Soko la mahindi janga jipya kwa wakulima

Monday September 06 2021
mahindi pc
By Waandishi Wetu

Dar/mikoani. Wakati wakulima wakijiandaa na msimu mpya wa kilimo, uhaba wa masoko kwa zao la mahindi umezidi kuwa mwiba na kuathiri maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, Serikali imesema inafanya jitihada za kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Maeneo tofauti hapa nchini yamekuwa na mrundikano wa mahindi, huku hoja ya kupunguzwa kwa bajeti kulikofanywa na Serikali ikizusha mjadala.

Hata hivyo, katika msimu wa 2020/21, Serikali imeeleza kutenga Sh15 bilioni kwa ajili ya manunuzi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Baadhi ya wakulima waliozungumza na Mwananchi wamesema wameathirika kwa kuwa wamelazimika kuuza kwa bei ya hasara chini ya Sh500 kwa kila kilo moja ili kupata pesa ya kuendesha familia zao.


Advertisement

Hali ilivyo mikoani

Mkoa wa Rukwa unategemea kuuza ziada yake ya tani 354,117.42 katika tani 651,433 ilizozalisha, lakini siku chache zilizopita NFRA mkoani hapo imesema itanunua tani 35,000 kwa mikoa ya Rukwa na Katavi.

Hali hiyo pia imeonekana mkoani Kilimanjaro na Njombe, huku Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge akiomba wanunuzi wa ndani na nje ya nchi kutumia soko la mkoa huo wenye ziada ya tani 336,000 za mahindi.


Athari kwa wafanyabiashara

Mfanyabiashara wa Rukwa, Mohamed Mdangwe alisema soko lao kubwa lilikuwa DR Congo na Burundi, lakini kwa sasa hali sio nzuri ya kibiashara ukilinganisha na ilivyokuwa awali.

“Zambia wanazalisha mahindi kwa wingi na wameingia katika soko la DR Congo, hivyo kufanya biashara kuwa na ushindani, sasa wengi wetu tumebaki tunategemea soko la ndani la NFRA, mitaji inakata,” alisema Mdangwe.

Mkulima wa mkoani Katavi, Peter Nguvumali alisema pamoja na Serikali kuanza kununua mahindi Agosti 15, mwaka huu, bado ununuzi ni mdogo na haumnufaishi mkulima.

“Unajua hatuna soko la uhakika tangu wakati wa Serikali ya awamu ya tano hadi sasa, kwa kuwa mnunuzi mkuu wa mazao yetu alikuwa NFRA, lakini wananunua tani chache ukilinganisha na uzalishaji wetu na ziada inayopatikana,” alisema Nguvumali.

Taarifa kutoka mkoani Katavi zinaeleza kuwa kipindi cha awamu ya nne, NFRA ilinunua kati ya tani 50,000 hadi 60,000, lakini ununuzi ulishuka kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kwa mujibu wa takwimu za mkoa huo, uzalishaji mahindi umeongezeka na wamepata tani 585,723, huku ziada ni tani 293,914.

Mbali na Katavi, mkoani Njombe walidai kushuka mauzo, wakisema mwaka jana waliuza tani kati ya 200 hadi 300, lakini tangu uanze msimu huu wa mavuno 2020/21 wameuza chini ya tani 100. Walisema licha ya kufunguliwa mipaka, hali ya kibiashara hairidhishi, hatua iliyoathiri kipato chao.

Daniel Nahumu, mkulima wilayani Siha mkoani Kilimanjaro alisema changamoto hiyo imechagiza wakulima wauze bidhaa hiyo kwa bei ya hasara kwa wafanyabiashara wanaopita mashambani.


Msimamo wa Rukwa

Katibu Tawala Msaidizi wa Kitengo cha Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Rukwa, Ocran Chengula alisema haridhishwi na ununuzi wa tani 3,500, akishauri tani 10,000 kwa bei ya Sh500 kwa kilo.

Mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Rukwa, Deus Sangu alisema mahitaji ya mahindi ni makubwa katika nchi za DR Congo, Sudan Kusini na Kenya imeingia mkataba wa kuwauzia mahindi kutoka nchini.

Sangu, ambaye siku chache zilizopita alishiriki mkutano wa nchi za maziwa makuu alisema; “Tumejadili juu ya changamoto ya soko la mahindi, wenzetu wana mahitaji makubwa na tutafanya nao biashara, kwani tayari Serikali imeingia mkataba na baadhi ya nchi kama DRC, Kenya na Sudan Kusini, huku wakiendelea na mazungumzo na Burundi,” alisema Sangu, ambaye ni mbunge wa Kwela.

Ofisa Kilimo mkoa wa Njombe, Wilson Joel alisema katika msimu wa mwaka jana walizalisha tani 596,634, huku kukiwa na ziada ya tani 423,000. Alisema msimu wa mwaka juzi uzalishaji wa mahindi ulikuwa tani 526,957, ziada ya chakula tani 353,336.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mahindi mkoani Kilimanjaro, Ridhiwani Mfinanga alisema pamoja na masoko ya Himo na Holili kuwa kitovu cha wafanyabiashara kutoka Kenya, Serikali itekeleze ahadi ya kuwa na soko la kisasa la kimataifa la mahindi nchini ili kuwezesha biashara kuwa na tija.

“Soko la mahindi Himo na Holili linategemea mahindi kutoka maeneo yote nchini, ikiwemo Songea, Mbeya, Sumbawanga, Singida, Kiteto, Kateshi na Babati, kikubwa tunachoangalia ni ubora wa mahindi na kwa Kilimanjaro eneo linalolima mahindi mengi ni Siha,” alisema.

Alisema hali ya biashara ya mahindi imeanza kuimarika: “Corona iliteteresha soko la mahindi, baadhi ya wafanyabiashara waliacha kuja na wengine walipoteza mtaji kabisa, lakini kwa sasa tunashukuru, wafanyabiashara wameanza kuingia,” alisema Mfinanga.


Utafutaji wa masoko

Kutokana na changamoto hiyo ya muda mrefu, juhudi mbalimbali za utafutaji wa masoko zimekuwa zikiendelea chini ya NFRA, ambayo imekuwa ikitafuta masoko nje ya nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Agosti 21, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alimuagiza Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo kutafuta masoko ya mahindi kupitia uwakilishi wake katika mashirika ya kimataifa. Nchi nyingine anazowakilisha Kombo ni Albania, Mesodonia, Crotia, Slovania, Serbia na Ugiriki.

“Kwa mfano WFP (Shirika la Mpango wa Chakula Duniani) ni wanunuzi wazuri wa mahindi nchini, kwa hiyo unaweza kufanyia kazi hilo ili kuongeza idadi ya chakula wanachonunua, wakulima wetu wanalima lakini soko hakuna, kwa hiyo ni vizuri uwashawishi wanunue kwa wingi zaidi.”

Kwa mujibu wa tovuti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masoko ‘Research and Market, katika mwaka huu, Afrika Kusini imeporomoka uzalishaji wake kwa asilimia 30, hivyo kuagiza tani 770,000 katika masoko ya nje ya bara la Afrika, hatua iliyoongeza changamoto kwa wazalishaji Afrika, ikiwamo Tanzania.

Ukiachana na Afrika Kusini, Machi mwaka huu thamani ya mahindi yanayouzwa Kenya kutoka Tanzania na Uganda iliporomoka kwa asilimia 73, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Peter Munya akinukuliwa na gazeti la Business daily alidai ilikuwa ni utekelezaji wa sera inayoagiza kuzuia mahindi yenye sumu.

Imeandaliwa na Kelvin Matandiko, Mariam Mbwana (Dar), Joyce Joliga (Ruvuma, Songea), Seif Jumanne (Njombe), Beldina Nyakeke (Mara), Florah Temba (Kilimanjaro) na Mussa Mwangoka (Rukwa, Katavi)

Advertisement