Sungusungu wapeleka wanafunzi 40 ‘waliokacha’ shule

kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM wilayani Shinyanga, ikiendelea kukagua miradi ya maendeleo katika kata ya Mwamalili. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Jeshi la jadi la Sungusungu limewafuatilia na kuwapeleka shule wanafunzi 40 wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Mwamalili, Manispaa ya Shinyanga baada ya kutoripoti shuleni.

Shinyanga. Jeshi la jadi la Sungusungu limewafuatilia na kuwapeleka shule wanafunzi 40 wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Mwamalili, Manispaa ya Shinyanga baada ya kutoripoti shuleni.

Akisoma taarifa ya shule hiyo Ijumaa Mei 26, 2023 mbele ya kamati ya   utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM wilayani Shinyanga, Mkuu wa Sekondari ya Mwamalili, Colleta Mgatta amesema licha ya wanafunzi hao kupelekwa kwa nguvu na sungusungu kuendelea na masomo lakini bado wanasuasua kuhudhulia darasani.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini, Doris Kibabi amewataka wanafunzi waache utoro na kuiga vitendo visivyofaa yakiwemo mapenzi ya jinsia moja na uvutaji bangi badala yake wahudhulie vipindi vyote vya masomo na kuwa na hofu na Mungu.

"Ndugu zangu idadi hii ya zaidi ya wanafunzi 40 ni kubwa mno tunaomba wazazi muwalete watoto hao waendelee na masomo kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha yao na mtoto akisoma baadaye atakusaidia wewe mzazi lakini mkikaa nae kwamba aolewe ataolewa na umri mdogo atakapopata ujauzito na kutaka kujifungua anaweza kupata ugonjwa wa fistula ama kuhatarisha maisha yake,”

"Niwasisitize wanangu mkawahamasishe wanafunzi wenzenu ambao wanaendekeza utoro mashuleni waache mara moja tabia hiyo waje wahudhulie vipindi vyote kwani kuolewa na kuowa kupo tu mtaolewa na kuowa msiwe na haraka ila malizeni kusoma kwanza na kama kuna watoto wanafunzi  wameolewa ama wanachunga mifugo tunaomba mtupe  taarifa tuwafuatilie mara moja warudi shuleni,"amesema Kibabi

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwamalili akiwemo Herema Patrick amesema wazazi wengi hawana uelewa wa elimu na wanaamini mtoto akiolewa au akichunga mifugo atakuwa ni msaada mkubwa katika familia ndiyo maana wanataka waishie darasa la saba tu ili waendelee na mambo mengine ya kifamilia.

Naye Diwani wa kata hiyo, James Furushi ameishukuru Serikali kwa kupeleka fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo mbalimbali ukiwemo ujenzi wa daraja lililotumia zaidi ya Sh400 milioni pamoja na ujenzi wa choo cha shule ya msingi Ujamaa kata ya Mwamalili.