Siri sanamu za hayati Nyerere kuzusha utata

Dar es Salaam. Wataalamu wa uchongaji, ufinyanzi na uchoraji wametaja sababu zinazoweza kufanya sanamu kushindwa kubeba mfanano wa mtu husika, ikiwamo kukosekana uwiano halisi na vipimo.

Mbali na hayo, wameshangaa kuendelea kuwapo sanamu ambazo hazina uhalisia, wakieleza hivi sasa teknolojia imerahisisha kila kitu ikiwamo utengenezaji sanamu.

Wametoa kauli hizo siku moja baada ya kuzinduliwa sanamu la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Sanamu hilo limezua gumzo mitandaoni, huku watu wengi wakieleza halifanani na hayati Nyerere.

Sanamu lililozinduliwa makao makuu ya Umoja wa Afrika limewekwa mbele ya jengo la siasa, amani na usalama la Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kuhimiza umoja na amani.

“Hakuna mtu aliyewahi kumpatia Nyerere, sanamu zote ukiangalia hazifanani naye, hata mtoto mdogo ukimuuliza anaweza kushindwa kumtambua. Sasa sijui wanaochukuliwa si wazoefu au hawajui kazi au hawalipwi,” alisema Magesa Mchenjewu, mkazi wa Ubungo.

Hata hivyo, Madaraka Nyerere, mtoto wa Nyerere alipohojiwa wakati wa uzinduzi wa sanamu hilo, alisema akiwa miongoni mwa wanakamati maalumu iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kusimamia mchakato wa utengenezaji wa sanamu hilo waliipitisha kwa zaidi ya asilimia 90.

“Wanakamati wote tulikuwa na nafasi sawa, hakuna aliyemzidi mwingine, mchakato ulikwenda vizuri, sikumbuki vizuri ni kwa kiasi gani tuliupitisha, lakini ulikuwa ni zaidi ya asilimia 90,” alisema Madaraka.

Akizungumzia changamoto katika uchongaji na ufinyanzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sanaa, Dinnah Enock alisema makosa yanayofanyika ni wasanii kushindwa kufuata kanuni za uchongaji na ufinyangaji.

“Kuna kanuni za kufuata katika utengenezaji wa sanamu, uwiano wa viungo vilivyopo katika picha na hapa tunaangalia sana sura. Tunaangalia ukubwa wa pua, macho, mdomo,” alisema Dinnah.

Sababu sanamu za Nyerere kukosolewa

Alisema kwa binadamu pia ili sanamu liwe zuri, lazima uwiano uwe mzuri katika viungo vyote kama vile kichwa kuendana na ukubwa wa mikono, ukubwa wa macho kuendana na upana wa sura.

“Kama mtu umewahi kumuona inaweka urahisi kwa msanii kukadiria baadhi ya vitu katika sanamu, nadhani wasanii wengi wanaotengeneza hawajawahi kumuona (Nyerere) wanatumia picha, hivyo kuweka ugumu kuhamisha baadhi ya vipengele katika kazi,” alisema Dinnah.

Alitoa mfano wa pua, akisema ukimfahamu mtu unaweza kujua pua yake ni ndefu kiasi gani tofauti na kutumia picha, inaweza kutoa matokeo tofauti katika ukadiriaji.

Alikiri kuwa miongoni mwa waliowahi kushuhudia sanamu za Nyerere zikiondolewa kutokana na kukosa vigezo.

Maneno yake yaliungwa mkono na mmoja wa wachongaji, Vincent Mapunda aliyeeleza mbali na kushindwa kuweka uwiano sawa, pia wakati mwingine baadhi ya vifaa vinavyotumika vinaweza kuwa sababu.

“Kama unachonga kwa mti kuna miti mingine si mizuri inaweza kukupa shida katika umaliziaji, ukipata mti ambao si mzuri unaweza kukupa matokeo hasi,” alisema Mapunda.

Alisema uzoefu juu ya kazi husika na kufahamu kile unachoenda kukifanya inaweza kusaidia.

“Nani anayetengeneza, ana uzoefu kiasi gani, unaweza kuwa humjui unayemtengenezea, lakini kwa sababu ni mzoefu ukaweza kutengeneza kitu sawa na ulichoelekezwa, mbona mara nyingi tunatengeneza sanamu ambazo tunaziona katika picha na zinatoka vizuri?” alihoji Mapunda.

Wenceslaus Ngonyani, ambaye pia ni mchongaji alisema wakati mwingine bajeti inaweza kukupa kile ambacho unastahili na si unachohitaji.

Ukiachana na sababu za kitaaalamu, bajeti yako pia itaamua upate kitu cha aina gani, huwezi kupata kitu cha Sh5 milioni kwa Sh2 milioni kikawa vile ulivyohitaji,” alisema Ngonyani.

