Strategis yapanua wigo, yatinga Dodoma

Naibu Waziri (Ofisi ya Rais), Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi  (wa pili kushoto)  na Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Khadija Said wakifunua pazia ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa tawi la Kampuni Binafsi ya Bima ya Strategis  jijini Dodoma. Kushoto ni ni Ofisa Mtendaji Mkuu (Mali), Jabir Kigoda na kutoka kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu (Bima ya Afya), Dk Malav Manek na Ofisa Mtendaji Mkuu Kiongozi,Dk. Flora Minja.

Muktasari:

  • Kampuni ya Bima ya Strategis imezindua tawi jipya jijini la Dodoma ikiwa na lengo la kuleta manufaa kwa wananchi.

  

Dodoma. Kampuni ya Bima ya Strategis imezindua tawi jipya jijini la Dodoma ikiwa na lengo la kuleta manufaa kwa wananchi.

Miongoni mwa viongozi wa Serikali waliohudhuria uzinduzi huo wa kampuni hiyo binafsi  ya pili kwa ukubwa nchini  ni Naibu Waziri (Ofisi ya Rais ) Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Deogratius  Ndejembi na Naibu Kamishna wa Bima Khadija Issa Said.

 “Kama tunavyofahamu Dodoma ndio makao makuu ya nchi yetu sasa na tayari Serikali imeshahamia jijini hapa kwa ukamilifu. Inapendeza kuona mashirika kama Strategis yanaunga mkono juhudi hizi za Serikali ,” amesema Ndejembi mwanzano mwa wiki katika uzinduzi huo.

 Naibu waziri Ndejembi ameipongeza Strategis kwa hatua hiyo kubwa na yenye manufaa kwa wananchi wanaohitaji huduma ya bima, “mnastahili kuigwa kwa namna yoyote kwa sababu ya utendaji wenu lakini pia ubora wa huduma zenu.”

Ndejembi  amesema kampuni hiyo inastahili pongezi kwa kuhakikisha madai ya wateja yanashugulikiwa ndani ya muda mfupi kama wanavyohitaji wateja huku akitoa wito kwa makampuni mengine ya bima yaige mfano huo.

Amesema hatua ya sasa ya Strategis ni kujikita katika bima za mali na ajali ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi ni nzuri na kutoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kukata bima na sio kusubiri wakati wa majanga tu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis, Dk  Flora Minja amesema wana kila sababu ya kujivunia kuhusu kukua kwao katika zaidi ya miaka 20 ya biashara ya bima na ndio maana wameona umuhimu wa kufungua matawi zaidi ili kuwafikia watanzania wengi kwa haraka zaidi.

“Kwa sasa tupo Dar es Salaam, Mwanza, Zanzibar, Arusha na sasa Dodoma,  tawi jipya la Dodoma pia litatumika kuwafikia wateja walioko mikoa ya jirani kwa kuwa  Dodoma panafikika kwa urahisi lakini pia wataendelea kufungua matawi mengine katika siku za usoni kulingana na mahitaji,” amesema Dk Minja.

Amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utendaji hasa katika kushugulikia madai ya wateja ili waweze kuhudumiwa kwa muda mfupi zaidi iwezekanavyo.

Dk Minja amesema awali walijikita sana katika bima ya afya, lakini kwa takribani miaka minne sasa wamepanua wigo wao na kutoa bima za mali na ajali. 

 “Bima hizi zinajumuisha bima za magari, biashara, uhandisi, kazi, usafirishaji mizigo nchi kavu na majini, bima za safari, moto, wizi, fedha na nyinginezo,” 

Amesema mwaka uliopita, ukuaji wa kitengo cha bima za mali na ajali ulifikia asilimia 70 na kwa jumla kampuni ilikuwa kwa takribani asilimia 20.