Spika Tulia: Vyombo vya habari toeni nafasi sawa habari za uchaguzi

  • Tulia Ackson akipotea tuzo kutoka kwa waandishi wa Habari akipongezwa kuwa Rais wa Mabunge Duniani(Picha na Hamis Mniha)

Muktasari:

  •  Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuripoti kwa  usawa kwa vyama vyote vya siasa na wagombea wote bila kujali vyama vyao, jinsi au maeneo wanayotoka katika chaguzi za serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amevitaka vyombo vya habari nchini kutoa nafasi sawa wakati wa kuripoti habari za uchaguzi bila kujali chama cha siasa anachotoka mgombea, jinsi yake au mahali anapotoka.

Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 2, 2024 wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani ambayo kwa hapa nchini yamefanyika jijini Dodoma.

Amesema uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 unakuja, hivyo vyombo vya habari vitoe fursa sawa kwa wagombea wote kwenye vyombo vyao bila kujali itikadi zao.

"Tumieni vyombo vyenu vya habari kuwahimiza wananchi wengi wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi ujao ili tupate viongozi wazuri watakaoliongoza Taifa letu," amesema Dk Tulia.

Amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kutoa elimu kuhusu uchaguzi huo kwa sababu sauti yao inafika maeneo mengi zaidi.

Mbali na hilo, amevitaka vyombo vya habari nchini kutoa elimu kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwani wananchi wengi hawajui tofauti ya mambo hayo mawili.

Amesema panapotokea majanga mbalimbali nchini wananchi wanakuwa hawajui chanzo chake kama ni uharibifu wa mazingira au mabadiliko ya tabia nchi.

"Kupitia vyombo vyenu vya habari toeni elimu kuhusu haya mambo mawili, wajue tofauti ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu yanapotokea yanawachanganya wananchi lakini kwa wale waliozaliwa zamani wanajua, maana ukiwauliza watakwambia kuna mwaka hali kama hii ilijitokeza kwa hiyo wanaelewa ni nini kinaendelea," amesema Dk Tulia.

Amesema kuna utafiti uliofanywa unaoonyesha takribani watu milioni 16 maisha yao yanategemea kwenye ukanda wa Pwani, hivyo elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira utasaidia watu hao waendelee kuishi, hasa kwa kutotupa taka za plastiki baharini.

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mambo mengi yamefanyika ili kuhakikisha uhuru wa habari unakuwepo nchini kwani kwa hatua iliyofikiwa sasa, hata kama hayajaisha yote, lakini kuna hatua imefikiwa katika kufikia uhuru wa vyombo vya habari.

Amesema kuna sheria tisa za vyombo vya habari zimeondolewa na hata zile nyingine zilizobaki ambazo bado zinalalamikiwa, zinaendelea kufanyiwa kazi.

Nape amesema vyombo vya habari nchini vimeendelea kubeba ajenda za Serikali kama vile mazingira, matumizi ya nishati safi ya kupikia na uchaguzi.

"Na kama mnavyofahamu jambo likishikwa na vyombo vya habari huwa halikwami," amesema Nape.

Kwa upande wake, Deogratius Nsokolo, rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), amesema bado kuna sheria ambazo zinawakwaza waandishi wa habari katika utendaji wao wa kazi na kuomba zifanyiwe marekebisho ili kuondoa vikwazo hivyo.