Spika Tulia aipiga ‘tafu’ Mchas, agawa vitabu 700 Mbeya
Muktasari:
- Vitabu hivyo vimekabidhiwa leo Alhamisi, Mei 18, 2023 kupitia taasisi yake ya Tulia Trust, kwa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Mchas) mkoani hapa, na Maktaba ya Mkoa.
Mbeya. Taasisi ya Tulia Trust imetoa vitabu zaidi 700 kwa ajili ya kuboresha ujuzi wa kitaalam kwa wanafunzi na walimu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Mchas) Mkoa wa Mbeya ambapo kati ya hivyo 500 vimetolewa kwenye Maktaba ya Mkoa.
Akikabidhi vitabu hivyo leo Alhamisi, Mei 18, 2023 kwa Dk Tulia Ackson ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano, Joshua Mwakanolo amesema lengo ni kuchochea elimu ya ujuzi kwenye nyanja ya afya.
“Tumekabidhi vitabu zaidi 700 kati ya hivyo 140 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Mchas) na vilivyosalia ni kwa ajili ya maktaba ya Mkoa ambavyo vinagusa nyanja mbalimbali za elimu hususan masuala mazima ya maharifa kwa watoto, '' amesema.
Mwakanolo amesema kuwa uwepo wa vitabu hivyo kutapunguza hadha ya changamoto zinapojitokeza sambamba na kuboresha mitaala ya elimu, kuanzia elimu ya msingi, Sekondari vyuo.
“Huu ni mwendelezo wa uwekezaji katika sekta ya elimu hususan kwa vyuo vikuu mkoani hapa, kupitia Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust ambapo kwa mwaka jana zaidi ya vyuo vya vitatu vikifikiwa,” amesema.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo, afya na Sayansi Shirikishi Mbeya, Dk Adili Hauled amesema uwepo wa vitabu hivyo utachochea hamasa kwa wanafunzi wanaochukua fani masuala ya afya kufanya vizuri zaidi na kuzalisha wataalam wabobezi.
“Tuna kila sababu kuishukuru taasisi hii, pia Mbunge kwa kuchagua chuo hiki kutuwezesha upatikanaji wa vitabu ambavyo vitakuwa chachu kwa walimu kuandaa mitaala ya kufundisha na wanafunzi kujifunzia,” amesema.
Naye Peter Bugarama, Waziri wa Elimu Serikali ya wanafunzi, ambaye yupo mwaka wa pili akisosomea fani ya utabibu, amesema kitendo kilichofanywa spika huyo ni uzalendo mkubwa na kinachochea ukuaji wa sekta nyeti ya afya.
Naye Mstahiki Meya Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema katika Jiji Dk Tulia anaendele kusaidia Serikali kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, elimu, afya vinavyogusa jamii.