Hata hivyo, maoni ya Ally Masoud maarufu Masoud Kipanya, ambaye ni mchoraji wa katuni yapo tofauti.

Kipanya alisema kwa hali ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa kutengeneza sanamu imekuwa kitu rahisi.

Urahisi huo hauhitaji hata mtu halisi kuwapo katika eneo husika, bali picha inaweza kutumika kutengeneza uhalisia.

“Picha ile unayotaka iwe sanamu unaichapisha (print) katika mfumo wa 3D, baadaye 3D hiyo itawekwa katika plastiki laini ambayo baadaye mtu huweza kutumia umbo hilo kutengeneza aina ya sanamu anayoihitaji,” alisema Kipanya.

Alisema teknolojia hiyo haihitaji mtu kuchonga wala kufinyanga, huku akitaja kuwa moja ya sababu ambayo sanamu za viongozi wengine wa nchi mbalimbali kufanana nao.

Taswira ya Sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyowekwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia.

Kupitia njia hii, umbo halisi la kitu kinachotakiwa kutengenezwa kama sanamu linapopatikana, huzamishwa katika uji maalumu ulio kama plastiki laini na baada ya kutolewa, hujazwa uji mwingine kulingana na aina ambayo mtumiaji huhitaji kutumia kwa ajili ya kupata umbo halisi la kitu.

Wakati Kipanya akisema haya, baadhi ya watu pia walikuwa wakihoji kwa nini katika picha, hayati Nyerere amekuwa akipatiwa zaidi tofauti na vinyago.

Flavian Dauda ambaye ni mchoraji, alisema sanaa yao inawapa uwanja mpana wa kutengeneza picha inayobeba uhalisia tofauti na vinyago.

“Katika kuchora ukikosea unaweza kufuta na kurekebisha, lakini katika kuchonga ikitokea sehemu ya shavu umechonga sana ndani ni ngumu kurejesha kipande cha gogo ulichokata,” alisema Dauda.

Katika uchoraji pia wanaweza kutumia projekta na kuionyesha picha katika kitambaa cheupe na kisha kuanza kuchora kwa kufuata picha hiyo.


Si mara ya kwanza

Hii si mara ya kwanza kwa sanamu za hayati Nyerere kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii.

Jambo kama hili liliwahi kushuhudiwa katika utawala wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Sanamu la Mwalimu Nyerere lililopo Chato.

Sanamu la Nyerere lililowekwa katika lango kuu la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato mkoani Geita lilizua mjadala baada ya uzinduzi wa hifadhi hiyo Julai 9, 2019 uliofanywa na Magufuli.

Mjadala uliibuka katika mitandao ya kijamii kuwa sanamu halifanani na mwonekano wa Nyerere.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kupitia video iliyosambaa mitandaoni alisema kama kuna upungufu wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo wenye dhamana ya kuangalia kama ina kasoro, ili ifanyiwe marekebisho.

Sanamu nyingine za Nyerere zinapatikana katika mikoa ya Dodoma (Nyerere Square), Dar es Salaam (Bwalo la Polisi), Mwanza (mzunguko wa Nyerere), Mara (Butiama- karibu na kaburi alilozikwa Nyerere).

Sanamu lililokuwapo jijini Mwanza ni kati ya yale ambayo yalipigiwa kelele na wananchi wakieleza halifanani na Nyerere na baadaye inasadikiwa lilivunjwa.

Akifafanua suala hilo, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine alisema sanamu lililokuwapo eneo hilo liliondolewa kutokana na mabadiliko ya mpango wa maboresho ya makutano.

Mpango huo ulibadili baadhi ya vitu ikiwamo kuweka bustani na kutanua maeneo hayo ambayo zamani yalikuwa madogo.

“Pia barabara hizi zina historia kubwa na hii ya Nyerere ni miongoni mwake, kwani alikuwa akiitumia Baba wa Taifa alipokuwa akienda Butiama, hivyo upo mpango sahihi wa uandaaji wa uwekaji sahihi wa hizo sanamu ambazo zinaendana na hadhi ya sasa,” alisema Constantine.

Basata wafunguka

Ofisa sanaa mwandamizi wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Abel Ndaga alisema kuna sheria inayozungumzia namna ya kutengeza sanamu za Mwalimu Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Alisema bila kufuata taratibu hizo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa namba 18 ya mwaka 2004.

“Ili kutengeneza sanamu hizo huwa kuna kamati inayohusisha pia familia kuanzia hatua za awali na Basata inakuwa mjumbe kwenye kamati hiyo,” alisema Ndaga na kuongeza:

"Wale wanaojitengenezea tu huko mtaani bila kufuata utaratibu ni makosa kwa sababu ndani ya kamati miongoni mwao ni familia ya viongozi hao, ili wathibitishe inafanana au haifanani na baba yao.