SSRA yasaka maoni fao la kujitoa

Mkurugenzi wa Utafiti wa SSRA, Asgar Mushi

Muktasari:

Mamlaka hiyo ilikutana jana na wahariri wa vyombo vya habari nchini kujadiliana juu ya fao hilo ili kuona namna gani wafanyakazi watapata mafao wakiwa kazini au wakistaafu.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikijiandaa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itakayoondoa fao la kujitoa, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (CSSRA) imeanza kukusanya maoni ya wadau kuhusu suala hilo.

Mamlaka hiyo ilikutana jana na wahariri wa vyombo vya habari nchini kujadiliana juu ya fao hilo ili kuona namna gani wafanyakazi watapata mafao wakiwa kazini au wakistaafu.

Mkurugenzi Mkuu wa CSSRA, Irene Kisaka alisema maoni na mawazo hayo yatasaidia kupata utaratibu maalumu kwa wanachama kupata mafao yao.

“Tunataka kurekebisha Sheria ya mwaka 2012 Namba Tano ambayo haikuruhusu kujitoa, kuna baadhi ya mifuko sheria zao hazikuguswa ndiyo zinaruhusu kujitoa, lakini nazo zina masharti magumu,” alisema Kisaka.

Mkurugenzi wa Utafiti wa CSSRA, Asgar Mushi alisema malalamiko waliyopokea kutoka kwa wanachama yanaakisi mabadiliko ya soko la ajira nchini, kwamba wanaweza kuacha au kuachishwa kazi muda wowote.