Songwe watakiwa kujenga tabia kunawa mikono kuepuka magonjwa ya mlipuko

Mkuu wa Mkoa Songwe, Waziri Kindamba akionyesha mfano wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa wananchi wa kijiji cha Mbozi leo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kunawa mikono. Picha na Stephano Simbeye
Muktasari:
Afya za watu ziko hatarini kufuatia tabia ya watu kunawa mikono ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko kupungua katika jamii ikilinganishwa na kipindi cha mapambano dhidi ya Uviko-19.
Songwe. Mkuu wa Mkoa Songwe, Waziri Kindamba amesema tahadhari zilizochukuliwa za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 zilisaidia kutokomeza baadhi ya magonjwa ya milipuko katika jamii.
Pia, Kindamba amewataka wananchi katika mkoa huo kujenga tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kuepuka magonjwa yakiwamo ya milipuko.
Amesama kuwa tahadhari ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni iliyochukuliwa wakati huo ilisaidia kutokomeza kipindupindu magonjwa mengine ya kuhara yamepungua.
Kindamba amesema hayo leo Jumamosi Oktoba 15, 2022 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kunawa Mikono Duniani ambayo kimkoa yanafanyika katika Kijiji cha Mbozi kilichopo kata ya Igamba mkoani Songwe.
Amesema “Kunawa mikono na maji tiririka mara kwa mara kutatukinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza na kuwakinga wengine huo ndiyo mpango mzima" amesema RC Kindamba
"Tukumbuke tangu Corona hakuna kipindupindu hii ni ishara kuwa kunawa mikono mara kwa mara kuna nguvu ya kutokomeza maradhi na natumia nafasi hii kuagiza maeneo yote ya mkusanyiko yawekwe kipaumbele cha kunawa mikono" amesema mkuu huyo wa mkoa
Baadhi ya wananchi ambao wameshiriki katika kilele cha maadhimisho hayo wamesema kuwa tangu kupungua kwa ugonjwa wa Uviko-19 wengi wamekuwa hawazingatii tahadhari za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kutokana kukosekana kwa hamasa kama ilivyokuwa wakati wa mapambano ya ugonjwa wa Uviko-19.
Mkazi wa kijiji cha Mbozi Misheni, Kennedy Kamwela amesema watu wameacha kunawa kwa sababu hamasa iliyokuwepo kuacha kutolewa kwa wananchi na hata ulazima wa kuweka ndoo za maji ya kunawa kwenye maeneo ya biashara na mikusanyiko ya watu haupo tena.
"Kukosekana kwa hamasa kumewafanya wananchi wajisahau na kuendelea kuishi kama walivyozoea bila kujali magonjwa ya kuambukizwa" amesema Kamwela.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu Mkoa wa Songwe Dk Boniface Kasululu amesema unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni kunasaidia kupunguza magonjwa ya kuambukizwa kwa asilimia 42 na magonjwa ya mfumo wa hewa kama Uviko 19 na Nimonia kwa asilimia 25.
"Tunasisitiza jamii kujenga utamaduni wa kunawa mikono ili kujilinda na magonjwa ya mlipuko kwani mikono yao ndiyo wakala nambari moja wa kuambukizwa maradhi" amesema Dk Kasululu