Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Songwe washerehekea mvua mwaka mpya

Muktasari:

Baadhi ya wananchi mkoani Songwe wamesherehekea kuanza kwa mwaka mpya kwa kushangilia kunyesha mvua nyingi wakidai imeashiria mwaka 2022 utakuwa na neema kufuatia ukame ambao umesababisha walio wengi kushindwa kupanda mazao.

Songwe. Baadhi ya wananchi mkoani Songwe wamesherehekea kuanza mwaka mpya kwa kunyesha mvua nyingi wakidai imeashiria mwaka 2022 utakuwa na neema kufuatia ukame ambao umesababisha walio wengi kushindwa kupanda mazao.

Kwa kawaida Mkoa huu hupata mvua za vuli kuanzia katikati ya Oktoba na kuendelea hali ambayo huruhusu kuanza msimu mpya wa kilimo kwa kupanda mazao mbalimbali, lakini imekuwa tofauti ambapo msimu huu mvua hizo zimekuwa zikinyesha kidogo na kufanya washindwe kupanda mazao.

Mkazi wa Chiwezi katika Wilaya ya Momba, Lacksoni Sichone amesema katika eneo lao imenyesha mvua nyingi iliyoanza jana mchana hadi leo Jumamosi Januari Mosi, 2022 hali iliyomfanya kuamua kwenda kulima licha ya kuwa amekesha kanisani kuupokea mwaka mpya.

"Licha ya ukame uliokuwepo muda mrefu lakini wapo wakulima ambao walikuwa wakipanda kwenye vumbi lakini nilichoshuhudia mimea mingi imeota kwa shida na mingi kutoota hali itakayowalazimu kurudia kupanda" amesema


Mkulima wa kata ya Nyimbili wilayani Mbozi, Joshua kijalo amesema kitendo cha kukosekana mvua hadi mwishoni mwa Desemba, 2021 katika maeneo yao si cha kawaida na ambacho kimeibua hofu miongoni mwao ya kutojua hatima ya maisha iwapo mvua haitanyesha, lakini kutokana na mvua iliyonyesha jana kwa muda mrefu inaleta tumaini.

"Tutumie mapumziko ya sikukuu ya mwaka mpya kujitafakari wapi tunekosea na nini kifanyike ili kurejesha hali ya zamani ya kupata mvua kwa muda uliozoeleka" amesema Kijalo

Mmoja wa wauza pembejeo za kilimo katika mji wa Mlowo, Bahati Haonga amesema biashara yake imesimama kutokana na mvua kutonyesha ambapo wakulima hawanunui pembejeo wamechanganyikiwa hawajui cha Kufanya, lakini kutokana na mvua ya leo inatia moyo.

"Kabla ya msimu kukaribia nilikuwa nasikia malalamiko kuwa bei ya pembejeo iko juu na hawakujua watalima vipi, lakini siku za hivi karibuni kilio cha bei ya mbolea kimeisha imebakia watu wanalia kukosekana kwa mvua" amesema Haonga.

Kufuatia kuchelewa mvua za vuli Mkuu wa Mkoa huu, Omary Mgumba amekuwa akiwahamasisha wananchi kuhifadhi vizuri chakula walicho nacho na kupanda mazao yanayostahimili ukame yakiwamo mihogo, mtama na uwele.

Aidha Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) zinasema kutakuwa na upungufu wa mvua za vuli, hivyo kuwataka wakulima kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.