Anayedaiwa kuua mke na kumfukia ndani apandishwa kizimbani
Muktasari:
- Anayedaiwa kumuua Beatrice na kumfukia ndani afikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manne, arudi mahabusu kwa kukosa wadhamini.
Morogoro. Mohamed Salanga (37) mkazi wa Kimamba wilayani Kilosa anayedaiwa kumuua mkewe Beatrice Ngongolwa (32) amefikishwa mahakamani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro na kusomewa mashtaka manne likiwemo hilo la kuua na kubaka.
Wakisoma hati ya mashtaka yanayomkabili mshtakiwa huyo mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo Renatus Barabara mwendesha mashtaka wa Serikali Elizabeth Marya na mwenzake Jacklin Nyoka wameyataja mashtaka hayo kuwa ni kuua, kufanya ukatili kwa watoto wawili na kumbaka mtoto mmoja ambao wote ni watoto wa marehemu Beatrice.
Mshtakiwa huyo alianza kusomewa shitaka la kuua ambapo mwendesha mashtaka Mary amedai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo Januari 1 mwaka huu ambapo alimuua Beatrice Kwa kumpigia na kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba kwenye chumba walichokuwa wakiishi.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo na hivyo ilihairishwa hadi Aprili 9 mwaka huu kesi hiyo itakaporudishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Katika mashtaka mengine yaliyosomwa na mwendesha mashtaka Jacklin Nyoka imedaiwa mahakamani hapo kwamba kati ya Aprili 2023 hadi Januari mwaka huu mshtakiwa huyo alimbaka mtoto wa miaka 12 ambaye ni mtoto wa marehemu Beatrice na hivyo kumsababishia maumivu makali na kumuathiri kisaikolojia.
Mwendesha mashtaka huyo ameendelea kudai kuwa katika kipindi hicho hicho kilichotajwa mshtakiwa alimfanyia tena ukatili mwingine mtoto huyo kwa kumpigia na kumng'oa meno mawili, kumchoma na moto mapajani, kumtoboa na misumari sehemu mbalimbali za mwili na kumpigia na rungu kichwani.
Katika shtaka la nne nne linalomkabili mshtakiwa huyo, mwendesha mashtaka huyo amedai kuwa mshtakiwa alimfanyia ukatili mtoto wa miaka tisa ambaye naye ni mtoto wa marehemu Beatrice kwa kumchoma na moto mdomoni, makalioni, kumtegua mkono, kumng'oa meno na kumtoboa sehemu za siri.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo ya ukatili mshtakiwa amekana kutenda makosa hayo hata hivyo mwendesha mashtaka huyo amedai kuwa mshtakiwa anayo haki ya kudhaminiwa katika mashtaka hayo ya ukatili kama atatimiza masharti ya dhamana.
Kufuatia hayo hakimu Barabara ameainisha masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mwenye mali isiyopungua Sh5 milioni na isiyohamishika,kuwa na mdhamini atakayesaini dhamana ya Sh5 milioni, wadhamini watatu ambao kila mmoja atakuwa na barua ya utambulisho kutooka Serikali ya mtaa, kitambulisho Cha Taifa ama kadi ya kupigia kura.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshindwa kutoka kwa dhamana baada ya kukosa wadhamini wenye sifa hizo, ambapo alidai kwa sasa bado hajapata watu wa kumdhamini labda wiki ijayo anaweza kuwapata.
Kutokana na kukosa wadhamini mshtakiwa huyo amerudishwa rumande hadi Machi 28 ambapo kesi hiyo ya ukatili itarurudi mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizaji wa maelezo ya awali.