Stars yajipa mtihani mzito Cameroon

Stars yajipa mtihani mzito Cameroon

Muktasari:

  • Timu ya Taifa ‘Taifa Stars inalazimika kushinda mechi zake mbili za Kundi D kama inahitaji kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan).

Limbe. Timu ya Taifa ‘Taifa Stars inalazimika kushinda mechi zake mbili za Kundi D kama inahitaji kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan).

Taifa Stars ilianza vibaya mchezo wake wa kwanza wa makundi baada ya jana kutandikwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Limbe, Cameroon.

Katika mchezo huo, kocha Etienne Ndayiragije alitumia wachezaji wapya kadhaa kama Baraka Majogoro katika kiungo na Lucas Kikoti, Yusuph Mhilu, Ayoub Lyanga, Edward Charles na Kalos Protus.

Licha ya ugeni wa mashindano makubwa ya kimataifa ya aina hiyo, nidhamu iliyoonyeshwa na Taifa Stars katika kipindi cha kwanza ilishindwa kuonekana kipindi cha pili na kuigharimu Stars.

Kipindi cha kwanza kilikuwa bora zaidi kwa miamba hiyo ya Afrika Mashariki, lakini nafasi kadhaa walizozitengeneza zilishindwa kuzaa matunda.

Nafasi ilityokuwa ya kuitanguliza Taifa Stars kwa bao la kuongoza ilikuwa ya Ayoub Lyanga, ambaye alipata pasi ndefu kutoka winga ya kulia na kuutuliza vizurio ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilipaa.

Zambia walirudi kipindi cha pili wakiwa na mpango wa kufanya mashambulizi ya kushitukiza baada ya kuona kasi ya Taifa Stars inaogopesha kama watapoteza umakini katika ulinzi.

Mabao ya Cillins Sikombe alilofunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 64 baada ya beki Shomari Kapombe kunawa mpira katika eneo la hatari na Emmanuel Chabula yalitosha kuipa usindi Zambia katika mchezo huo.

Na sasa, kocha Ndayiragije atatakiwa kushinda michezo miwili iliyobaki, akianza na ule dhidi ya Namibia utakaochezwa Jumamosi, kabla ya kumaliza na Guinea, Januari 27.

Ni wazi kuwa Taifa Stars inapanda mlipa mkubwa, matokeo kama yalivyokuwa mara ya kwanza waliposhiriki na kutakiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Zambia na kuambilia sare, 2008.