kuwasaka wote waliohusika na matukio ya kushambulia kwa risasi na ya mauaji.
“Tukio kubwa kama hili (la kushambuliwa Ole Sendeka) ingawa hatujafahamu chanzo ni nini, ni la kukemea, lakini pia Serikali ijitahidi kuwasaka na kuchukuliwa hatua. Kwa ujumla yote ni matukio ya kukemea na kulaani,” alisema Sheikh Mruma.
Mratibu wa huduma za makundi maalumu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Daniel Sendoro alisema matukio kama hayo ni vitendo vya kikatili, hivyo vinapaswa kukemewa.
Alisema ili kuepuka matukio hayo, binadamu anapaswa kupuguza idadi ya maadui anaoishi nao lakini pia kukaa karibu na Mungu.
“Uadui hauwezi kutokea kama hakuna kitu kibaya kama vile dhuluma, uonevu au chuki mambo haya yanapaswa kukemewa lakini tuishi kama ndugu tukiepuka visasi,” alisema Mchungaji Sendoro.
Akihubiri wakati wa ibada ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Handeni, Mchungaji wa kanisa hilo na mkuu wa Jimbo la Magharibi, Ismail Ngoda alisema amani inatakiwa kuwepo katika ngazi zote ili kuzuia uhalifu.
Alisema watu wanatakiwa kuepuka mambo ambayo yanaweza kuleta uvunjivu wa amani katika familia, kwani kwa sasa wanaume na wanawake wote wamekuwa wakifanya ukatili kwa nyakati tofauti, sababu kubwa ni kukosekana amani katika mioyo na familia zao.
Mchungaji Ngoda alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakifanya ukatili kwa wanaume zao, chanzo cha yote ni kukosekana amani na imani kwa watu.
Matukio ya mauaji
Katibu wa Jimbo la Chaani wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kaskazi Unguja, Ali Bakari Ali (62) aliuawa kwa kuchomwa kisu.
Chama hicho kilidai aliuawa na majambazi waliokimbia kusikojulikana. Lakini Polisi mkoani humo walidai waliomuua walikuwa wanafanya naye biashara na tayari wamekamatwa.
Wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Mohamed Salanga (37) anadaiwa kumuua mkewe Beatrice Ngongolwa kisha kuufukia mwili wake chini ya kitanda ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi.
Mauaji ya Beatrice (32), mkazi wa Sekutari, yalidaiwa kutokea usiku wa Desemba 31, mwaka jana na mazishi kufanyika Januari Mosi, 2024.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, alisema Salanga alikamatwa Machi 21, 2024 na tayari alishafikishwa mahakamani. Mwili wa Beatrice ulifukuliwa na kuzikwa upya.
Mkoani Kilimanjaro mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mrupanga, Wilaya ya Moshi, Jonathan Makanyaga (6), alifariki dunia ikidaiwa ni kutokana na viboko alivyochapwa na mwalimu tarajali wa mafunzo ya ualimu aliyekuwa akifundisha shuleni hapo.
Mwanafunzi huyo, mkazi wa Kijiji cha Kimanganuni Chini, kata ya Uru Kusini, alifariki dunia Machi 10, mwaka huu, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi mkoani Kilimanjaro liliwakamata walimu watano tarajali na kuwahoji.
Tukio lingine lilitokea wilayani Rombo, ambako watu wanne walishikiliwa na Polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji ya fundi uashi, Benson Machui (30), aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na kisha mwili wake kutelekezwa katika ofisi ya Kijiji cha Mamsera Juu, wilayani humo.
Kijana huyo mkazi wa Kijiji cha Old Moshi, alikuwa akijishughulisha na ujenzi wilayani Rombo, aliuawa usiku wa Januari 14, 2024 alipotoka kuangalia mpira.
Februari 8, 2024 Polisi lilimkamata Sofia Kimaro (48), mkazi wa Kijiji cha Ushili wilayani Arumeru kwa tuhuma za kumuua mumewe Estomii Nnko (59) kwa kumkata na shoka kichwani.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mathias Timothy alisema walipata taarifa asubuhi ya Februari 7, 2024.
Tukio lingine ni la dereva wa pikipiki, Amedius Mfoi (25) mkazi wa Muriet, aliyedaiwa kumuua kwa kumchinja mtoto wake, Amani mwenye umri wa miaka mitatu kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.
Tukio hilo lilitokea Januari 23, 2024 saa 12 jioni katika mtaa wa Muriet, jijini Arusha. Mtuhumiwa anadaiwa baada ya kumkata shingo mtoto kwa kitu chenye ncha kali alitenganisha kichwa na kiwiliwili na kisha kuviweka kwenye ndoo ya maji na kufunika.
Mkoani Mbeya mwalimu wa Shule ya Msingi Mbugani, Herieth Lupembe (37) na binti aliyekuwa akiishi naye Tatizo Haonga (16), waliuawa wakiwa ndani ya nyumba wanaoishi katika kijiji cha Mbugani, Kata ya Kiwanja, wilayani Chunya.
Tukio hilo lililotokea Machi 31, mwaka huu saa 2.30 usiku. Waliuawa kwa kupigwa na vitu vyenye ncha kali mwilini.
Happiness Mwinuka (40), aliuawa kwa kuchinjwa shingo na mume wake, Ombeni Kilewa (43), baada ya kumtuhumu kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine.
Tukio hilo lilitokea Machi 14, mwaka huu katika Kijiji cha Lusese wilayani Mbarali mkoani Mbeya. Mtuhumiwa alikamatwa na Polisi.
Katika tukio lingine, watoto Mario Adamson (4) na Beonis Adamson (2) walifariki dunia baada ya kunyweshwa sumu na mama yao mzazi, Dainess Adamson.
Tukio hilo lilitokea Machi 5, mwaka huu katika kijiji cha Mashese, Mbeya Vijijini.
Jijini Dodoma katika Kata ya Nala, yalitokea mauaji ya mama na binti yake waliodaiwa kuchinjwa na mume wa binti huyo kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Waliouawa ni Anna Manyehe (63) na mwanaye Maria Lubeleje (42), ambao walikutwa wameuawa jikoni. Mtuhumiwa alitajwa kuwa ni Festo Maganga.
Katika tukio hilo lililotokea Januari 28, 2024, Maganga hata hivyo, aliuawa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.
Mkoani Kigoma, mkazi wa Mtaa wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Rashid Mkayala (38), alituhumiwa kumuua mkewe, Benadetha Cosmas (34), kwa kumnyonga hadi kufa.
Mtuhumiwa naye alijinyonga kwa kutumia kitambaa cha kichwani, chanzo kikitajwa kuwa ugomvi baada ya mke kumtuhumu mume kuuza vitu vya ndani. Tukio hilo lilitokea Februari 21, 2024.
Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya liliripoti kumkamata Marwa Meng'anyi (40), mkazi wa kijiji cha Keroti wilayani Tarime kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa miezi minne ili apate fedha kutoka kwenye kikundi cha kusaidiana, kisha alipe madeni.
Mbali na hilo, wilayani Musoma polisi liliwakamata watu wawili wakituhumiwa kwa mauaji ya mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Magharibi, Wilaya ya Butiama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase alimtaja mwanafunzi aliyeuawa ni Kambarage Reuben (8), mkazi wa kijiji cha Mwibagi wilayani Butiama. Mauaji yalitokea Februari 8, 2024 jirani na shule alipokuwa akisoma mwanafunzi huyo.