Sita wadakwa wakituhumiwa kutorosha madini, Sh97 milioni Shinyanga

Thursday August 11 2022
DHAHABU PIC

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha fedha ambazo zilikamatwa kwa watuhumiwa sita wanaodaiwa kutorosha fedha hizo na madini aina ya dhahabu.

By Suzy Butondo

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kupatikana na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 930.88 yaliyokuwa yakitoroshwa pamoja na zaidi ya Sh97.02 milioni na mzani mmoja wa kielektroniki wa kupimia dhahabu pamoja na mashine moja ya kupimia ubora wa dhahabu.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Alhamisi Agosti 11, 2022 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi amesema watu hao walikamatwa jana saa 3 usiku huko katika barabara ya Ilogi kuelekea mkoa jirani wa Geita kata ya Bugarama halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoa wa Shinyanga.

Magomi amesema askari polisi wakiwa katika doria walilitilia mashaka gari aina ya Toyota Land Cruiser rangi ya njano na kulisimamisha ndani ya gari hilo walikuta watu sita baada ya kupekuwa wakishirikiana na idara zingine za serikali wakifanikiwa kukuta madini hayo na fedha tasilimu.

Kamanda Magomi amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watuhumiwa walikuwa wakitorosha madini hayo kwenda nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kodi na tozo za serikali, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

"Taratibu za kipolisi kama wasimamizi washeria zitakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani, hivyo ndugu wanahabari jeshi lapolisi mkoa wa Shinyanga linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye maeneo yao ilihatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa haraka," amesema kamanda Magomi.

"Naomba nitoe rai kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za kutafuta kipato kupitia biashara ya madini wafuate. Sheria zilizopo hatimaye kuinua kipato cha familia na pato la Taifa kwaujumla,” amesema.

Advertisement

Kiasi hicho cha madini kimekamatwa ikiwa ni mwendelezo wa ukamataji wa madini hayo, ambapo, Januari 4, 2019, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilikamata watuhumiwa watatu waliokuwa na dhahabu kilo 323.6.

Mbali ya dhahabu hiyo, watuhumiwa walikutwa na Sh305 milioni ambazo hazikuelezwa mara moja zilikuwa zinapelekwa wapi.

Hata hivyo, baadaye polisi wanane waliohusika katika kuwakamata watuhumiwa hao, nao walikamatwa kwa madai ya kufanya mpango wa kuwatorosha watu hao.

Januari 12, askari hao walifikishwa mahakamani kwa makosa 12 likiwemo la uhujumu uchumi. 

Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Gwae Sumaye, na mawakili wa serikali Castuse Ndamgoba, Robert Kidando na Jackline Nyantori.

Advertisement