Spika ambana Waziri Mabula kuhusu kauli yake kwa Kunambi

Thursday June 23 2022
mabulapiic

Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi Picha na Edwin Mjwahuzi

By Habel Chidawali

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson ametoa mwongozo wa Bunge kuwa maneno aliyoyatumia Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula kwa mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi hayakuwa sahihi.

Spika Tulia ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 23,2022 kuwa lugha iliyotumiwa na Waziri huyo inamdharirisha mbunge na kumpa usumbufu kwa wananchi wake, hivyo akaagiza maneno yaliyotamkwa na Waziri Mabula yaondolewe kwenye kumbukumbu sahihi za Bunge.

Waziri Mabula aliliambia Bunge kwamba Kunambi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jijini la Dodoma, alisababisha migogoro mikubwa ya ardhi iliochangia kuongezeka kwa dhuruma za ardhi kwa wananchi.

Mabula alitoa kauli hiyo wakati akiomba kumpa taarifa mbunge Kunambi kwenye mchango wake ambao ulikuwa ukielezea namna ambavyo Serikali inaweza kupata mapato kwa kupima ardhi.

Kunambi pia alizungumzia mbinu alizotumia kwa kupima ardhi ya jiji akitaka iigwe na serikali ambayo ingemaliza kazi ya kupima ardhi kwa muda mfupi. Lakini baada ya kuelezwa hayo aliomba mwongozo kwa Spika iwapo kauli ya Waziri Mabula inakubalika.

Leo Spika ameeleza kwakirefu kuhusu kilichotokea na kusema Kunambi alikuwa sahihi kutoa kauli hiyo kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya ushauri ambao Serikali ingeweza kuuchukua au kuupuuza lakini si kujibiwa kama ilivyotokea.

Advertisement

Ameonya kuhusu matamshi yanayotolewa ndani ya Bunge kwamba yanaweza kuwaumiza wengine kwa kuwa kumbukumbu za Bunge zinadumu.

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Kunambi amesema kauli ya Spika imeukonga moyo wake na ameamua kusamehe japo ilimuumiza kwa namna moja na kuwaumiza wapiga kura wake.

Hata hivyo, Mbunge huyo amesema ataendelea kuishauri Serikali kwa vyovyote kwa kuwa anaamini siku moja wakimsikia na kutekeleza, Tanzania itasonga mbele kwenye makusanyo.

Advertisement